Jan 25, 2012

Tungetumia filamu, nyimbo zetu kuhamasisha uzalendo

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi akiwa na wajumbe wa kamati ya kutafuta vazi la taifa, ofisini kwake jijini Dar es Salaam

MWAKA jana tumetimiza miaka 50 tangu tuwe huru, lakini bado jamii ya Kitanzania imeendelea kupoteza maadili, mila na tamaduni zake kila kukicha. Baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana iliundwa mwaka 1962, rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alitamka wazi kuwa Utamaduni ndiyo kiini na roho ya Taifa, na nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.



Miaka hii hamsini ya uhuru tunazidi kushuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili huku tasnia ya sanaa hapa ikionekana kutelekezwa kabisa na serikali yetu bila kujali kuwa tasnia hii imesheheni utajiri mkubwa ambao ungeliingizia taifa hili mapato,
ingawatuna wizara inayohusika na utamaduni. Badala yake kinachoshuhudiwa hivi sasa ni nguvu kubwa inayotumika kutafuta vazi linaloitwa la taifa utadhani ndiyo suluhisho na mmomonyoko huu wa maadili na kupotea kwa tamaduni zetu!



Sera ya utamaduni ilizinduliwa Agosti 23, 1997 mjini Dodoma, hii ilikuwa ni hatua ya pili muhimu baada ya ile ya kwanza ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962. Wizara inayosimamia utamaduni ipo lakini hatuoni mipango yoyote ya kimaendeleo ambayo imekuwa ikibuniwa au kutekelezwa ili kujenga moyo wa uzalendo kwa jamii. Utamaduni umekuwa haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inadhaniwa kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.



Hili la Serikali kutoipa umuhimu tasnia ya sanaa/utamaduni ndiyo sababu ya uchafu na tatizo la maadili tunalolishuhudia katika filamu na nyimbo zetu, kwani kumekosekana uthibiti wa kazi chafu. kwa sasa wizara ipo katika mchakato wa kutafuta vazi ambalo wanaamini kuwa ndilo suluhisho la maendeleo ya nchi na uzalendo kwa vijana. Naamini kuwa wizara inaamini hivyo kwa kuwa hadi sasa pamoja na watu kulalamika kukosekana kwa maadili katika filamu na nyimbo zetu lakini wizara haijawahi kufikiria kuunda kamati.



Kwa nini tunakosa alama ya mfano wa filamu zetu? Hivi tutaendelea kujidanganya hadi lini kuwa alama ya filamu zetu ni Kiswahili kinachozungumzwa wakati lugha hii inazungumzwa pia katika nchi zingine kama Kenya, Rwanda, Kongo na kwingineko? Na bahati mbaya sana ni kwamba majina tunayotumia kwenye filamu zetu ni ya Kizungu!


Kwa nyakati tofauti pia nimewahi kuwasikia viongozi wa serikali wakilalamikia kuhusu maadili katika filamu hizi. Kila kukicha ni filamu za mapenzi peke yake zinazotawala kwenye tasnia yetu au hadithi zisizo na asili yetu tulizonakili kwa wenzetu zenye vitendo na maudhui ya jamii za nje. Kwa nini Wizara haifikirii kutafuta tiba ya kuunda kamati (
kama inavyofanya kwenye nguo) ili watayarishaji wa filamu na wasambazaji wabanwe kutumia visa vyetu wenyewe na aina ya mavazi yetu hadi tuige kutoka kwa wenzetu?



Kwa kweli haya ni maswali muhimu na inabidi kila mdau aliye kwenye tasnia ya filamu na sanaa kwa ujumla anapaswa ajiulize. Tusipokuwa makini tutajikuta tukipita njia potofu na kukipoteza kizazi chetu kwa kuwa njia tunayoenda nayo sasa katika filamu zetu ni ile iliyojengwa juu ya msingi wa wimbi la utandawazi inayoakisi utamaduni wa Kimagharibi. Hata tukisisitizwa kuvaa hiyo nguo inayotafutwa sasa bado haitatusaidia lolote.



Tutake tusitake, ukweli ni kwamba fani yetu ya filamu kwa sasa ipo katika hatari kubwa ya kuporomosha mfumo mzima wa maadili katika jamii zetu kwani watayarishaji na wasanii walio wengi katika tasnia hii wameshapotea njia kwa kutofuata au kutoijua miiko na maadili katika hadithi wanazoandaa, mitindo na maudhui ya hadithi yanaonekana dhahiri kupotosha kulingana na asili yetu, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.



Kama wizara ingefikiria kuwa na kamati ya kuhakikisha maadili kwenye filamu yanazingatiwa na kuhimiza uvaaji wa mavazi ya aina fulani, bila shaka hata hii nguvu kubwa inayotumika kutafuta vazi linaloitwa la Taifa isingekuwa kubwa kiasi hiki, kwa kuwa tungewatumia wasanii hawa hawa kuvaa mavazi tunayoyataka ili kuzitambulisha jamii zetu. Ni kama ilivyo kwa nchi za Ghana, Nigeria, Afrika Kusini, ambazo hazijawahi kuwa na kamati ya kutafuta mavazi bali tumeyajua mavazi yao kwa sababu yamekuwa yanatumiwa sana na wasanii wao kiasi cha kuonekana ni mavazi ya taifa, hata hivyo si kweli kwamba ni mavazi ya taifa, hayo ni mavazi yanayovaliwa na makabila makubwa katika nchi hizo.



Kwa hali hii ya serikali kutoizingatia sekta hii na kukosa udhibiti wa sanaa huku ikituacha tujifanyie tunavyodhani inatufaa ni ishara ya hatari inayoashiria mporomoka si kwa fani hii tu bali kwa jamii nzima ya Tanzania. Hata tukilazimishana kuvaa hilo vazi linalotafutwa sasa bado haitatusaidia kama hatutaangalia mambo haya kwa mapana yake. Je, kama ni kweli hatua zipi zichukuliwe ili kunusuru au kudhibiti tatizo hili?



Ninachoamini ni kuwa sanaa ya filamu ni zao la matokeo ya juhudi za mtayarishaji, watendaji wengine katika kazi ya filamu na wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu na hii kama tanzu muhimu ya utamaduni si kitu kilichoibuka tu.



Hivyo jambo muhimu na la msingi hapa ni kwa Serikali na wadau wote kuzingatia, kuzitambua na kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria. Sanaa ya filamu ni kazi ya ubunifu yenye ufundi na mvuto, inapaswa kutopoteza ubunifu, uasili na kukosa mbinu bora ya uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.



Wizara ingeliangalia sana suala hili la mzalishaji wa filamu anayeumiza kichwa kutafuta mtaji na kuandaa bajeti ya filamu - uandaaji hadi kukamilika - lakini bado hana sauti wala nguvu sokoni, hili ndilo linalochochea mmomonyoko huu wa maadili, kwa kuwa mtayarishaji anatengeneza filamu kwa matakwa ya msambazaji ambaye yeye anaangalia soko tu.



Mtayarishaji wa filamu nchini huwa anafanya kazi kwa shinikizo la woga wa soko! Hana uhakika wa soko lake na endapo atakuwa jeuri basi kuna hatari ya filamu yake kutosambazwa, hivyo kinachobaki kwake ni kuweka mikono nyuma awapo mbele ya msambazaji ili filamu yake isambazwe!



Kwa hali hii maadili yanazidi kupotea kwa kuwa mnunuzi wa mwisho bado hujikuta anafuata mkumbo wa nguvu ya msambazaji bila kujali ubora filamu, kuanzia kwa mtunzi wa hadithi, muigizaji, muongozaji, mazingira na taaluma ya filamu yote! Ananunua filamu kwa mazoea ya majina na hadithi!



Hadi sasa filamu nyingi za Kitanzania au michezo ya kuigiza katika runinga ni vitu vilivyopoteza mwelekeo kwani leo hii inafuata mifumo na mtiririko wa kigeni zaidi kama filamu za Nigeria, Philippine na kwingineko. Yote hii inasababishwa na wavamizi kwenye fani hii waliodhani kuwa mtu akikosa kazi ya kufanya basi kimbilio lake ni kwenye sanaa hasa filamu. Hapa ndipo wizara ingeunda kamati ya kushughulikia mambo haya kwa kuwa athari zake ni kubwa kuliko kukosa vazi linaloitwa la taifa.



Matokeo yake tumejikuta tukiwa na idadi kubwa ya watayarishaji filamu, waandishi wa miswada, waongozaji filamu na waigizaji bandia wasio na misingi wala kanuni za fani husika jambo linalosababisha kazi zetu kuwa sawa na Big G inayoisha utamu kwa muda mfupi, huku watu wenye taaluma na misingi wakitupwa nje ya soko kwa kuwa sanaa siku hizi imekuwa ni biashara isiyozingatia na kufuata maadili ya Taifa.



Alamsiki…

No comments: