Jan 3, 2013

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo yatuma rambirambi msiba wa Sajuki


Sadiki Juma Kilowoko (Sajuki) enzi za uhai wake

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, amewatumia salamu za rambirambi, ndugu, jamaa na wasanii wote nchini kufuatia kifo cha msanii Juma Kilowoko (Sajuki) kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Taarifa iliyotolewa leo, jijini Dar es salaam, Wizara ya Habari, Vijana na Utamauni na Michezo imepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha msanii huyo na kuongeza kuwa kifo hicho ni pigo katika tasnia ya filamu hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Kifo chake ni pengo kubwa kwa Serikali, wadau wa tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza nchini kwa ujumla.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Sajuki sina maneno ya kuelezea masikitiko na huzuni niliyonayo, kwani kifo chake ni pigo katika tasnia ya filamu za michezo ya kuigiza” alisema Dk. Mukangara.

Dk. Mukangara amewataka ndugu, jamii na wasanii wote kuwa wavumilivu na watumilivu wakati wote wa msiba na kumuombea marehemu makao mema kwa Mwenyezi Mungu.

Sajuki ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma. Alianza kujihusisha na masuala ya maigizo alipojiunga na kikundi cha Kaole na baadaye kuanza kuigiza filamu. Filamu ya kwanza kucheza ni ile ya Revenge  ya Kampuni ya RJ.

Mwaka 2008 aliamua kuanza kutengeneza kazi zake mwenyewe ambapo filamu yake ya kwanza itwayo Two Brothers  kwa kushirikiana na Shija Deogratious ilitoka. Sajuki baadaye aliamua kuanzisha kampuni yake iitwayo WAJEY Production Company ambapo alitengeneza filamu nyingi zikiwemo Mboni Yangu, Round, Briefcase, Kijacho, Kozopata, Mchanga na Keni, 077 nk. 

Sajuki alifanikiwa kucheza michezo ya kuigiza na filamu na wasanii wengi wenye majina hapa nchini, amebobea katika Uigizaji, Utayarishaji na Uongozaji wa filamu.

Alianza kuugua mwaka 2010 na hali ilizidi kudhoofu mwaka 2011, ambapo alikwenda kutibiwa nchini India. Wadau wengi wa tasnia ya filamu walifanikiwa kutoa michango mbalimbali iliyomwezesha Sajuki kupata matibabu yake. Alirudi na kuonekana kapata nafuu kidogo jambo ambalo lilileta matumaini na  furaha kwa Watanzania; aliporejea tu aliweza kutoa filamu iitwayo Kivuli huku filamu nyingine ikiwa katika hatua ya utengenezaji.

Aidha hali yake ilibadilika jambo lililolazimu alazwe katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili hadi umauti ulipomkuta usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013.

Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi Amen

Imetolewa na:
Mkurugenzi
Idara ya Habari (MAELEZO).
Dar es Salaam.
2 Januari 2013

No comments: