Bayport

Bayport

fofam

fofam

imetosha

imetosha

Ads

Ads

Apr 11, 2013

Ili kudumisha maadili: Tuipe kipaumbele Idara ya Utamaduni


Mkurugenzi wa Utamaduni wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Prof. Hermas Mwansoko, akiongea
jambo katika moja ya shughuli za Idara yake

BAADA ya uhuru Disemba 1961, Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na vijana, mwaka 1962, Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.

Lakini chakushangaza pamoja na umuhimu uliopo katika suala la utamaduni kwa maisha ya watu, bado sera ya utamaduni imepewa nafasi finyu katika serikali yetu tangu ilipoanzishwa wizara ya kushughulikia masuala ya sanaa. Katika kipindi chote tangu mwaka 1962, shughuli za sanaa zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali lakini zimekuwa hazithaminiwi.


Katika duru nyingi za kimataifa, nchi yetu ilipata kusifiwa sana kwa jitihada zake za kushughulikia ukuzaji wa utamaduni. Hata hivyo, kwa hali ilivyo sasa na kama hatua za dhati hazitachukuliwa, kazi iliyofanywa miaka ya nyuma, hasa mara miaka takriban 20 iliyofuata baada ya uhuru, tutajikuta tukuangukia kulekule kwenye maneno aliyoyasema Mwalimu Nyerere ya kuwa kusanyiko la watu wasio na roho; tutapotea na kujikuta tukiwa taifa lisilo na utamaduni wake.

Siyo hilo tu, tutajikuta pia tukiwa taifa lenye raia wasio na mwelekeo, wasiojifahamu, wasio na fahari ya utaifa wao, wasio na umoja, mshikamano au heshima mbele ya mataifa mengine. Utamaduni huipa jamii utambulisho. Sura na haiba ya jamii huweza kueleweka na kuelezeka kutokana na utamaduni wa watu wake.
Utamaduni hurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kupitia lugha, sanaa na imani za kiroho. Mila na desturi wanazofuata, matamasha au sherehe wanazoendesha, mavazi yao, chakula chao na taratibu nyingine za utamaduni wanazofuata huunganisha jamii.

Ingawa sekta ya utamaduni imekuwa katika mfumo wa serikali tangu 1962, nafasi yake katika maendeleo ya taifa bado haijatambuliwa kikamilifu kutokana na sababu nitakazozieleza baadaye. Mipango ya Maendeleo imekuwa ikibuniwa na kutekelezwa bila kujali utamaduni wa wananchi, utamaduni haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inaaminika kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.

Sera ya utamaduni ilizinduliwa Agosti 23 mwaka 1997 mjini Dodoma, na hii ilikuwa ni hatua ya pili muhimu baada ya ile ya kwanza ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962.

Pamoja na kuwepo kwa sera ya utamaduni (ingawa ina mapungufu yake), lakini kuna maswali nimekuwa najiuliza; je, ni Watanzania wangapi wameshafikishiwa machapisho ya sera hii ya utamaduni ili waisome na kuielewa?

Je, ni Watanzania wangapi wameshaelimishwa kikamilifu juu ya sera hii ili waweze kushiriki katika utekelezaji kwa upana wake? Je, vyombo vya habari vimeshirikishwa kwa kiwango gani katika kusaidia msukumo wa wananchi  kuielewa sera ya utamaduni?

Ndiyo maana Watanzania wengi siku hizi hawazingatii, hawazitambui wala kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake katika wimbi hili la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria.

Pamoja na Serikali yetu kujinadi kuwa inawajali wasanii na kuutambua mchango wao kwa kuirasimisha sekta ya sanaa - filamu na muziki, bado kuna maswali mengi yanayojitokeza ambayo hayana majibu.

Inashangaza kuona kuwa Wasanii ambao Serikali inajigamba kuwajali hadi leo tunapojigamba kuingia kwenye urasimishaji bado hawana sera (ya filamu kwa waigizaji au ya muziki kwa wanamuziki) inayowaongoza katika kufikia mafanikio ya tasnia yao. Pia inashangaza kuona kuwa Idara muhimu ambayo ndiyo uti wa mgongo wa sanaa nchini, ya Utamaduni imekuwa tatizo jingine kubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya sanaa nchini.

Idara hii imekwishahama Wizara zaidi ya kumi toka nchi hii ilipopata Uhuru wake mwaka 1961. Kwanini? Sidhani kama hali hii inatokea tu kwa bahati mbaya. Mwaka 1995 na pia mwaka 2010, Idara hii ilisahauliwa kutajwa wakati wa kutangaza Baraza la Mawaziri baada ya Uchaguzi Mkuu, mwaka 2010 tulipewa taarifa kuwa jambo hilo lilitokea kwa bahati mbaya ingawa mwaka 1995 hapakutolewa maelezo yoyote, ila kimya kimya ikaelezwa kuwa Utamaduni utaendelea kuwa chini ya Wizara ya Elimu.

Kuanzia kipindi cha miaka ya 90, Serikali ilifuta ngazi kadhaa za uongozi katika  Utamaduni, kulikuweko na nafasi ya Kamishna wa Utamaduni ambayo leo hii haiko tena, kulikuweko na nafasi ya Afisa Utamaduni wa Mkoa, nayo haiko tena. Na Maafisa Utamaduni tulionao leo hii, wa Wilaya na Manispaa, hawawajibiki katika Wizara inayohusika na Utamaduni, bali wako chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo ni wizara tofauti kabisa na ile inayohusika na Utamaduni. Kwa wenye uelewa watagundua kuwa hapa pana tatizo kubwa linatokea.

Kwa hali hiyo, shughuli za pamoja za Kitaifa zinazohusu Utamaduni ni ngumu kuzifanya katika mazingira ya sasa, ndiyo maana hata Mashindano ya Kitaifa ya kazi za sanaa hayasikiki tena, hata shughuli zinazohusika na maslahi ya pamoja ya wasanii kama vile ulinzi wa haki za wasanii (Hakimiliki) umekuwa wa shaghalabaghala, maana hakuna ajenda ya pamoja kwa viongozi hawa wanaotegemewa kuwa karibu kabisa na wasanii.

Kazi za Maafisa Utamaduni wa Wilaya zimekuwa ni ukusanyaji wa pato la Wilaya bila kuwa na mchango kwa wadau waliomo katika tasnia mbalimbali za Utamaduni wilayani mwao jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya sanaa, kwa kuwa wao ndiyo walio karibu na wananchi. Pia wamekuwa wakikumbukwa nyakati za Mwenge tu kwa kupewa fedha za kukamilisha shughuli hiyo, jambo ambalo ni tofauti na majukumu yao halisi.

Pia hali iliyopo sasa ya Maafisa Utamaduni kuwa chini ya Idara ya Elimu na Mafunzo iliyo chini ya Afisa Elimu wa wilaya inawafanya wakose gawio la kutosha la bajeti kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya utamaduni badala ya wao kuwa na bajeti maalum kwa ajili ya kushughulikia sekta hiyo muhimu.

Nakumbuka miaka ya nyuma sana, wakati huo nikiwa mdogo, Maafisa Utamaduni walikuwa kimbilio la wasanii, waliweza kutafuta vifaa vya muziki kwa wanamuziki, kutafuta maeneo ya kufanyia mazoezi kwa wasanii wasio na nafasi. Hata yale majumba yaliyojengwa karibu kila wilaya maarufu kama Community Centres yalikuwa chini ya Maafisa Utamaduni na kuwa mahala ambapo serikali ilipajenga maalum kwa ajili ya shughuli za sanaa.

Community Centres hazipo tena baada ya kugeuzwa aidha kuwa ofisi za Manisipaa au kukodishwa kwa watu binafsi kuongeza pato la serikali za mitaa bila kujali vijana waliomo katika Manispaa wanapewa sehemu maalum kufanya shuguli zao za sanaa.

Kwa kukosa sera nzuri ya filamu/muziki, kukosekana kwa Community Centres na mkanganyiko katika Idara ya Utamaduni ni mambo ambayo, tupende tusipende, yanadidimiza sanaa nchini japo serikali inajidai kuwathamini wasanii. Pia ukiangalia Bajeti ya Tamisemi unajiuliza ni asilimia ngapi ya bajeti hiyo huenda katika shughuli za Utamaduni?

Tunasahau kuwa Utamaduni ukilelewa vizuri ni chombo chenye nafasi nyingi sana za ajira, huweza kuongeza pato la eneo husika kwa kuhamasisha maendeleo, huleta uzalendo, ubunifu wa mambo mbalimbali ya Utamaduni, huweza kuhamasisha Utalii katika Utamaduni, na huwa ni sehemu ya Utalii ambayo kwa bahati mbaya sana haijatumika kikamilifu katika kuongeza kipato cha nchi hii kwa ujumla.

Mkanganyiko huu umeifanya sekta ya sanaa kuyumba kwa kuwa inashughulikiwa na wizara tatu tofauti; Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, hali ambayo imekuwa ikisababisha migongano ya kiutendaji na ukosefu wa usimamizi wa moja kwa moja wa sekta hii katika wizara moja.

Hali hii imekuwa ikisababisha si Sera ya utamaduni tu kupuuzwa, bali hata huo utamaduni wenyewe unapuuzwa…

No comments: