Mar 2, 2016

Nani kaiua Sekta ya Filamu ya Tanzania?

Afisa kutoka Bodi ya Filamu Tanzania, Wilhad Tairo, akifafanua jambo kwa mfanyabiashara wa duka la Filamu wakati wa Operesheni ya kukagua Bidhaa zisizo na stika za TRA
Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Tanzania, Sylvester Sengerema

HALI ya Sekta ya Filamu ya Tanzania kwa sasa ni mbaya sana. Ninathubutu kusema kwamba sekta hii ipo ukingoni mwa kifo, kilichobaki ni ung’ang’anizi tu. Ikumbukwe kuwa mzunguko wa maisha hufuata hatua nne: kuzaliwa, kukua, kukomaa na kuzeeka kabla ya kifo, ambapo kama hakuna matatizo, tunategemea mwanadamu kufa baada ya hatua hizo.


Kwa hali ya sekta ya filamu ilivyo sasa, wasanii na wadau wa filamu nchini wanapaswa kukaa chini na kutafakari kuhusu hali hii jinsi ilivyofika hapa, kwani hali ni mbaya sana, na baada ya utambuzi wanaweza kufanya kitu fulani na ikazaliwa upya na kufuata tena ngazi hizo. Vinginevyo itabaki historia.

Lakini hata wakati sekta hii ilipokuwa ikikua kwa kasi, thamani ya kazi zetu (filamu) ilikuwa inashuka siku hadi siku na kusababisha zitengenezwe filamu nyingi zisizokuwa na ubora. Soko la filamu limejengwa katika mazingira ambapo linabana sana uwezekano wa kuibuka kwa wasanii, watayarishaji au waongozaji wapya.

Pamoja na kasoro hiyo, bado soko hili lilifikia hatua ya sinema zetu kuuzwa sana mitaani na kuzipiga kumbo sinema kutoka Nigeria na kwingineko, huku wanawake na vijana ndiyo wakiwa wateja wakubwa wa sinema hizi. Kwa sisi tuliokuwa tukibahatika kutembelea nchi za jirani kama Kenya, Congo DRC, Rwanda, Burundi nk. ni mashahidi wakubwa wa jinsi sinema zetu zilivyoteka soko la filamu katika nchi hizo.

Ilifika mahali ukitembelea nchi hizo na wakagundua kuwa wewe ni Mtanzania basi utakuwa katika wakati mgumu sana kwani utaulizwa maswali mengi kuhusu filamu na wasanii wa Kitanzania na wengi wao wakitaka uwape maelezo mengi kuhusu hizo filamu na wasanii. Watazamaji wetu katika nchi za Afrika Mashariki, hasa wazungumza Kiswahili, wakaonekana kuzipenda sana sinema hizi pamoja na kuwepo kasoro nyingi, lakini walikuwa na hamasa kubwa.

Kama zilivyo sinema za Nigeria ambazo alama yake kubwa ya kibiashara ni Kiingereza chao aina ya ‘Pidgin’, Kiswahili cha kisasa cha Tanzania kilikuwa kinazipa utambulisho wa kitaifa filamu hizi.

Pamoja na kufikia hatua hii, Serikali (kupitia idara zake) haikuwahi kufanya tafiti za kina wala kuweka kumbukumbu (data) za kusaidia kutambua thamani halisi ya sekta au soko la filamu nchini. Hili lilikuwa kosa namba moja! Pia kulikosekana udhibiti wa filamu kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kwa njia za kiharamia kama inavyofanyika sasa.

Ndipo yalipoanza malalamiko kuwa Serikali ilikuwa imelala usingizi na kutoitilia maanani sekta hii ambayo ingeweza kuwa suluhisho kubwa la ajira kwa vijana wengi, chanzo cha mapato ya nchi na ingesaidia kutangaza vivutio vya nchi na hivyo kuvutia watalii wengi na kuliingizia taifa pesa nyingi kupitia utalii.

Na serikali ilipokuja kuzinduka usingizini ikakurupuka kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147, kwa madai ya kutambua uwepo kwa kilio cha muda mrefu cha wasanii na wadau. Ikaipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kazi ya kuweka stempu kwenye DVD za filamu na muziki (pasipo kujua nguvu ya soko) ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi, wakidhani kuwa huko ndiko kuirasimisha sekta ya filamu na kuwa wanawawezesha wasanii kupata kipato stahili kutokana na kazi zao.

Lakini pia tayari kulikuwa kumeshaibuka ubinafsi mkubwa kwenye biashara ya filamu uliokuwa chanzo cha kushuka kwa thamani ya filamu zetu. Ubinafsi wa wasambazaji wa filamu, ambapo waliwagawa wasanii kwenye matabaka ya ‘masupastaa’ na ‘andagraundi’, kisha kuingia mikataba ya kusambaza kazi za wasanii ‘masupastaa’ wale walio kwenye mikataba yao tu na kuwakataa wale wasio kwenye mikataba nao ‘andagraundi’.

Kama hiyo haitoshi, wasambazaji wa filamu wakaanza kuwalazimisha watayarishaji wa filamu kutengeneza sinema zenye sehemu mbili au zaidi hata kama hadithi hairuhusu! Kitendo hiki kilimlazimisha msanii kuigiza awamu ya pili ya filamu (kwa pesa ileile) hata kama hakuwa na lengo la kuigiza sehemu hiyo, jambo lililotafsiriwa kama kuendelea kuwanyonya wasanii kupitia kazi zao kwa malipo kiduchu wanayowalipa.

Baadaye ikazuka tabia ya wasambazaji wakubwa, wenye mtandao mpana kukataa kuuza sinema za wasambazaji wengine wadogo (wanaowatumia wasanii wanaochipukia), hata kama itatokea wasambazaji hao wadogo wataomba wafanyiwe hivyo kwa makubaliano maalum. Hali hii ikasababisha wasambazaji wengine kukosa fursa ya kazi zao kuwafikia watu wengi japo zilikuwa nzuri na zinahitajika mno.

Si hivyo tu, wakashindwa hata kupeana zamu za kusambaza, soko likawa holela lisilokuwa na muongozo huku wakishindwa kutumia soko vizuri, na matokeo yake ikalazimishwa kuwa ili uuze ni lazima kutumia ‘masupastaa’ katika filamu, jambo lililofanya kushindwa kutengeneza wasanii chipukizi wenye nidhamu katika kujenga sekta.

Matokeo yake sekta hii ikawa ni ya kujikimu tu, licha ya ukuaji wa haraka uliokuwa unahubiriwa kwenye majukwaa ya siasa! Hadi leo bado hakuna mavuno halisi katika kukuza pato la Taifa na hata watayarishaji walio wengi hawajafanikiwa kupata matokeo mazuri kiuchumi kupitia filamu.

Sekta hii ikabaki kuwa mfano wa ‘kuganga njaa’ ili mradi mkono uende kinywani. Watayarishaji, wasanii na watendaji wengine wakabaki wakiwa wanaitumia sekta hii kujaribu kuweka mambo yao yaende sawa mezani, kwa maana ya kutafuta jinsi ya kujikimu tu!

Hata hivyo, wasanii ‘masupastaa’ waliokuwa katika mikataba na wasambazaji wakubwa wakaanza kutembelea magari, na kukatokea matabaka huku wasanii chipukizi ‘andagraundi’ wakiwa hawathaminiwi, hapo ndiyo ukawa mwanzo wa kujisahau na matokeo yake sekta ya filamu kukosa vitu vipya. Sanaa ya Tanzania ikageuka kuwa ni kipaji na si taaluma. Japo ni kweli sanaa inaanzia kwenye kipaji, lakini ni taaluma pia. Sanaa inasomewa!

Sanaa kwa Tanzania ikawa ni kati ya fani zisizo na vigezo vya kupima utaalamu na ubora. Kukaanzishwa michakato ya kuibua vipaji vya vijana bila kukazania kusomesha vipaji vya vijana hao. Kila mtu akijisikia anajitangaza msanii! Tena anatengeneza pesa nyingi kuliko wasanii waliokwenda shule. Sanaa ikawa si taaluma bali kitu kinachofanana na taaluma.

Wafanyabiashara wakaanza kuwatumia wale wanaojiita wasanii kwa kujipatia fedha kwa kuuza kazi zao. Wasanii wakawa ni kundi linalofikiri kuwa hawathaminiki kwa kuwa wao wenyewe wameshindwa kujithaminisha kwa kujikomba bila kujua thamani yao.

Kukaibuka utamaduni unaoendelea hadi leo wa wasanii kubwabwaja bila kujua wanabwabwaja nini zaidi ya ‘sanaa ni kioo cha jamii’. Ukiwauliza dira yenu ni nini, hakuna ambaye angeweza kukuambia. Kila mmoja anasema lake. Sekta ya filamu imekosa muongozo, mipaka, miiko na maadili katika utendaji.

Kwa kuwa sanaa ya Tanzania si taaluma bali ni kitu kinachofanana na taaluma ikasababisha kushuka kwa ubunifu miongoni mwa wasanii nchini ambako kumesababisha uwepo wa sinema hafifu isiyoweza kustahimili ushindani wa soko la filamu duniani.

Hata vyama vya wasanii vilivyoanzishwa ambavyo vilitegemewa kujikita katika kuhakikisha ubora wa utendaji wa wanachama unazingatiwa, pamoja na kuwaadhibu wale ambao watabainika kuwa hawakutenda kazi zao kwa mujibu wa sheria vikageuka kuwa vichekesho! Vyama hivi vilitegemewa kuwa nguzo ya kufungua mijadala ya kuleta maendeleo endelevu huku vikifuata na kusimamamia sheria za nchi na hata kudai mabadiliko pale inapobidi.

Lakini vyama hivi vikawa mwanzo wa makundi ya fitina, ugomvi, chuki na hata ukiukaji wa sheria na taratibu za utendaji kazi. Vikabakia kuwa taasisi za kubembeleza wafadhili (mapedejee) watoe hela na kulaumu kutothaminiwa na serikali. Vikajaa unafiki na kuogopana kuambiana ukweli!

Kiukweli sekta ya filamu ya Tanzania imesafiri njia ndefu sana hasa tunapoangalia katika suala la muda, lakini linapokuja suala la ukuaji ili kujilinganisha na maendeleo ya haraka katika sekta za filamu za nchi zilizoendelea duniani, inaonekana wazi kuwa hata yale tuliyokuwa tunadai ni mafanikio tuliyoyapata ni sawa na fizikia ya muda wa safari… Hakuna uhalisia kabisa!

Hebu tujiulize; tumekwenda umbali upi? Ukweli tunaonekana kusimama palepale katika jiwe lilelile lisilotembea (unmovable stone).


Alamsiki.

No comments: