Bayport

Bayport

fofam

fofam

imetosha

imetosha

Ads

Ads

Feb 24, 2012

Tutumie nafasi za kujikosoa kuboresha kazi zetu.

Mmoja wa wasanii wenye mafanikio kisanii nchini Tanzania,
Yvonne Cherryl maarufu kwa jina la Monalisa

HIVI karibuni nilikuwa katika kikao cha wadau saba wa filamu waliopendekezwa kuunda kamati maalum itakayokuwa na lengo kuu la kupitia na kutoa maoni katika filamu zetu, ili kuziboresha na hatimaye kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa filamu kwenye tasnia hii nchini. Kamati hiyo ya watu saba ilipendekezwa na wadau mbalimbali wa filamu kwa kupiga kura kupitia mtandao wa kijamii wa facebook/ Tanzania Film Critics Association.

Ukosoaji wa filamu duniani ni uchambuzi na utathmini wa filamu, iwe kwa mtu mmoja mmoja au kwa pamoja. Kwa ujumla, kazi hii ya ukosoaji wa filamu inaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali kama vile mapitio ya filamu yanayofanywa na waandishi wa habari ambayo huonekana mara kwa mara katika magazeti,
na njia nyingine maarufu, kupitia maduka ya usambazaji, au ukosoaji wa kitaaluma ambapo wasomi na wanataaluma katika filamu hutoa taarifa na nadharia ya filamu na kuchapishwa katika majarida.

Wapitiaji wa filamu hufanya kazi kwenye magazeti, majarida, vyombo vingine vya habari, na machapisho mengine kwenye mitandao, hasa hupitia kazi mpya zilizotoka karibuni au zilizo mbioni kutoka ili kuuhabarisha umma. Kwa kuichambua filamu kitaaluma na kuweka wazi mapungufu na hata mazuri yake hasa kwa filamu ambazo zipo karibuni kutoka inaweza kuwa na impact kubwa katika kile ambacho kama mapitio hayo yatakuwa yenye tija watu wataamua kuitafuta filamu.

Kwa vyovyote vile upitiaji mbovu (poor review) wa filamu au kutafuta makosa tu bila kuangalia mazuri unaweza kusababisha hasara kwa waandaaji husika wa filamu na kuathiri mauzo ya filamu husika, na ndiyo chuki binafsi zinapoanzia.

Katika siku za hivi karibuni, mapitio na ukosoaji wa filamu nchini yamekuwa yakizua mjadala mkubwa, hasa pale wapitiaji na wakosoaji hawa walio wengi wanapoonekana kulenga zaidi katika kutafuta makosa tu na kushindwa hata kuyaona mazuri machache yaliyopo kwenye kazi husika jambo linalowachukiza waandaaji wa kazi hizo.

Kwa kawaida, kama ni mpitiaji au mkosoaji wa filamu, kabla hujaanza kutoa makosa ni lazima kwanza ueleze yale mazuri (hata kama ni moja) uliyoyaona, kisha ndipo ueleze makosa uliyoyaona na kuelekeza namna nzuri ya kuyarekebisha ili mtayarishaji, msanii au muongozaji husika asije akayarudia tena. Hii ni aina nyingine nzuri ya kupeana darasa na inaweza kuwasaidia wasanii ambao hawakubahatika kukaa darasani.

Badala yake tumekuwa tukishuhudia wakosoaji ambao kiukweli hawakosoi bali wanaponda, inawezekana kwa chuki au kwa kutokujua pia. Ndiyo maana hushauriwa kuwa mkosoaji wa filamu lazima awe na elimu ya filamu ili iwe rahisi kwake kuitazama filamu kitaaluma zaidi badala ya kuvutwa na shabiki.

Kuna wale wanaofikiria kuhusu soko la filamu, kwa kutumia utamaduni na vyombo vya habari vya kijamii pamoja na njia za jadi za matangazo, jambo ambalo limekuwa likiwafanya wapitiaji hawa katika ukosoaji kujijengea uhalali ambao hata hivyo hauwafikii wahusika walio wengi.

Bado elimu inahitajika sana nchini kwa watayarishaji, waigizaji, waongozaji na hata kwa wakosoaji wa filamu ili tuweze kuandaa kazi nzuri. Walio wengi wanashindwa kuelewa umuhimu wa kukosoa na kukosolewa, kwani kukumbushana kwa kukosoana ndilo darasa linalohitajika ili kuwafanya wasanii, waongozaji na watayarishaji wetu kukubaliana na jambo hilo linaloleta changamoto.

Lakini pia tunahitaji wakosoaji wenye taaluma ya filamu ambao watakosoa kitaalamu na kuelekeza njia sahihi ya kufanya ili kuboresha, na si hawa walio wengi ambao kazi yao ni kuponda tu bila kuelekeza nini cha kufanya. Hapo tutakuwa tumejenga badala ya kubomoa.

Ukosoaji nchini kwa asilimia kubwa haujasaidia katika kutujengea mfumo mzuri wa kutoa kazi bora, bali umekuwa ni kichocheo cha kuangamiza tasnia hii na kujenga chuki katika ya wakosoaji na wasanii, waandaaji na wadau kwa ujumla.

Upungufu mwingi unaojitokeza mara kwa mara katika filamu zetu wakati mwingine huzua tafrani hizi na zile ama hata wasanii husika kujikuta wakishuka thamani na kudharauliwa. Lakini hapo hapo wakosoaji wamekosa mbinu na wanashindwa kutumia njia sahihi ya kuwaelekeza wasanii hawa ili wajifunze.

Aidha, hii imesababisha, kwa sehemu kubwa, wengi wa wakosoaji filamu kwenye magazeti, televisheni na redio kuonekana wanalenga katika kuzilinganisha kazi hizi na zile zinazotengenezwa katika tasnia zilizoendelea bila kujali mazingira, mifumo na bajeti, na hivyo kujenga chuki. Leo ukosoaji wa sanaa kwa ujumla haushikilii nafasi ya kumwelimisha msanii bali kumbomoa.

Tumekuwa tunashuhudia wanaojiita wakosoaji wasio na simile kuanza kuponda bila hoja zenye mashiko zinazoweza kumsaidia msanii au mtayarishaji. Lakini wanaofikia kuponda kwa maneno hayo kutokana na kazi isiyo na ubora iliyotolewa na mtayarishaji fulani, kwa kiasi fulani tunaweza kuwatetea kuwa wana haki ya kusema hayo kwa sababu mtayarishaji huyo lazima awe amejiandaa kabla hajatoa kazi husika.

Ieleweke kuwa kuna kasumba moja kubwa waliyonayo wasanii/ watayarishaji wetu ambayo mara nyingi husababisha makosa mengi katika kazi nyingi miongoni mwa kazi za sanaa kila zinapotoka, nayo si nyingine bali ni kutopenda kuambiwa ukweli, kurekebishwa na kukosolewa.

Pia wasanii wanaokosolewa wanapong’ang’ania kuangalia mafanikio waliyonayo katika mauzo ya filamu kama kigezo pekee kinachohitajika kufafanua mafanikio kisanii ni kosa, kwani filamu inaweza kuwa imeuza vizuri kutokana na kutangazwa sana lakini isiwe na kiwango kizuri. Mafanikio ni pamoja na kupata tuzo, si hizi tunazopeana zilizobatizwa jina la Red Capert.

Baadhi ya mitandao ya kijamii siku hizi kama vile facebook, twiter na kadhalika, imekuwa ni sehemu ya majukwaa maalum ya kuzichambua na kuzikosoa filamu zetu. Mfano ni ukurasa maalumu wa uchambuzi wa filamu wa Tanzania Film Critics Association katika facebook ambao umeanzishwa ili kutafuta namna nzuri ya kuboresha matumizi ya mapitio ya filamu na kupima mapokeo.

Pia kuna blogu nyingi zimeanzisha fursa na wimbi jipya la wakosoaji wachanga wa filamu (amateur) na hata waliobobea na kutoa maoni yao kuhusiana na filamu zetu. Blogu hizi zinaweza kuzingatia aina moja; muongozaji au mwigizaji, au kuingiza aina tofauti za filamu. Tatizo bado ni kwamba, je, wote tuko katika lengo la kuboresha au wengine nia yetu ni kubomoa?

Kuna baadhi ya wakosoaji wamekuwa wakilalamika kuwa nongwa huibuka pale wanapokosoa filamu za watu fulani, ambapo aliyeigiza katika nafasi fulani habebi vema uhusika wake. Anayekosolewa hivyo kama ni hawa wanaojiita ama kuitwa waigizaji wakubwa mara nyingi huhamaki hata kama si kwa waziwazi, ambapo wakati mwingine hufikia kuanza kumsema vibaya mkosoaji huyo kuwa si lolote, si chochote, anajifanya anajua sana wakati hajui chochote.

Endapo watajua kuwa mkosoaji huyo amesomea fani husika ndiyo nongwa inapozidi zaidi na hata unaweza kusikia wakisema anajifanya msomi au mjuzi wakati hana lolote. Na wengine huenda mbali zaidi kwa kudhani kuwa mafanikio kidogo waliyonayo ya kuendesha gari au kuweka heshima baa ni kigezo cha kazi nzuri au kukubalika.

Kukataa kukosolewa ni kutokana na kuwa wengi wanaamini katika kipaji na si katika stadi na maarifa, ambayo yote haya hupatikana baada ya mtu kupata mafunzo. Ndiyo kipaji hutanguli, lakini kipaji bila kukiendeleza bado hakitusaidii. Kama kweli tunahitaji mapinduzi na maendeleo ya dhati katika sanaa, hatuna budi kukubali kukosolewa kila pale inapoonekana dhahiri kuwa iko haja ya kufanya hivyo, kwani kwa asilimia fulani, wengi wetu hujifunza katika njia hiyo ya kukosolewa.

Lakini pia wakosoaji wawe tayari kuonesha kusifia yale machache wanayoyaona na kuonesha njia sahihi ya kufuatwa ili kuboresha kazi. Tusiishie kuponda tu tukasahau kuwa mfumo huu haujengi bali unabomoa na kuzidisha chuki miongoni mwetu.

Na hata kwa wasanii na watayarishaji wa filamu tukubali kukosolewa na tusijengeane chuki za kijinga na ambazo hazina msingi wowote pindi anapojitokeza mmoja wetu na kutupa ukweli wa hali ilivyo na inavyotakiwa kuwa, kwa masilahi ya soko na tasnia ya filamu ya Tanzania.

Tukumbuke pia kuwa, chuki ni uchafu wa moyo na ni hasara kubwa kuwa nayo, hivyo hata inapoonekana kuwa tumekosolewa kwa kuonewa, tujitahidi kuelezana kwa utaratibu badala ya kutumia hasira, kwani pamoja na yote, hii ni namna nyingine ya kujifunza.

Alamsiki.

No comments: