Mar 2, 2012

Sasa tujikite kutengeneza filamu fupi.

* Zinalipa zaidi kuliko filamu ndefu
Fasta Fasta, moja ya filamu fupi za Watanzania ambayo imefanya vizuri katika soko la kimataifa

WIKI iliyopita katika ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Chama cha Waongozaji wa Filamu Tanzania (Tafida) kiliandaa mafunzo maalum ya siku tatu kwa waongozaji wa filamu nchini, mafunzo yaliyotolewa na wataalam wawili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dodoma. Mafunzo haya yalifungwa na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza, ambao walipongeza sana juhudi hizi za Tafida kuyaandaa.

Lengo kuu la mafunzo haya lilikuwa kujaribu kuongeza uelewa kwa waongozaji wa filamu ambao hawakubahatika kwenda shule za filamu kusomea.

Kwa kweli kwa kiwango fulani chama hiki kimefanikiwa katika lengo lake, kwani nilijaribu kuzungumza na baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo baada ya mafunzo na kuona namna walivyo na uelewa tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Elimu ni jambo zuri sana ingawa kila unapojaribu kuongeza maarifa ndivyo unavyozidi kuuona ugumu katika kufanya kazi, hasa unapolifikiria soko la filamu la hapa nchini linalodhibitiwa na Wahindi.

Hii ilidhihirishwa pia na mshiriki mmoja wa mafunzo hayo aliyeshindwa kujizuia na kueleza hisia zake kuhusu ugumu anaouona hivi sasa wa kufanya kazi kwa kufuata misingi ya uongozaji aliyofundishwa, hasa kwa kuwa soko la filamu nchini limejengwa katika mazingira magumu yasiyoangalia misingi ya uongozaji, weledi wala ubora wa kazi bali huangalia majina fulanifulani.

Mimi pia nimekuwa nikiiona hofu hii ndiyo maana niliwataka washiriki wajifunze misingi ya uongozaji ili waweze kuandaa filamu bora, na si kutegemea soko la filamu linalodhibitiwa na watu wachache. Niliwataka wajaribu kufikiria kutengeneza filamu fupi fupi (short films) ambazo zitafuata misingi yote waliyofundishwa na pia kuzingatia weledi, ambazo naamini zina soko kubwa mno kimataifa na hazina presha kubwa katika kuziandaa kama hizi zinazotegemea soko lililodhibitiwa na watu wachache.

Soko la filamu fupi limejengwa katika misingi imara, hasa mtengenezaji anapaswa kuipeleka filamu yake kwenye matamasha ya filamu ambako huwa hawaangalii majina ya watu bali wanazingatia misingi na weledi. Kupeleka filamu fupi katika tamasha la filamu kwa ajili ya kuonekana ni jambo zuri sana hasa baada ya kazi ngumu ya kuitengeneza ambapo mtengenezaji hutaraji watu waione.

Pengine inaweza kuwa mara ya kwanza kwa watazamaji tofauti ambao si marafiki au familia ambao wanaiona filamu hiyo, na hatimaye mtengenezaji ataweza kuona kama ametengeneza filamu nzuri iliyokidhi matakwa au la, kupitia maoni ya watazamaji wenye kujali misingi. Na hapo ndipo anapoweza kupata wanunuzi na hatimaye kujipatia pesa nyingi kuliko soko hili.

Matamasha ya filamu yamekuwa ni sehemu nzuri zaidi kwa ajili ya kutengeneza mtandao na kumfanya mtengenezaji kujulikana kimataifa, na ukibahatika kuwa mmoja wa washindi wa tuzo, jua itakuwa rahisi kwako kupata pesa (funds) za kutengeneza kitu kikubwa unachohitaji siku zote kwa kuwa utaingia kwenye orodha ya watu wanaoaminiwa, na hapo ndo’ washindi hujua kuwa wapo katika mstari sahihi.

Siku zote soko la filamu fupi limekuwepo na si la ubabaishaji kama hili la hapa kwetu, kwani ukitengeneza kazi nzuri ujue itapata soko tu. Kuna matamasha zaidi ya elfu tano katika sehemu mbalimbali duniani, na idadi huongezeka kila mwaka. Matamasha mengi hutoza malipo ya ada ya kuingia, chochote kuanzia dola 10/ na 50/.

Kabla ya kuingia kwa undani katika kuziangalia sinema fupi, uchunguzi wa tabia ya falsafa unahitajika. Watu wengi wamekuwa wakitumia mamilioni ya pesa kutengeneza filamu ndefu ambazo hata hivyo soko lake bado ni la mashaka makubwa, kwani mtengenezaji hulazimika kwenda kwa msambazaji akiwa mikono nyuma japo ametumia pesa na muda wake mwingi katika kuifanikisha kazi yake hiyo. Na mwisho wa siku anaambulia mikono mitupu au kupewa masharti yasiyomsaidia chochote.

Tusidanganyane, thamani ya kazi za sanaa (filamu) inaendelea kushuka siku hadi siku hapa nchini, hii inatokana na wasambazaji wa filamu waliolihodhi soko hili kutozingatia weledi wala misingi na hivyo kusababisha zitengenezwe filamu nyingi zisizo na ubora. Pia kukosekana kwa tafiti na kumbukumbu (data) zinazowekwa kutusaidia katika kutambua thamani halisi ya tasnia na soko la filamu nchini imekuwa sababu nyingine kubwa.

Soko ya filamu nchini limejikita katika kanuni ya mwenye nguvu ndiye anayefaidi (Darwinism) kitu ambacho ni hatari kwa taifa, kwa sababu pia muundo wa soko letu umekuwa ukishusha hadhi ya utamaduni na sanaa zetu huku serikali ikionekana kulala usingizi wa pono.

Wadau wa filamu wamekuwa wakiilalamikia serikali kutotilia maanani tasnia hii ambayo ingeweza kuwa suluhisho kubwa la ajira kwa vijana wengi, chanzo cha mapato ya nchi na ingesaidia kutangaza vivutio vya nchi na kuvutia watalii wengi ambao wangeliingizia taifa hili pesa nyingi.

Umuhimu wa sinema fupi unaonekana sasa hasa kutokana na ile dhana ya filamu kusemwa kuwa hazifanyi vizuri sokoni kinyume na ukweli ulivyo, tatizo ni kutokuwepo uwazi katika biashara kati ya mtayalishaji na msambazaji. Wamekuwa wanadurufu nakala nyingi zinazofurika sokoni wakati huohuo wakidai eti filamu haziuziki.

Soko la filamu nchini ni kama yalivyo masoko mengine, hutegemea sana taarifa iliyo sahihi, ndiyo maana nimekuwa nikiishauri Serikali ihakikishe taarifa muhimu kuhusu soko la filamu zinapatikana. Ili masoko yaweze kuwa katika ushindani mzuri, wadau wote sokoni wanapaswa kuwa wamepata taarifa sahihi kuhusu madhara yanayoweza kuwakumba kutokana na matendo yao.

Ikiwa baadhi watakuwa na taarifa sahihi zaidi kuliko wengine, hizo tofauti zitasababisha kuwepo na matokeo mabaya. Serikali lazima iingilie kati kwa kutoa taarifa ambazo masoko yanapaswa kuwa nazo, na kuweka mazingira bora zaidi yenye mafanikio na haki.

Nimewahi kuandika kuwa michakato ya masoko mara nyingi hugawanya tena utajiri kwa wingi mno. Kinyume chake, ugawanyaji tena wa rasilimali usiofuata matakwa ya wengi unapofanywa na wachache, hujulikana kama “wizi”. Na hii ndiyo hali halisi ya soko letu la filamu.

Kuna matatizo mengi katika soko la filamu nchini, ugumu na makosa yanayofanya utengenezaji wa filamu kuwa wa gharama kubwa zaidi na kutumia muda mwingi kuliko inavyotakiwa kuwa huku mtengenezaji akiwa hajui atakachopata. Katika kutengeneza Filamu Fupi kuna mambo ya kitaalam yanayoweza kusaidia kutengeneza filamu hizi.

Kwanza kabla hujaamua kutengeneza unatakiwa kutafuta hadithi nzuri.  Kumbuka, kama mtengenezaji wa filamu unasimulia hadithi, hakikisha kuwa unacho cha kusimulia ambacho jamii mbalimbali zitapenda kukifuatilia. Pia elewa kuwa unatengeneza filamu kwa ajili ya soko la kimataifa – kwa ajili ya watu wanaojali zaidi misingi – hivyo simulia hadithi zetu; za Kiafrika ambazo zitawavutia watu wa mataifa mengine kuzifuatilia.

Unaweza kujaribu kuelezea hadithi zenye unyeti fulani, lakini uzoefu wetu unatuambia tusifanye hivyo. Nakumbuka nilipotoa hoja ya kuwataka watengenezaji filamu nchini watengeneze filamu fupi, mmoja wao aliniuliza swali hili: ni nini kitakachomsaidia katika kuifanikisha filamu fupi? 

Jibu langu lilikuwa rahisi... hadithi nzuri na script iliyosukwa vizuri, basi. Hata kama ni filamu ya dakika mbili au saa mbili, bado tunapaswa kuanza na mwongozo-imara (script).

Jibu hili lilikwenda sambamba na swali jingine: ni nini huifanya filamu fupi kuwa ya kuvutia? Naam, sanaa ni kitu cha ajabu sana. Si kila mtu anaweza kuipenda kazi yako. Hii imewahi kutokea hata kwa watu kama Steven Spielberg! Hivyo unachotakiwa ni kuelekeza juhudi na nguvu zako mbele. Ukiwa na script nzuri na mipango sahihi, wote tunaweza kutengeneza filamu nzuri na bora kama tutajipanga ipasavyo.

Kama utatumia muda vizuri ukiisuka script yako kwa kufuata misingi, utengenezaji wa filamu unaweza kuwa rahisi na kwenda vizuri zaidi. Ni rahisi kuhariri stori ikiwa bado katika ukurasa, kuliko kutumia muda mwingi na fedha nyingi kwa kupiga picha vitu ambavyo hutavihitaji baadaye. Na katika utengenezaji wa filamu tunapaswa kuelewa kuwa muda ni fedha. Hivyo tunapaswa kutoa visivyotakiwa kabla ya upigaji picha. Inapendeza pia kuwa na script fupi yenye kueleweka.

Ili kumudu bajeti, jaribu kuwa na eneo (location) moja au mawili ya kupigia picha – huhitaji kuwa na maeneo mengi yasiyoleta tija. Kama huwezi kupata eneo zuri unalohitaji, unaweza kufikiria namna ya kuhariri script yako ili iendane na maeneo uliyopata lakini angalia isiharibu mtiririko wa hadithi.

Katika filamu fupi, huhitaji kuwa na wahusika wengi, kumbuka kuwa kila mhusika na kila tukio lazima viwe na sababu kwenye stori yako, hivyo unapaswa kuwa nao wachache. Jaribu na endelea kuifanya stori yako iwe rahisi na ya kuburudisha zaidi. Kumbuka wazo lako litakusaidia kuonesha kipaji chako na kuonesha namna unavyoweza kuwahadithia wengine kwa kufuatia mtiririko wa kitaaluma: mwanzo, kati na mwisho.

Alamsiki.

No comments: