Oct 14, 2017

Miaka 18 baada ya kifo cha Mwalimu Julius K. Nyerere: Je, tunalinda utamaduni wetu kama alivyoamini?


LEO tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 18 tangu Baba wa Taifa na muasisi wa taifa hili, Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999 jijini London, Uingereza na kuzikwa Butiama, kijiji alichozaliwa.

Mwalimu Nyerere alikuwa kati ya viongozi wachache wa Afrika walioacha mwangwi katika utamaduni wa nchi zao.

Nyerere alikuwa mwalimu. Ni sahihi kusema silika ya ualimu iliathiri siasa na matendo ya Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Tanganyika na baadaye Tanzania. Aliiona nchi yake kama darasa na daima alikuwa akiwafundisha watu.

Yapo mengi kuhusu Mwalimu Nyerere lakini ninachosema hapa ni ule mchango wa Mwalimu katika sekta ya utamaduni.

Baada ya Tanganyika kuwa huru Desemba 9 mwaka 1961, Mwalimu Nyerere aliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962.

Wakati akiunda wizara hiyo, alitamka wazi kwamba utamaduni ni kiini na roho ya Taifa akisema nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho hivyo kukosa sifa ya kuitwa Taifa.

Katika kipindi chote tangu mwaka 1962, shughuli za sanaa na utamaduni zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali.

Wakati wa Mwalimu Nyerere uhusiano wa sekta ya utamaduni na maendeleo ulitambuliwa hasa miaka ya 70.

Kwa mfano iliyokuwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana (1979) iliwateua wataalamu waandike kitabu Utamaduni Chombo cha Maendeleo.

Katika dibaji ya kitabu hicho, aliyekuwa waziri wa wizara husika alitoa maelezo yaliyojaribu kuonesha uhusiano kati ya utamaduni, uhuru na maendeleo nchini. Nanukuu:

“Kuna sababu nyingi za kuutambua utamaduni kuwa ni chombo cha maendeleo. Moja ni kuwa vipengele na fani mbalimbali za utamaduni ndizo zilizo katika kiini cha umoja wa jamii. Utamaduni ni sehemu ya siasa ya Taifa letu lenye msingi na shabaha ya umoja wa kweli. Uhuru wetu uliletwa na umoja. Maendeleo hayapatikani bila ya uhuru na umoja. Hivyo utamaduni kama nguzo ya umoja, ni chombo cha maendeleo (Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, 1979, uk. vii)”.

Katika jitihada za kukuza utamaduni, Mwalimu Nyerere alianzisha Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) mwaka 1967, hiyo ikiwa ni miaka sita tu baada ya uhuru, ili kukuza Kiswahili kiwe lugha inayoweza kutumiwa katika nyanja zote za jamii, utawala, elimu, mafunzo na biashara nchini.

Miaka minane baadaye, Serikali ya Nyerere ilianzisha Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), ambayo yaliunganishwa mwaka 1984 kuwa Baraza la Sanaa la Taifa la sasa (Basata).

Madhumuni ya Basata na mabaraza yaliyolitangulia yalikuwa kufufua, kuendeleza na kukuza sanaa za asili (utamaduni) mbalimbali za Watanzania.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzisha masomo ya sanaa tangu mwaka 1966. Mwaka 1973, mafunzo ya sanaa kwa walimu wa shule za msingi yalianzishwa katika Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa katika Chuo cha Ualimu Butimba, jijini Mwanza.

Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambacho sasa kinaitwa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa) kilianzishwa mwaka 1981 kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wasanii ili kukuza na kuenzi utamaduni wa Mtanzania.

Mwaka 1985 Serikali ilianzisha matamasha na mashindano ya fani za utamaduni kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kanda hadi taifa.

Katika duru nyingi za kimataifa, nchi yetu chini ya Mwalimu Julius Nyerere ilisifiwa kwa jitihada za kukuza utamaduni.

Lakini sasa tumejikuta tukiangukia kule kule alikosema Mwalimu Nyerere wakati ule kuwa ni ‘kusanyiko la watu wasio na roho’; tunapotea taratibu tukibaki kuwa taifa lisilo na utamaduni wake, lenye raia wasio na mwelekeo, wasiojifahamu, wasio na fahari ya utaifa wao, wasio na umoja, uzalendo, mshikamano au heshima mbele ya mataifa.

Kwa kawaida utamaduni huipa jamii utambulisho kama Taifa. Sura na haiba ya jamii ya nchi hueleweka na kuelezeka kutokana na utamaduni wa watu wake. Utamaduni hurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kupitia lugha, sanaa na imani.

Mwalimu Nyerere alihakikisha utamaduni wetu haupotei bali unaendelezwa na alijua kuwa nyenzo ya kuuendeleza ni kuanzisha vituo maalumu vya jumuiya vilivyojengwa katika kila wilaya, 'Community Centres'.

Vituo vya jumuiya viliwekwa chini ya maofisa utamaduni kuvisimamia na kuwa mahala ambapo serikali ilipatenga maalumu kwa ajili ya shughuli za sanaa na kutafiti masuala yaliyohusu utamaduni: Lugha, Mila na Desturi katika ngazi ya Wilaya.

Vituo vya jumuiya au vituo vya kijamii yalikuwa maeneo ya umma ambapo wanajumuiya walikuwa wanakusanyika kwa shughuli za vikundi, usaidizi wa kijamii, habari za umma, na madhumuni mengine.

Leo hii vituo hivyo havipo tena baada ya kugeuzwa kuwa ofisi za Manispaa au kukodishwa kwa watu binafsi ili kuongeza pato la serikali za mitaa bila kujali vijana walio Manispaa wanapewa sehemu nyingine maalumu kufanya shughuli zao za sanaa.

Kukosekana kwa vituo hivyo vya kijamii na maofisa utamaduni kuwa chini ya Tamisemi badala ya idara ya tamaduni yamechangia kuudidimiza utamaduni na sanaa nchini.

Utamaduni ukilelewa vizuri ni chombo chenye nafasi nyingi za ajira, huongeza pato la eneo husika kwa kuhamasisha maendeleo, huleta uzalendo, ubunifu wa mambo ya utamaduni, huhamasisha utalii katika utamaduni, ni sehemu ya utalii ambayo kwa bahati mbaya haijatumika kikamilifu katika kuongeza kipato cha nchi hii kwa ujumla.

Nina matumaini makubwa kuwa Rais John Magufuli ataendeleza alipoishia Mwalimu Nyerere kwani tangu ameingia madarakani mwaka 2015 namwona Mwalimu Nyerere mpya kupitia kazi mbalimbali anazofanya na bila shaka hatosita kuingia pia eneo hilo la utamaduni kwa mapana yake.

No comments: