Mar 21, 2012

Tunamuenzi vipi Mzee Kipara?

. Alitumia sehemu kubwa ya maisha yake katika sanaa
. Aliishi maisha ya mateso makubwa mno kuliko jina lake
Mzee Kipara enzi za uhai wake akiwa kazini

Mzee Kipara wakati akiwa anaumwa 
    “Buriani Mzee Kipara”. Maneno yaliyoanza kusikika siku ya Jumatano ya Januari 11, 2012, baada ya saa 2:00 asubuhi, ambapo Mungu aliichukua roho yake na kumpumzisha na maumivu makali ya muda mrefu aliyokuwa akiyapata.

    Neno Buriani ni neno lililotawala kwenye machapisho mbalimbali zikiwemo wavuti (website), mitandao ya kijamii na blogu mbalimbali na lingeweza kumtoka binadamu yeyote aliyeshuhudia, kufuatilia ama kusoma kwa ukaribu sana kuhusu maisha ya mateso ya Mzee Kipara kabla ya umauti wake.

    Jina lake halisi aliitwa Fundi Said, alikuwa msanii mkongwe katika tasnia ya uigizaji hapa nchini, aliyetumia sehemu kubwa ya maisha yake katika sanaa kabla ya mauti kumfika.

    Mzee Kipara alianza kusikika kwenye maigizo enzi za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo kwa sasa inajulikana kama TBC Taifa, na alifariki dunia katika nyumba aliyokuwa amepangishiwa na kundi lake sanaa la Kaole iliyopo eneo la Kigogo Mbuyuni, jijini Dar es Salaam.

    Kwa mujibu wa mmoja wa waigizaji wa kundi la sanaa la Kaole aliyekuwa akimhudumia Mzee Kipara kabla ya umauti wake, Mariam Athuman maarufu kwa jila la Kalunde, hali ya Mzee Kipara ilikuwa mbaya zaidi siku moja kabla ya kifo chake, yaani Jumanne ya Januari 10, ambapo mzee huyo aliyekuwa na miaka 89, alikata kauli. Kabla ya hapo hali ilikuwa ya kuridhisha sana, ila miguu ndiyo ilikuwa bado inamsumbua.

    Mzee Kipara amefariki na kuacha msiba mkubwa mno kwenye tasnia ya filamu na fundisho kubwa kwa wasanii waliobaki. Ingawa jina lake lilikuwa kubwa kwa maana ya umaarufu lakini alikuwa akiishi maisha ya mateso makubwa mno kuliko jina lake, kufuatia kutelekezwa na wahusika japo kazi aliyoifanya ilikuwa ya kuelimisha na kuburudisha jamii. Amefariki wakati akiwa hawezi hata kugeuka kitandani zaidi ya kukoroma tu.

    Kutokana na chanzo cha uhakika kuhusu maradhi yaliyokuwa yakimsumbua Mzee Kipara na kusababisha mauti yake ni matatizo ya shinikizo la damu (High Blood Pressure) lililosababishwa na moyo kupanuka na kushindwa kufanya kazi, kitaalamu huitwa Congestive Cardiac Failure (CCF). Mzee Kipara alikuwa akilalamika kusumbuliwa na miguu ambayo ilikuwa ikivimba.

    Congestive Cardiac Failure husababisha moyo kushindwa kusukuma damu na maji kutoka chini kwenda juu, hivyo miguu kuvimba na ugonjwa tatizo linaloitwa kitaalamu kama Oedema.

    Mazishi yake yalifanyika Alhamisi ya Januari 12, 2012 saa 10 jioni katika makaburi ya Kigogo, jijini Dar es Salaam na kuhudhuliwa na Waziri wa Afrika Mashariki, Mh. Samuel Sitta, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan na viongozi wengine akiwemo mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Henry Clemens, pamoja na wasanii mbalimbali maarufu na wasio maarufu.

    Kifo chake kimeongeza pengo lililoachwa na rafiki zake waliotangulia aliokuwa akiigiza nao kama; Rajab Hatia ‘Mzee Pwagu’ na Ali Keto ‘Pwaguzi’. Hawa wawili walikuwa na kipindi chao cha ucheshi maarufu kama Pwagu na Pwaguzi ambacho kilitamba sana enzo hizo.

    Historia yake

    Fundi Said au Mzee Kipara ambaye aliishi sehemu nyingi katika Jiji la Dar es Salaam kama; Gerezani, Ilala na Kigamboni, kabla ya mauti kumfika akiwa anaishi Kigogo, lakini asili yake ni Mkoa wa Tabora, akiwa amezaliwa mwaka 1922 katika eneo la Ndala, wilaya ya Nzega.

    Amewahi kufanya kazi kama mkaguzi wa tiketi (TT) wa treni katika reli ya kati kabla hajajitumbukiza kwenye sanaa.

    Mzee Kipara alianza rasmi sanaa mwaka 1964 kwa kufanya kazi za mitaani, kabla ya mwaka 1966 kuchukuliwa na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Akiwa RTD, Mzee Kipara aliigiza katika michezo mingi na kipengele kilichompatia umaarufu zaidi ni ule uigizaji wake wa kujifanya mbabe na mkorofi uliomfanya kujizolea mashabiki lukuki hasa ukizingatia kuwa wakati huo Tanzania ilikuwa na kituo kimoja tu cha redio na mamilioni ya wanachi walikitegemea kwa ajili ya kupata habari mbalimbali na burudani ikiwemo michezo mbalimbali ya uigizaji iliyokuwa ikirushwa wakati huo.

    Hakuishia hapo alikiendeleza kipaji chake alichokuwa amejaaliwa na Mungu ambapo aliweza kuonyesha umahiri katika uigizaji uliompatia umaarufu mkubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

    Kufuatia kuanza kwa vituo vya televisheni nchini mwanzoni mwa miaka ya 90, Mzee Kipara aliingia rasmi katika sanaa ya maigizo kwenye televisheni akiwa katika kundi la sanaa la Splendid lenye makao yake makuu Ilala Bungoni, jijini Dar es Salaam, ambapo michezo yao ilionyeshwa katika kituo cha televisheni cha CTN. Hapo alicheza michezo kadhaa ukiwemo ule wa “Nani Zaidi”.

    Baadaye mwaka 1999, Mzee Kipara akiwa na wasanii wengine; Zena Dilip maarufu kama Bi Sauda, Rasia Makuka, marehemu Rajab Hatia aliyekuwa maarufu kwa jina la Mzee Pwagu na Mama Haambiliki, walijiunga na kundi la sanaa la Kaole ambalo lilipata nafasi ya kurusha michezo yake ya katika kituo cha televisheni cha Independent Television (ITV). Mchezo wao wa kwanza ukijulikana kwa jina la “Hujafa Hujaumbika”.

    Mzee Kipara ametumia sehemu kubwa ya maisha yake katika sanaa ambayo ameienzi hadi wakati akiwa katika siku zake za ugonjwa aliweza kucheza filamu bila kujali maumivu aliyokuwa akiyapata.

    Ni vigumu sana kuzungumzia michezo ya kuigiza kuanzia redioni hadi kwenye televisheni bila ya kutaja jina la Mzee Kipara. Ukiondoa maradhi yake pia umri wake wa miaka 89 umechangia kwa kiasi kikubwa kupata maumivu ya miguu aliyokuwa akiuguzwa na wasanii wa kundi lake la sanaa la Kaole.

    Kuhusu familia

    Kabla ya mauti kumfika Mzee Kipara aliwahi kufanya mahojiano na gazeti moja litolewalo kila wiki kuhusu ilipo familia yake, Mzee Kipara alisema:

    “Nakumbuka nilifiwa na mwanangu Said Fundi niliyezaa na mke wangu wa pili, Zena, mwaka 1980, ilikuwa ni baada ya kuachana na mke wa kwanza aliyeitwa Msimu niliyemuoa mwaka 1970. hakukuwa na taarifa za kuwa na watoto hadi siku moja kabla ya mazishi alipojitokeza kijana mmoja aliyeitwa Fundi Saidi na kudai kuwa ni mtoto wa Mzee Kipara.

    No comments: