Jan 19, 2012

KANUNI ZA BODI: Waziri Nchimbi, ni busara zako tu ndio zitamaliza mgogoro huu

*Vinginevyo tutarajie yaliyotokea Nigeria

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk Emmanuel J. Nchimbi

Muigizaji wa Nigeria, Desmond Elliot

Tasnia ya Filamu ya Nigeria

NOLLYWOOD imekufa! Imekufa kwa sababu ya viongozi waliopewa dhamana ya kuilinda na kulinda maadili kujiingiza katika kuanzisha miradi ya kukusanya mapato bila hata kujali itaathiri vipi soko la filamu la nchi hiyo. Fikiria, kwa sekta ya filamu iliyokuwa inatengeneza sinema mia moja kila mwezi katika siku za nyuma, hivi sasa haiwezi hata kutengeneza sinema saba katika mwezi! Hapa lazima kuna tatizo kubwa; 7/100!  Hakika huko ni kushindwa!



Nollywood kumebakia watu wachache kama Desmond Elliot, Uche Jumbo, Monalisa Chinda, Stephanie Okereke, Emem Isong na wengine wachache wanaojaribu kutoa sinema. Wao wanajaribu kupambana kama mtu mmoja mmoja.
Pia ieleweke kuwa wao ni sehemu ya wasanii tu ambao wanapenda kufanya wakipendacho. Lakini unaweza kuona, wao si watayarishaji wa filamu, ni waigizaji tu.



Hivyo mwisho wa siku, watayarishaji halisi wa Nollywood hawatoi tena sinema. Kwa yeyote anayefuatilia tasnia ya filamu ya Nigeria atakuwa anajiuliza wako wapi kina Chico Ejiro, Zeb Ejiro, Fred Amata, Paul Obasele, Jetta Amata, Teco Benson, Fidelis Duker na wengine? Tujiulize, kwa nini Nollywood imesimama? Kwa nini haifanyi tena sinema katika Lagos? Hata Idumota au Ebinpejo Lane hazisikiki tena katika ulimwengu wa filamu? Kwa asiyejua, haya ndiyo maeneo maarufu ya Nollywood.



Zimebaki sinema chache sana, hasa sinema kutoka katika jamii ya Yoruba. Naomba nieleweke kuwa siandiki haya kwa kujifurahisha au kwa kuwa nina chuki na Taasisi fulani, la, na siandiki haya kwa kuwa nahisi bali naandika kwa kuwa nina taarifa rasmi (official data) kuhusiana na tasnia ya filamu nchini Nigeria. Kama utafuatilia kwa makini utagundua kuwa hakuna tena sinema mpya zinazotoka Nigeria, zinazoonekana ni zile zilizotoka siku nyingi, na wadau wa sinema nchini Nigeria sasa wanailalamikia serikali kuwa ndiye muuaji wa sinema zao. Hasa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu ya Nigeria.



Wanasema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu ya Nigeria aliibuka tu siku moja na kutunga kanuni kandamizi kama zilizoandaliwa hapa kwetu bila hata kuwashirikisha wasanii, watayarishaji wala wadau wa filamu. Kanuni zilizotungwa zilikuwa maalum kwa ajili ya kuwabana wasanii na wasambazaji wa sinema, ili wabaki wachache; kwamba hakuna atakayeruhusiwa kusambaza filamu mpaka kwanza alipe Naira million 5!



Upuuzi ulioje! Hata hao wachache waliokusudiwa kubakia pia wamekimbia! Aina hii ya viongozi ni wale wanaopenda kuvuna pasipo kupanda. Hata ng’ombe wa maziwa huhitaji matunzo kwanza ili aweze kutoa maziwa yaliyo bora na si kufikiria kumkamua tu bila kumlisha! Matokeo yake wamekamua hadi damu imetoka na kumuua ng’ombe mwenyewe, hawajui kesho watakamua nini baada ya ng’ombe kufa. Mtu analala usiku na asubuhi anakuja na kanuni inayotaka watu watoe ada kubwa ambazo wala hazisaidii kulinda maadili, lakini hajiulizi sinema ambazo anazikamua kiasi hiki zinauzwa kwenye soko lipi na mazingira ya soko yakoje?



Badala ya kuhamasisha kwanza soko la ndani na kuwahamasisha wananchi kuwa wazalendo kwa kununua kazi halisi (original) wao wanafikiria kuanzisha miradi tu itakayotunisha mifuko yao, na wakiulizwa wanakuwa wakali huku wakijibu kibabe. Wamesahau kuwa zama za ubabe zimeshapitwa na wakati.



Kuhamasisha soko la ndani ingesaidia kuliinua soko ambalo lingemsaidia mzalishaji wa kazi za sanaa kupata kipato cha kutosha kitakachomuwezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakazomsaidia kuwa na uwezo wa kuuza hata katika soko la nje na hivyo nchi ingepata pato kubwa kupitia filamu.



Kwa maana hiyo, si sahihi kuendelea kusema kuwa Nollywood (tasnia ya filamu nchini Nigeria) bado inashika nafasi ya pili kwa ukubwa katika uzalishaji wa sinema duniani kama ambavyo tafiti za UNESCO zilivyowahi kubainisha wakati fulani. Ki ukweli Ghana ndiyo inayowaokoa waigizaji wa Nigeria kwa sasa, kwa kuwa wao hawana kanuni kandamizi kama hizi.



Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini ilizindua kanuni mpya za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza mjini Musoma mkoani Mara, mnamo Oktoba mwaka jana zilizozinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal. Kanuni hizo zimeainisha adhabu mbalimbali ikiwemo kulipa faini ya papo kwa hapo isiyopungua Shilingi milioni mbili kwa watengenezaji, waoneshaji na wasambazaji wa filamu watakaozikiuka.



Kuzinduliwa kwa kanuni kuliambatana na kauli ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi, kuwataka wote kufuata sheria na kusajiri kazi zao kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao. Waziri Nchimbi alisema Serikali imechoshwa na uwepo wa filamu zisizo na maadili. Lakini naamini kabisa hadi anasaini kanuni hizi hakuwa kazisoma.



Kukosoa kwangu kanuni hizi hakumaanishi kuwa nashabikia kufanya kazi bila udhibiti, la hasha! Lakini wasiwasi wangu ni pale suala la ada linapopangiwa muda wa kawaida na haraka na kiwango cha ada hizi. Nakubaliana na nia njema ya Serikali kutaka kulinda maadili, sina tatizo kama Bodi wana nia ya kulinda maadili katika filamu zetu yasipotoshwe, lakini kwa nini hawataki kukaa na wadau na kuangalia namna ya kupanga ada ambayo itaendana na soko?



Ada zimepangwa kwa kuzingatia muda wa kawaida na wa haraka. Kawaida ni muda gani na haraka ni muda gani? Bodi wanapaswa kuainisha jambo hili ili isije ikawa ukitoa kiasi kikubwa unapata kibali leoleo na ukitoa kiasi kidogo utapata baada ya miezi sita (kawaida)! Hili suala la kuwepo haraka ni jambo litakalochangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa rushwa, na ndiyo shaka yangu inapoanzia; je, ni kweli kanuni hizi zina lengo la kusimamia maadili au ni mradi tu wa kujiongezea mapato? Hivi ni nani aliyeziandaa? Hivi aliyeziandaa alikuwa anajua anachoandika au akili yake ilitekwa zaidi katika kuangalia Bodi itapata (benefit) nini?



Pia kuna mkanganyiko mkubwa kwenye kanuni hizo, mfano kanuni ya 4 kifungu cha kwanza; sina tatizo katika kuwasilisha maombi ya kibali cha kutengeneza filamu mwezi mmoja kabla, lakini mbona haijawekwa wazi, Bodi itachukua muda gani kuyatafakari maombi na kutoa kibali?



Hizi zimeonekana kuwa kanuni za gharama tu mwanzo mwisho, gharama ni nyingi mno, yaani hata chapisho la tangazo litakalobandikwa mtaani litangazalo filamu ama kazi yoyote ya sanaa (poster) linapaswa kulipiwa Bodi shilingi 5,000/! Hii si kazi ya Manispaa? Na vipi kuhusu kulipa ada ya uzinduzi wa filamu au matamasha kwa Bodi sh 500,000/? Haya si majukumu ya Basata na Manispaa? Pia kuna vitambulisho sh 10,000/ kwa kila mtu! Hivi vitambulisho ni vya nini? Kwani Bodi ni chama kama ilivyo Cosota au ni shirikisho kama ilivyo TAFF? Hivyo vitambulisho vitaandikwaje? Waajiriwa au wanachama wa Bodi? Bodi imeamua kupora mamlaka mengine ambayo kisheria yalipaswa kuwa chini ya Shirikisho la Filamu Tanzania.



Suala la ada na michango ni suala tete katika kila kona, lazima tutazame ni kwa kiwango gani gharama zinakidhi faida inayokusudiwa, Bodi inataka pesa ambazo ukizikusanya kwa pamoja ni nyingi mno, lakini haieleweki fedha hizi na michango mingine lukuki zinatumikaje? Kwa manufaa ya nani? Kwa lengo gani?



Tatizo jingine ninaloliona katika hizi taasisi zetu za serikali ikiwemo Bodi ni kutokuwa na nia ya dhati ya kutoa taarifa au kukaa na wadau. Ungetegemea Bodi wangejitahidi kuwemo hata kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook ambako wadau wengi wapo na kanuni hizi zimechukua mjadala mkubwa mno, huko wangesikia na kujibu kinachoendelea. Si wao tu, hata Cosota nayo ni hivyo hivyo, ukiongea nao wana mambo na matarajio mengi, lakini hakuna wanapoyaweka wazi.



Sijui kwa kufanya hivi wanategemea watu waote? Wasanii wakilalamika utasikia, “mmezoea kulalamika!” Cosota wana wavuti (website) lakini imelala usingizi! Halafu wavuti yenyewe ni ya Kiingereza katika nchi ya Waswahili! Hizi ni ofisi zinazoendeshwa kwa kodi zetu, lazima tuseme. Jumatatu ya wiki hii kulikuwa na kikao cha wasanii na wadau wa filamu kuzijadili kanuni.



Kikao hicho kilitawaliwa na kejeli, dharau na majigambo kutoka kwa baadhi ya wasanii waliposimama kuchangia mada zilizotolewa, kwa kweli hali haikuwa shwari kabisa kwa kila aliyesimama kuzungumza lolote kuhusiana na kanuni, karibu kila aliyechangia alitoa kauli moja tu ''Kanuni na sheria hizi hazifai na hatuzitaki!'' Hii ni ishara kuwa mambo yalipofikia yanahitaji busara za waziri katika kunusuru suala hili, endapo Bodi wataendelea kushikilia msimamo wao. Vinginevyo tutarajie machafuko.



Kwa leo naishia hapa…

No comments: