Jan 2, 2013

Kifo cha Sajuki chaacha simanzi nzito


Sajuki, enzi za uhai wake

Watu wengi wamepokea taarifa ya kifo cha Msanii maarufu wa filamu nchini Tanzania Sadiki Juma Kilowoko au Sajuki kama ambavyo anajulikana na wengi aliyefariki dunia alfajiri ya kuamkia leo katika hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salam alikokuwa akitibiwa.

Sajuki anajulikana na wengi kwa sinema zake za kashkash alikuwa akiugua maradhi ya muda mrefu mpaka kufikia hatua ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi.

Inaeleweka  kwamba  msanii huyo alikuwa anaugua na maradhi yaliyosababisha uvimbe ndani ya tumbo lake lakini kwa msaada wasamaria wema waliweza kumchangia na kumfanya apate matibabu nchini India ambapo hali yake iliendelea kuimarika na kuwa nzuri kwa afya yake na kurudi Nchini Tanzania.

Sajuki ameacha mjane ambaye pia ni msanii aitwaye Wastara Juma ambaye ni mlemavu wa mguu mmoja ambao ulisababishwa kwa kupata ajali mwaka 2008, siku chache kabla ya ndoa yao. Hata hivyo Sajuki aliamua kumuoa hivyo hivyo kwani alikuwa ameshapeleka posa kwa kina Wastara.

Tukio hilo liligusa hisia za watu wengi na kumchukulia Sajuki kama shujaa na mwanaume mwenye mapenzi ya kweli kwa kitendo hicho alichokifanya.

Mwaka 2011 haukuwa mzuri kwa Sajuki kwani ndio mwaka ambao maradhi yaliyomsumbua muda mrefu yalipamba moto. Inajulikana kuwa Sajuki aliumwa na kufikia kipindi cha kudhoofu mwili wake kitu kilichosababisha wasanii wenzake na watu wengine waanzishe mchango wa kumchangia Sajuki.

Wasanii, wanasiasa, wananchi walifanikisha zoezi hilo na kumfanya aweze kwenda India kwa matibabu zaidi. Alirudi na kuonekana kapata nafuu kidogo jambo ambalo lilileta nyuso za furaha na amani miongoni mwa Watanzania.

Hata hivyo alikuwa hajapona sawa sawa na alikuwa anajiandaa kurudi tena India kwa matibabu zaidi, na hii alikiri kwenye kipindi cha 'Mkasi' kinachoendeshwa na kituo cha televisheni cha EATV.

Sajuki ambaye ni Mngoni ameshacheza maigizo na filamu na wasanii wengi karibia wote wenye majina hapa Tanzania. Sajuki kwa kusaidiana na mkewe walifungua kampuni ya productions kwa ajili ya filamu (movies) za hapa hapa nchini.

No comments: