May 30, 2013

Vita ya bidhaa bandia ianze na maudhui






KWA siku za karibuni tumekuwa na mazungumzo ya kina kati Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na taasisi zingine kuhusu mpango-mkakati wa nam,naa ya kudhibiti bidhaa bandia na hafifu (counterfeit and substandard) zinazotishia uhai wa soko la kazi za Kitanzania zikiwemo kazi za sanaa (filamu na muziki).

Siku hizi imekuwa si jambo la ajabu kusikia au kushuhudia bidhaa kama nondo za ubora hafifu, betri, TV, mafeni, breki za gari, dawa nk. Jambo hili limekuwa likituumiza mno na sasa tumelishuhudia kwa kasi likivamia sekta ya sanaa kwa kiwango kikubwa na kutishia uhai wa soko la filamu na muziki, hasa kwenye bidhaa kama DVDs, CDs, Tape, Vifungashio (Packaging system) nk, ambazo zinahusiana moja kwa moja na sanaa la filamu. Inaudhi mno pale unaponunua sinema (DVD) unayotegemea kwenda kuangalia nyumbani lakini unapoiweka kwenye deki unaitazama mara moja tu, ukiirudia unagundua kuwa inakwama, na wakati mwingine hugoma hata kabla haijaangaliwa!

Tape ndogo (Min div) zinazotumika kwenye kamera kwa ajili ya kuchukulia picha nyingi ni bandia, na hata vifungashio si imara kabisa. Huu mpango-mkakati unalenga kutafuta wataalam wa kusaidia kugunduaa bidhaa bandia kwani kuna tishio la kuja kukosa maktaba za kazi zetu siku za baadaye, kwa kuwa kazi zote (DVD na CD) zitakuwa hazichezi (zinagoma kuonesha).

Hili ni jambo zuri sana kwa mustakabali wa soko la kazi zetu, lakini bado tunatindikiwa na jambo moja muhimu sana katika kudhibiti kiwango hafifu, jambo hili ni maudhui katika hadithi zetu, kwani nayo yanaonekana kukosa viwango vinavyotakiwa.

Kwa miaka kadhaa, sekta ya filamu Tanzania imeshuhudia utofauti mkubwa kati ya maudhui katika hadithi zetu na kile watazamaji wanachokihitaji, na matokeo yake yameendelea kuyumbisha mikakati ya soko na sera za usambazaji. Maudhui lazima yahusishwe moja kwa moja na mahitaji ya watazamaji ili kuwe na nafasi ya mafanikio kwenye soko.

Maudhui yanayofaa katika kizazi cha leo ni yale yanayokwenda sambamba na watazamaji ndani ya akili zao na kuihusisha jamii moja kwa moja. Mafanikio yanayotokana na maudhui yanategemea sana mmenyuko wa watazamaji, na kujenga maudhui yaliyo kwenye mstari na mwelekeo wa watazamaji na matarajio yao imekuwa vigumu, na sasa inahitajika kwa watayarishaji/ waandishi wa miongozo ya filamu kujihusisha moja kwa moja na mtazamo wa watazamaji katika mazingira waliyomo. Kwa matokeo haya, utafiti ni suala la kupewa umuhimu mkubwa kabla ya kuandaa kazi husika.

Kitu ambacho mtayarishaji/ mwandishi anapaswa kujua kuhusu watazamaji wake ni muhimu sana kwa mafanikio katika biashara ya usambazaji. Kujenga maudhui bila uelewa mkubwa na ufafanuzi kwa walengwa, ni kama kufunga safari ya kwenda mahali bila kufikiria jinsi ya kufika huko. Kama maudhui yako hayakushikamana na aina ya maisha au matarajio ya watazamaji wako, jua umewapoteza.

Kundi la kwanza la watazamaji wa filamu ni la akina mama wa nyumbani, wafanyakazi wa ndani, na vijana wasio na ajira. Kundi la pili ni la watazamaji linalotokana na matokeo ya moja kwa moja ya kituo cha Africa Magic kuonesha filamu kwenye familia za watu wa tabaka la kati na la juu wenye uelewa mpana kwa maana ya kwenda shule.

Na bila shaka kuna kundi la tatu linalotokana na watazamaji Watanzania walio nje ya nchi na Waafrika (hasa wanaojua au kukipenda Kiswahili) katika bara la Afrika na maeneo waliko. Ni muhimu kuelewa kwamba kila moja ya makundi haya ya watazamaji yana muundo na mawazo ambayo ni tofauti sana na kundi jingine.

Utafiti nilioufanya kwa miaka mitatu unaonesha kwamba watazamaji wa filamu za Kitanzania wamegawanyika kama ifuatavyo:
Asilimia 67 ya watazamaji wa filamu hizi wanaishi ndani ya Tanzania, asilimia 25 wanatoka katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, na asilimia 8 wanatoka sehemu zilizobaki za dunia, hasa ambako Kiswahili kinafundishwa au kupewa umuhimu.

Pia ni asilimia 30 ya wakazi wanaoishi mijini ndiyo huangalia filamu za Kitanzania. Takwimu hii inatofautishwa kulingana na umri: Asilimia 50 ya watazamaji hawa ni wenye umri kati ya miaka 10-24, asilimia 30 ni wenye umri kati ya miaka 25-34, asilimia 15 ni kati ya watu wenye umri wa miaka 35-49 na asilimia 5 tu ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50 ndiyo huangalia filamu hizi. Dar es Salaam ndiyo mji unaoongoza kuwa na idadi kubwa ya watazamaji wa filamu ikichukua asilimia 31. Hata hivyo, vijana wadogo ndiyo wenye mazoea ya kwenda kwenye mabanda ya video.

Katika utazamaji filamu hizi, kuna dhana ambayo huendana na mitazamo ya watazamaji (matamanio, maadili, na mtazamo wa mtu binafsi kulingana na uzoefu wake katika kuangalia kazi mbalimbali) na vitu hivi huathiri namna watazamaji wanavyohusiana na dunia inayowazunguka, ikiwa ni pamoja na maudhui.

Kabla hadithi yako haijawafikia watazamaji, tayari mtazamaji atakuwa na picha ya kipi anataka kukiamini na kama hadithi yako imeandaliwa katika mtazamo mzuri, mtu wa aina hiyo huamini na hununua kazi bila kusita. Kama hadithi itaifikia jamii ya watazamaji ambao mtazamo wao utalingana na kisa chako, wigo wake utapanuka, watu watapeana taarifa kwa njia ya neno kwa neno (ambayo ni njia ya ufanisi zaidi kwa mkakati wa soko) na hujenga nidhamu ya utazamaji wa filamu.

Hakuna hadithi inayofanikiwa kama watazamaji hawapati kitu wanachokiamini - na kwa wastani wa filamu 100 za Kitanzania, watazamaji wetu hawataweza na wala hawataona kila kitu wanachohitaji, watachukua na kuchagua kati ya filamu nyingi wanazoziona ili kuridhisha matakwa yao.

Maudhui yanayokubalika sana ni yale yanayosimulia jambo linalofahamika zaidi kwa watazamaji. Hii inaweza kupimwa kwa njia mbalimbali, wengi hasa, utafiti wa msingi unaweza kutusaidia kutambua aina ya hadithi tunazohitaji kuwaambia walengwa, aina ya wahusika tunaowahitaji kutusaidia kwenye hadithi zetu, aina ya watazamaji tunaowahitaji kuwaambia hadithi zetu, na majukwaa sahihi kwa ajili ya kusambaza hadithi zetu. 

Kuwaelewa watazamaji ni hatua moja muhimu sana katika mchakato wa biashara ya filamu. Kubainisha maudhui ili yaendane na matarajio yao ni muhimu sana. Kama huwezi kuambatanisha maudhui yako yaende sambamba na mtazamo wa watazamaji, basi, hadithi itapuuzwa.

Kama mtayarishaji wa filamu, suala la kwanza unatakiwa kuwajengea msingi watazamaji katika maudhui uliyoyakusudia, ukielewa kwamba unaweza kuwa bosi kwenye kampuni yako ya production; LAKINI UNACHOKIFANYA SI KWA AJILI YAKO! NI KWA AJILI YA WATAZAMAJI NA HADITHI ZAO!

Pamoja na ukamilifu wa filamu katika usambazaji mara kwa mara, watazamaji kwa urahisi wanaweza kujiendekeza katika mitazamo yao (indulge their worldviews); wakapuuza kazi ambayo haiwaakisi wao moja kwa moja.

Kuandaa hadithi iendane na ladha ya watazamaji - hasa kwa kuelewa kuwa watazamaji hawataki kubadilishwa mitazamo yao, wanataka kuimarisha mitazamo yao (they want it to be reinforced) - itakusaidia kuanzisha mijadala kuhusu masuala muhimu kwa watazamaji wako.

Vizuri tu kama, utaambatanisha ubora wa kiufundi wa filamu yako uendane na ubora wa watazamaji wako waliouzoea. Hutoweza kufanya biashara - kwa mfano, kuwapa filamu yenye ubora hafifu (low quality film) watazamaji ambao wamezoea kuangalia sinema za kigeni, ambazo  zimetengenezwa kwenye tasnia za filamu zilizoendelea zaidi kwa kiwango cha juu cha ubora.

Alamsiki…

No comments: