May 9, 2013

Malalamiko ya wizi wa kazi za Sanaa: Tuwe na elimu endelevu kuhusu mikataba


Biashara ya filamu huambatana na matangazo kama inavyoonekana kwenye picha hii

MAPEMA wiki hii nilipata nafasi ya kuhudhuria warsha ya siku tatu ya wadau wa filamu iliyokuwa na lengo la kutafuta njia nzuri ya namna ya kutatua matatizo ya wasanii na wadau wa filamu badala ya tabia iliyojengeka ya kumtafuta mchawi jambo ambalo limekuwa halitusaidii.

Warsha ilitokana na kilio cha muda mrefu cha wasanii kudai kuibiwa kazi zao huku baadhi ya waliokuwa wakisukumiwa lawama wakiwa ni wamili wa maktaba za video na wenye mabanda ya kuoneshea video. Warsha hii pia ilikuwa na kusudio la kuangalia mzunguko wa biashara ya filamu nchini kuanzia inapotengenezwa hadi kumfikia mtu wa mwisho (mtazamaji). Warsha hii iliandaliwa na taasisi ya MFDI-Tanzania kwa lengo la kuangalia namna ya kutatua tatizo la usambazaji nchini.

Katika warsha hii tulisikia pande zote zinazohusika na biashara ya usambazaji wa filamu wakiwemo wasambazaji, huku wamiliki wa video library, kumbi za video na machinga wakielezea kwa kina kuhusu kazi zao na changamoto wanazokutana nazo.

Katika kuangalia kwa kina jinsi biashara ya filamu Tanzania inavyokuwa, tuliangalia zaidi changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikitajwa kuwa kikwazo katika tasnia ya filamu nchini, baadhi ni zile ambazo serikali haiwezi kukwepa lawama na zingine zinawahusu wasanii wenyewe na wadau wa filamu, ingawa huwa wanapenda kuitupia mzigo wa lawama serikali pindi kunapotokea matatizo.

Kutokana na warsha hii iliyowakusanya wawakilishi wa wasambazaji wa filamu, mwakilishi wa wenye maduka ya kuuza filamu, wamiliki wa maktaba za filamu (video library), wamiliki wa mabanda ya video na wauzaji wa mitaani maarufu kama Machinga, huku sisi viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania tukiwa kama waangalizi (observers).

Ingawa warsha ilihusu zaidi biashara ya filamu, nilishindwa kujizuia pale nilipoibua hoja kuhusu kilio cha wasanii kulia kuibiwa kazi zao, hoja iliyoungwa mkono na kuzua maswali mengi. Je, ni kweli wanaibiwa? Na kama wanaibiwa, huwa wanaibiwaje? Je, ni kweli uharamia (piracy) wa kazi za filamu ndiyo tatizo kubwa kwenye tasnia ya filamu nchini? Kama ni kubwa lipo kwa kiwango gani? Hivi, wasanii wanayafahamu kweli matatizo yao ya msingi?

Wakati naibua hoja hii nilikuwa tayari nayajua majibu yake niliyoyapata wakati nafanya utafiti wangu miaka kadhaa iliyopita, na nilitaka kujua mitazamo ya wengine kuhusu suala hili la kilio cha wasani kuibiwa, majibu niliyoyapata hayakutofautiana nay ale ambayo tayari nayafahamu.

Ninatambua wazi kuwa katika biashara yoyote ile siku zote, katika makubaliano ya kazi, ni muhimu sana pande zote kuwa na haki na wajibu wa kila upande katika mkataba wa makubaliano wanaoingia baina ya pande mbili. Katika jambo hili, umakini wa hali ya juu huwa unahitajika sana ili kuepusha upande mmoja kuumizwa.

Inafahamika wazi kwamba katika suala la mikataba ni vyema kushirikisha wanasheria ambao ndiyo wataalam wa mikataba ili kuepuka kudhulumiwa, lakini pia kutokana na viwango vya elimu vya wasanii wengi katika nchi hii, ni muhimu kuwa na wasimamizi (mameneja) wanaoelewa masuala ya mikataba.

Ni vyema wasanii wakatambua kuwa kilio wanacholia cha kuibiwa si kweli, wengi wanaingiaa kwenye mkumbo wa wachache wanaotumiwa na wasambazaji (ambao walishawauzia haki zote) ili ionekane kuwa biashara ya filamu si nzuri na kuleta punguzo la kodi kwa wasambazaji hawa. Na hata kama kuna wizi unaaofanyika, wasanii hawaibiwi bali mikataba wanayoingia ndiyo inayowaponza.

Ili kutatua changamoto hii kwanza wakubali mapungufu yao na pindi wanapoona mikataba kwa lugha ya Kiingereza ambayo inawapa tabu walio wengi, basi ni vyema wakaikataa mikataba hiyo au kuipeleka kwa watu wenye utaalam na lugha hiyo, hasa wanasheria, wasipende kuendekeza njaa.

Warsha hii imenifanyaa nimkumbuke aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa, Ghonche Materego, aliyewahi kusema kwamba ni vyema vyama vya sanaa na mashirikisho kuwa na wanasheria ambao watasimamia shughuli za wasanii wao, ikiwemo kuwaongoza katika kuingia mikataba. Ghonche aliamiani kuwa kwa kufanya hivi, wasanii wataweza kujiamini katika utendaji wa kazi zao, kwani hawatakuwa na wasiwasi wa kunyanyasika pindi washirika wao katika mikataba watakapoonekana wanakengeusha mambo.


Nakubaliana kabisa na Mzee Ghonche lakini sijui kama anafahamu kuwa wasanii wetu wamekuwa hawashauriki, wenye kupenda njia za mkato ili kufanikisha mambo na wanaendekeza njaa, hasa pale wanapotajiwa pesa ambazo wanaamini zitawasukuma kwa wiki kadhaa. Taarifa nilizonazo ni kwamba Cosota na Bodi ya Filamu wana wanasheria waliojitolea na wako tayari kupitia mikataba ya wasanii lakini hakuwa hata msanii mmoja aliyewahi kujitokeza japo hata kuomba ushauri wa kisheria.

Wasanii wengi wamejikuta wakidhulumiwa au kupata malipo madogo kutokana kuendekeza njaa na kuwa na uelewa mdogo katika kuingia mikataba na baadhi ya watayarishaji/wasambazaji wa filamu hapa nchini. Suala la mikataba limekuwa likipuuzwa sana na Watanzania wengi (si wasanii tu), hasa linapokuja suala la kusoma vipengele na kuelewa vinamaanisha nini. Wengi hukimbilia kuangalia sehemu inayotaja pesa tu na wakiona pesa nyingi basi husaini bila hata kujali maeneo mengine muhimu.

Hali hii imemkumba jamaa yangu siku za hivi karibuni ambaye aliamua kuja kuniona ili kupata usaidizi baada ya kulizwa na kampuni moja kubwa ya usambazaji wa filamu. Amejikuta akiingia mkataba mbovu ambao sijawahi kuushuhudia katika maisha yangu. Mkataba wake alionionesha ambao ni wakusambaza kazi yake moja, kwa kuuangalia tu niligundua kuwa ulikuwa umetengenezwa na mwanasheria wa msambazaji huyo kwa jinsi ulivyokuwa umepangiliwa kitaalam lakini katika namna ya ujanja ujanja, tena kwa lugha ya Kiingereza. Kibaya zaidi alipopewa alitakiwa kuusaini palepale na wala hakuruhusiwa kutoka hata nao nje kabla hajausaini, ingawa alipewa nakala ya mkataba huo baada ya kusaini. Hili limekuwa ni tatizo ambalo wasanii wote wanatakiwa kulitatua wenyewe, na wala si suala la kuilalamikia serikali.

Mikataba ya aina hii imesababisha vilio, malalamiko na kesi za ajabu ambazo kimsingi zingeweza kuepukika endapo kungekuwa na umakini kabla ya kuingia mkataba husika.

Bahati mbaya wasanii wetu wamekuwa hawajifunzi kabisa kutokana na makosa ya wengine, kwani inapotokea mwenzao kaingia mkataba wa aina hii utashangaa hata watu wake wa karibu nao hurudia makosa kama hayo, kiasi kwamba suala hili limekuwa kama ni desturi kwa wasanii wetu.

Inakuwa vigumu kuelewa kama wanafanya shughuli zao kwa mazoea na si kitaalam, kwa maana ya kuifanya kazi yao kama ajira yao rasmi ambayo inawaingizia kipato kwa kujikimu na kuendesha maisha yao ya kila siku. Kukubali mikataba isiyo na maslahi kwao imekuwa ni sawa na kujimaliza wenyewe.

Kuhusu maisha duni na kudhulumiwa kwa haki zao, kunasababishwa na ubinafsi, kutokuwa na umoja katika kushinikiza haki zao, kutumia vibaya kile wanachokipata kwa anasa na kutotaka kujifunza juu ya haki zao mbalimbali kutokana na kulewa umaarufu na kukimbilia mafanikio ya haraka haraka.

Wasanii wachache wenye maendeleo ni wale wenye kupenda kuingia mikataba ambayo ama wameipitia kwa umakini au wamepata ushauri wa kisheria kutoka kwa wataalam wa sheria, na huingia mkataba hiyo kwa kila kazi wanazofanya na huwa na nakala za mikataba hiyo. Na ni vizuri zaidi mkataba huu ukawa umepitia mikononi mwa watu wanaoweza kuutafsiri.

Jambo jingine la ajabu ni pale wasanii wengi wanapodai kuwa na mikataba lakini wao wenyewe huwa hawana nakala za mikataba hiyo, na hasa mikataba inayohusu usambazaji wa kazi zao, kuna aina ya ujanja ujanja ambao hufanyika ambapo wasanii wengi huambiwa waache mkataba kwa wasambazaji ili ukasainiwe na mwanasheria na baada ya hapo wengi huwa hawauoni tena mkataba wao.

Tukutane wiki ijayo.

No comments: