Mar 28, 2013

Unauza haki yako ili iweje?


Aliyekuwa Afisa Mtendaji wa COSOTA, Yustus Mkinga

SIKU ya Jumanne ya tarehe 26 Machi 2013, ambayo kwangu ilikuwa siku muhimu sana kwani ndiyo siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu, siku hii nilipata maliko wa kuitwa kwenye kikao cha mazungumzo kati ya COSOTA na Viongozi wa Mashirikisho (Muziki, Stadi za Ufundi, Filamu), niliingia kwenye kikao hiki kwa mujibu wa nafasi yangu ya Ukatibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania.

Mazungumzo yetu yalikuwa na ajenda kadhaa ikiwemo kumtambulisha Afisa Mtendaji Mkuu mpya wa Cosota, baada ya aliyekuwepo kumaliza muda wake.

Katika kikao hicho tulizungumza mengi, mojawapo ikiwa ni mchakato wa mabadiliko ya sheria mpya za hakimiliki na hakishiriki. Kama kuna mambo yanayowasumbua wasanii wa Tanzania na watu wengi duniani ni suala la hakimiliki na hakishiriki kwa wasanii na wabunifu wa sanaa kwa ujumla.

Hapa Tanzania, baada ya sheria ya hakimiliki ya mwaka 1966 kuthibitika kwamba ina mapungufu mengi, ndipo mwaka 1999 Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipotunga sheria mpya ya hakimiliki na hakishiriki, namba saba ya mwaka 1999 na ambayo ni sura ya 218 ya sheria za Tanzania (kama zilivyorekebishwa mwaka2002).

Sheria ya hakimiliki na hakishiriki na 7 ya 1999 ina mapungufu kadha wa kadha. wadau waliyaona hayo kuanzia muda mrefu, na kuanzia mwaka 2006 kazi mbalimbali zilifanywa ili kupata mapendekezo ya mabadiliko katika sheria hiyo, mapendekezo yameshapelekwa wizara ya viwanda na biashara, lakini imekuwa bubu. harakati zilianza na kupelekwa mabadiliko hayo kwenye Baraza la Mawaziri kisha Bungeni, lakini kumekuwa na kigugumizi hadi sasa.

Kwa mujibu wa utangulizi wa sheria hii, imeletwa kutengeneza na kutoa manufaa zaidi na ulinzi zaidi wa kazi za wasanii wa kazi zinazolindwa na haki miliki na hakishiriki na zingine zote zinazoendana na hizo.

Chini ya kifungu cha 2(c) cha sheria hii, ambacho kimsingi kinazungumzia madhumuni ya kutungwa kwa sheria hii muhimu kwa maendeleo ya wasanii na watunzi na wabunifu wote katika sekta ya muziki, maigizo na tasnia nyingine nyingi zinazoendana na hizo.
Sheria hii pia ina madhumuni ya kuinua kazi za fasihi na za kisanii pamoja na nyinginezo zinazofanana na hizo.

Kwa mujibu wa sheria hii, kuna makundi makubwa mawili ya haki za wasanii zinazolindwa na sheria hii, ambazo ni haki ya kiuchumi na haki za kitamaduni ambazo mtunzi wa kazi zinazolindwa na sheria hii ana haki nazo.

Haki hizi zina msingi katika mkataba wa kimataifa wa Benne wa mwaka 1883 ambao uliridhiwa na Tanzania tarehe 25 mwezi wa Julai mwaka 1994 na hivyo kwa mujibu wa kanuni za kisheria za kimataifa, Tanzania ina wajibu wa kutimiza yaliyomo katika mkataba huu iliyouridhia.

Kwa mujibu wa sheria hii, chini ya kifungu cha 3(i) cha sheria hii, kazi zinazolindwa na sheria hii ni zile ambazo zimetengenezwa na mtunzi wa Kitanzania au zile ambazo mtunzi wake siyo Mtanzania lakini ana makazi yake ya kudumu hapa nchini au kazi hiyo iliyotengenezwa kwa mara ya kwanza hapa Tanzania au kazi ambazo ni za kusikika na kuona (audio-visual) ambazo mtayarishaji wake ni Mtanzania au makao makuu yake yakutengeneza kazi hizo zipo Tanzania.

Na kwa mujibu wa kifungu cha 3(3) cha Sheria hii wasanii wanaomiliki kazi za kisanii na wana hakishiriki pia watapewa ulinzi na sheria hii. Na kwa mujibu wa kifungu cha nne, msanii ametafsiriwa kama muigizaji, muimbaji, mwanamuziki, mchezaji (dancer) au mtu mwingine anayeigiza, kuchonga au kufanya maonesho jukwaani.

Lakini haki hizi hutofautinana sana kulingana na aina ya sanaa, kwani zipo sanaa ambazo hujumuisha watu wengi hadi kukamilika kwake. Kwa mfano; katika tasnia ya filamu kuna hatua tano katika kukamilisha zao la kazi (filamu) kabla ya kumfikia mlaji. Hatua hizo kwa kitaalam hujulikana kama Development, Pre-production, Production, Post-Production na Distribution.

Pia katika uandaaji wa kazi hizi kuna makundi ya wadau wa aina tofauti: wasanii waigizaji, watunzi wa hadithi, waandishi wa script, waongozaji, watayarishaji wa filamu, wasambazaji na kadhalika. Na baadaye kuna vyombo vya urushaji wa matangazo ya filamu na video kama vile vituo vya televisheni na kampuni kadhaa za usambazaji kazi kwa njia ya Cable.

Katika kila kundi kati ya haya niliyoyataja kuna aina mbalimbali za haki kulingana na ushiriki wa mtu husika. Kwa mfano wasanii waigizaji hulindwa na sehemu ya hakimiliki inayotajwa kama 'Hakishiriki', na hawa kwa kawaida hulipwa moja kwa moja kutokana na nafasi walizoigiza katika filamu, au hulipwa kwa scenes (matukio) kutegemea aina ya mkataba wao na mtayarishaji unasemaje.

Katika kile kinachosemwa kuwa watu wanaibiwa, utaona kuwa wasanii waigizaji hawana cha kuibiwa kwani wanakuwa wameshalipwa na watengenezaji wa filamu. Labda tatizo liwe ni malipo kiduchu wanayopewa na si vinginevyo.

Upande wa watayarishaji wa filamu ambao ndiyo wana jukumu la kuwalipa waandishi wa script, wasanii waigizaji, waongozaji wa filamu na washiriki wengine katika filamu. Hawa hutegemea kupata fedha zao kutokana na malipo wanayopata kwa wasambazaji. Na hapa ndo' penye ugomvi na kelele za kuibiwa.

Watengezaji wa filamu nchini wamekuwa wanalalamika kila mara kuwa wanaibiwa au kuwekewa masharti magumu ambayo yanadumaza tasnia ya filamu ikiwemo kuuza haki zao, kama nilivyoainisha katika makala yangu ya wiki iliyopita.

Kwa sasa imekuwa ni jambo la kawaida kusikia kuwa mtayarishaji wa filamu kauza kazi zake kwa msambazaji, jambo linaloshangaza sana hasa kwa nchi kama hii. Sababu za kushangaza ni nyingi; ya kwanza kubwa ambayo ni kuwa majukumu ya msambazaji yanajulikana wazi kuwa yeye kazi yake inapaswa kuishia kwenye kusambaza kazi husika tu, sasa anaponunua haki zote ndipo inapotia shaka kubwa! Kwa nini anunue haki yako?

Ndiyo maana katika makala yangu iliyopita niliishauri serikali kuingilia kati na kutoa elimu kwa wasanii na watayarishaji wa filamu kwa kuwa imeonekana kuwa wengi hawana uelewa wa haki zao, na wenye uelewa huo wanakwazwa na hali iliyopo sokoni kwa kuwa msambazaji ndiye anayelimiliki soko na mwenye kauli ya mwisho katika kazi yoyote ya filamu.

Kile alichotaka ufafanuzi msomaji wangu kuhusu haki, ambazo nadhani si yeye tu bali kila mdau anapaswa kuzielewa ili kama ataamua kuuza haki zake (ingawa siyo busara) ajue anapoteza nini. Pia hii itaondoa malalamiko ya kuibiwa kazi yanayoendelea kujitokeza. Kwani hata wale ambao kwa sasa wanaojiona wajanja kwa kuuza haki zao kwa msambazaji na kuishia kupewa gari na pesa zinazowasaidia kwa miezi michache, siku 'wakichuja' na thamani yao kupungua nina imani kuwa wataingia kwenye mkumbo wa kulalamikia haki zao.

Kwa kawaida kazi za filamu (kama ilivyo kwenye muziki) zina haki zipatazo kumi ambazo zimetajwa katika kifungu na 9(1) cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya 1999.

Haki hizo ni: (i) Kurudufu kazi, (ii) Kusambaza kazi, (iii) Kukodisha, (iv) Kuonesha hadharani, (v) Kutafsiri, (vi) Kubadili matumizi ya kazi, (vii) Kufanya maonesho ya hadhara, (viii) Kutangaza kazi katika vyombo vya utangazaji, (ix) Kutangaza kwa njia nyingine zozote, na (x)Kuingiza kazi nchini.

Kwa hiyo ukiangalia haki hizo kama zilivyoainishwa utaona wazi kuwa msambazaji kimsingi anahitaji haki mbili tu za mwanzo; yaani kurudufu kazi na kuzisambaza basi. Kwani hizi haki nyingine zinamruhusu mwenye mali (mtayarishaji) aendelee kufaidi matunda ya kazi yake kwa maisha yake yote na kuwaachia warithi wake miaka hamsini mingine baada ya kifo chake.

Kama inavyoeleweka, Sheria ya Hakimiliki ya nchi yetu inasema wazi kuwa hakimiliki hudumu kwa mwenye haki kwa maisha yake yote na miaka hamsini baada ya kifo chake. Kwa nchi kama Marekani wameongeza hadi miaka sabini. Ndiyo maana utaona kuwa kuna kazi nyingi ambazo zinaendelea kuwa maarufu miaka mingi baada ya wenye kazi kufariki, huku zikiwanufaisha warithi wao.

Sasa inapotokea mtu akaamua kuuza haki zake kwa msambazaji basi ajue kabisa kuwa anauza hata zile haki nane zilizobakia ambazo kimsingi hawezi tena kuzitumia, kwa kuwa tayari atakuwa ameshazipoteza.

Hivi ukiamua kuuza kazi zako kwa maana ya kumuachia haki zote msambazaji, unatarajia kuwaachia nini warithi wako, au unataka kubaki na ile sifa tu ya kuwa uliwahi kuwa na kazi? Lakini, kwa nini uuze haki yako?

No comments: