Jan 30, 2013

Kwa hili la Idara ya Utamaduni, tasnia hii itaendelea kuyumba


Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk. Fenela Mukangara

SERIKALI imekuwa ikijinadi kuwa inawajali wasanii ndiyo maana imeamua kuutambua mchango wao kwa kuirasimisha tasnia ya burudani - hasa filamu na muziki – ili wasanii wafaidi jasho la kazi yao, na imekuwa ikionesha kwa vitendo kuwa karibu na wasanii pindi kunapotokea msiba wa msanii maarufu, ingawa bado kuna maswali kadhaa ambayo yanajitokeza na kuleta maswali makubwa zaidi kama kweli inawajali.

Inashangaza kuona kuwa Wasanii ambao Serikali inajigamba kuwajali hadi leo tunapojigamba kuingia kwenye urasimishaji bado hawana sera (ya filamu kwa waigizaji au ya muziki kwa wanamuziki) inayowaongoza katika kufikia mafanikio ya tasnia yao. Pia inashangaza kuona kuwa Idara muhimu ambayo ndiyo uti wa mgongo wa sanaa nchini, ya Utamaduni limekuwa tatizo jingine kubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya sanaa nchini.

Idara hii imekwishahama Wizara zaidi ya kumi toka nchi hii ilipopata Uhuru wake mwaka 1961. Kwanini? Sidhani kama hali hii inatokea tu kwa bahati mbaya. Mwaka 1995 na pia mwaka 2010, Idara hii ilisahauliwa kutajwa wakati wa kutangaza Baraza la Mawaziri baada ya Uchaguzi Mkuu, mwaka 2010 tulipewa taarifa kuwa jambo hilo lilitokea kwa bahati mbaya ingawa mwaka 1995 hapakutolewa maelezo yoyote, ila kimya kimya ikaelezwa kuwa Utamaduni utaendelea kuwa chini ya Wizara ya Elimu.

Kuanzia kipindi cha miaka ya 90, Serikali ilifuta ngazi kadhaa za uongozi katika  Utamaduni, kulikuweko na nafasi ya Kamishna wa Utamaduni ambayo leo hii haiko tena, kulikuweko na nafasi ya Afisa Utamaduni wa Mkoa, nayo haiko tena. Na Maafisa Utamaduni tulionao leo hii, wa Wilaya na Manispaa, hawawajibiki katika Wizara inayohusika na Utamaduni, bali wako chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo ni wizara tofauti kabisa na ile inayohusika na Utamaduni. Kwa wenye uelewa watagundua kuwa hapa pana tatizo kubwa linatokea.

Kama wiki tatu hivi zilizopita nilialikwa kwenye kituo kimoja cha televisheni kwenye kipindi cha asubuhi ambacho hurushwa moja kwa moja, kwenye kipindi hicho nilikuwa nazungumzia kuhusu urasimishaji wa tasnia ya filamu na muziki na kujaribu kuukosoa mfumo uliopo huku nikijaribu kuelezea unaofaa kutumika nchini.

Wakati tukiwa katikati ya kipindi ndipo lilipoibuka suala la Maafisa Utamaduni walioonekana kusahaulika katika mfumo huu wa urasimishaji uliopo sasa. Lawama zilishushwa kwa wasanii kwamba wao hupenda kwenda moja kwa moja Wizarani (kwenye Bodi ya Filamu) na kulithamini Baraza la sanaa La Taifa (Basata) huku wakiwaacha Maafisa Utamaduni ambao ndiyo wako karibu na wasanii na jamii kwa ujumla.

Katika mazungumzo hayo yaliyoibua ukinzani fulani wa mawazo na hoja, nilijaribu kuelezea uelewa wangu kuhusu Maafisa Utamaduni na majukumu yao, ndipo Afisa Utamaduni wa Manispaa moja jijini Dar es Salaam alipopaza sauti akinialika kuwa nimtembelee ofisini kwake kwa mazungumzo zaidi. Sikujivunga, nilimtembelea ofosini kwake siku mbili baadaye.

Nikiwa ofisini kwake tuliongea mambo mengi sana, na alijitahidi kunielezea namna Maafisa Utamaduni wanavyofanya kazi zao na kusisitiza kuwa hizi taasisi zingine zimeamua kupora mamlaka ya Maafisa Utamaduni. Hapa hakumumunya maneno, alikuwa akizilenga Bodi ya Filamu na Basata. Nikakumbuka kuwahi kumsikia Afisa huyo huyo wakati fulani akitamba kuwa yeye hababaishwi na Basata. Nilijiuliza sana wakati ule, kumbe alitamba kwa kuwa hayuko chini ya Wizara ya Utamaduni!

Kwa hali hiyo, shughuli za pamoja za Kitaifa zinazohusu Utamaduni ni ngumu kuzifanya katika mazingira ya sasa, ndiyo maana hata Mashindano ya Kitaifa ya kazi za sanaa hayasikiki tena, hata shughuli zinazohusika na maslahi ya pamoja ya wasanii kama vile ulinzi wa haki za wasanii (Hakimiliki) umekuwa wa shaghalabaghala, maana hakuna ajenda ya pamoja kwa viongozi hawa wanaotegemewa kuwa karibu kabisa na wasanii.

Kwa mujibu wa Afisa wa Utamaduni niliyeongea naye, upokaji huo wa mamlaka kwa Maafisa Utamaduni wa Wilaya umewafanya wao kuwa wakusanyaji wa pato la Wilaya bila kuwa na mchango kwa wadau waliomo katika tasnia mbalimbali za Utamaduni wilayani mwao jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya sanaa, kwa kuwa wao ndiyo walio karibu na wananchi. Pia wamekuwa wakikumbukwa nyakati za Mwenge tu kwa kupewa fedha za kukamilisha shughuli hiyo, jambo ambalo ni tofauti na majukumu yao halisi.

Pia hali iliyopo sasa ya Maafisa Utamaduni kuwa chini ya Idara ya Elimu na Mafunzo iliyo chini ya Afisa Elimu wa wilaya inawafanya wakose gawio la kutosha la bajeti kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya utamaduni badala ya wao kuwa na bajeti maalum kwa ajili ya kushughulikia sekta hiyo muhimu.

Nakumbuka miaka ya nyuma sana, wakati huo nikiwa mdogo, Maafisa Utamaduni walikuwa kimbilio la wasanii, waliweza kutafuta vifaa vya muziki kwa wanamuziki, kutafuta maeneo ya kufanyia mazoezi kwa wasanii wasio na nafasi. Hata yale majumba yaliyojengwa karibu kila wilaya maarufu kama Community Centres yalikuwa chini ya Maafisa Utamaduni na kuwa mahala ambapo serikali ilipajenga maalum kwa ajili ya shughuli za sanaa.

Community Centres hazipo tena baada ya kugeuzwa aidha kuwa ofisi za Manisipaa au kukodishwa kwa watu binafsi kuongeza pato la serikali za mitaa bila kujali vijana waliomo katika Manispaa wanapewa sehemu maalum kufanya shuguli zao za sanaa.

Kwa kukosa sera nzuri ya filamu/muziki, kukosekana kwa Community Centres na mkanganyiko katika Idara ya Utamaduni ni mambo ambayo, tupende tusipende, yanadidimiza sanaa nchini japo serikali inajidai kuwathamini wasanii. Pia ukiangalia Bajeti ya Tamisemi unajiuliza ni asilimia ngapi ya bajeti hiyo huenda katika shughuli za Utamaduni?

Tunasahau kuwa Utamaduni ukilelewa vizuri ni chombo chenye nafasi nyingi sana za ajira, huweza kuongeza pato la eneo husika kwa kuhamasisha maendeleo, huleta uzalendo, ubunifu wa mambo mbalimbali ya Utamaduni, huweza kuhamasisha Utalii katika Utamaduni, na huwa ni sehemu ya Utalii ambayo kwa bahati mbaya sana haijatumika kikamilifu katika kuongeza kipato cha nchi hii kwa ujumla.

Mkanganyiko huu umeifanya sekta ya sanaa kuyumba kwa kuwa inashughulikiwa na wizara tatu tofauti; Wizara ya Viwanda na Masoko, Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, hali ambayo imekuwa ikisababisha migongano ya kiutendaji na ukosefu wa usimamizi wa moja kwa moja wa sekta hii katika wizara moja.

Hali hii imekuwa ikisababisha hata Sera ya utamaduni iliyozinduliwa mnamo Agosti 23, 1997 mjini Dodoma, ikiwa ni hatua ya pili baada ya ile ya kwanza ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962 kuonekana kupuuzwa, si hivyo tu, bali hata huo utamaduni wenyewe unapuuzwa…

No comments: