Feb 15, 2012

RIP Mwandishi Faraji H. Katalambula Mtunzi wa "Simu ya Kifo"

Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Muhammad Seif Khatib akimpongeza mtunzi wa riwaya Faraji H.H. Katalambula kwa umahiri wake kwenye fasihi. Hii ilikuwa wakati wa uzinduzi wa filamu ya Simu ya Kifo iliyotokana na riwaya yake.


Mwandishi Faraji H. H. Katalambula hayupo tena duniani. Amefariki jioni ya Jumanne wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Mzee Katalambula alikuwa mmoja wa watunzi mahiri wa vitabu kupata kutokea nchini mwetu, atakumbukwa zaidi kwa utunzi wake wa kitabu kilichosomwa sana cha “Simu ya Kifo” ambacho baadaye kilitengenezewa filamu iliyoongozwa na gwiji mwingine wa riwaya, ambaye pia hatunaye, Hammie Rajab.

Taarifa za msiba zilisambazwa na mdogo wa marehemu Gideon Katalambula. Msiba ulikuwa nyumbani kwa Marehemu, Mbagala Majimatitu. Mzee Katalambula alikuwa rafiki yangu, na nimewahi kuandika makala kuhusiana na mazungumzo yetu, kwani alifikiria sana kutengeneza filamu kwa kutumia hadithi zake.

Nakumbuka jinsi riwaya yake ya Simu ya Kifo ilivyoleta msisimko kwa wafuatiliaji wa riwaya za upelelezi. Uandishi wake ulikuwa wa aina yake, akiwa mmoja wa magwiji niliowahusudu hapa nchini, wakiongozwa na gwiji mwingine marehemu Eddie Ganzel.

Faraji Katalambula aliandika pia riwaya zingine, akaingia pia katika tasnia ya filamu. Ametoa mchango mkubwa kwa jamii, na ingawa ameondoka, kama walivyoondoka akina Eddie Ganzel, Hammie Rajab, Ben Mtobwa, A. E. Musiba, Mgeni bin Faqihi, Shaaban Robert, Amri Abedi, Mathias Mnyampala, Agolo Anduru, John Rutayisingwa na wengineo, lakini mchango wake utadumu duniani.

Wengi tutamkumbuka mtunzi huyu wa siku nyingi alifanya vizuri katika tasnia ya uandishi na hata pale hadithi yake ya Simu ya Kifo ilivyoigizwa filamu na kufanya vizuri katika tasnia ya filamu katika tasnia ya filamu ya Swahiliwood.


No comments: