Sep 8, 2017

Madhara Yanayosababishwa na Ponografia



MAPOKEO ya kazi za sanaa katika jamii yoyote hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo, mtindo, muundo, maudhui na hivyo hubaki kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio ya jamii husika.

Kama sanaa zenu haziakisi maisha yenu, basi mjue kuwa vizazi vyenu vitarithi mambo yasiyokuwa yenu. Sanaa kama nguzo mojawapo muhimu ya Utamaduni hukua na pia hufa.
Unaweza kujiuliza; Je, filamu zetu zilivyo leo zinaweka kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo? Au kizazi chetu kinaweka kumbukumbu potofu ya filamu na sanaa zetu na utamaduni kwa vizazi vijavyo?


Niliwahi kuandika kuhusu uoneshaji wa video na sinema kiholela unavyoathiri vijana na watoto kisaikolojia na kimaadili, na kwamba umechangia kwa kiwango kikubwa kuporomoka kwa maadili ya kijamii na kuongezeka kwa uhalifu miongoni mwa vijana.
Hii imetokana na kukosekana udhibiti wa mabanda ya video yaliyochukua nafasi ya majumba rasmi ya sinema yaliyofungwa au kugeuzwa kuwa ya kufanyia huduma nyingine za kijamii.

Mabanda haya yamekuwa yakionesha sinema chafu maarufu kama ‘Pilau’, ‘Kachumbari’, ‘Kuchikuchi Hotae’, ‘Yale mambo yetu’, ‘Picha la ukweli’, ‘Ubwabwa’ na majina mengine ambayo kwa mtu wa kawaida si rahisi kujua maana yake.

Siku hizi habari za kila aina kuhusu ngono zinapatikana kwa urahisi kupitia televisheni, sinema, video za muziki, na intaneti. Na imechukuliwa kama ni jambo la kawaida kutazama ponografia (picha za ngono).

Kutazama ponografia kunaweza kuwafanya watazamaji wafanye ngono potovu. Imani kwamba wanawake hufurahia ubakaji, na kwamba wabakaji ni watu wa kawaida imeenea sana miongoni mwa wanaume wenye mazoea ya kutazama ponografia.

Watafiti wanasema kwamba ukizoea kutazama ponografia unaweza kuathiri uwezo wako wa kufurahia na kufanya ngono katika ndoa. Dk. Victor Cline, mtaalamu wa kutibu watu wanaotawaliwa na mambo ya ngono, amewahi kueleza kwamba watu wanaotazama ponografia hujikuta wakipata aina fulani ya ulevi (addiction) unaowafanya kuendelea tu bila kuacha.

Mtu anayeanza kutazama ponografia kidogo-kidogo, asipoacha mwishowe anaweza kuwa na mazoea ya kusoma habari na kutazama picha chafu zaidi za ponografia. Dk. Cline anadai kwamba mazoea hayo yanaweza kuongoza kwenye matendo mapotovu ya ngono.
Wanasayansi wanaochunguza tabia za wanadamu wanakubaliana na jambo hilo. Dk. Cline anaripoti kwamba “upotovu wowote wa ngono unaweza kuanza hivyo... na kwamba mtu hawezi kuacha hata akisumbuliwa sana na dhamiri, maana inakuwa kama kilema.”

Hatimaye, huenda ikamfanya mtu anayetazama ponografia akajaribu kufanya mambo yasiyo ya adili aliyoona, na mara nyingi matokeo huwa mabaya zaidi.

Tatizo hilo linaweza kuanza hatua kwa hatua bila kutambuliwa. Huongezeka na kuenea kama kansa. Kwa kawaida mazoea hayo hayakomi, wala hayawezi kutatuliwa kwa urahisi kwa sababu yanakuwa yameathiri ubongo wa mtu husika.

Haishangazi kwamba mara nyingi wanaume waliozoea kutazama ponografia hawakubali kwamba wana tatizo, na ni kawaida kwa wenzi wa ndoa kukosana, nyakati nyingine kutalikiana, na hata mahusiano mengine ya karibu huharibika kwa sababu hiyo.

Takwimu zinaonesha kwamba watazamaji wengi wa ponografia ni wavulana wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17. Kwa kweli, wengi wao hujifunza masuala ya ngono hasa kupitia ponografia. Hilo lina matokeo mabaya sana.

Mbaya zaidi sinema za ponografia hazioneshi kuhusu masuala ya mimba za umri mdogo na magonjwa yanayoambukizwa kingono kama UKIMWI, jambo hilo huonesha kwamba mambo yanayooneshwa katika ponografia hayana madhara.

Watafiti fulani husema kwamba kutazama ponografia kunaweza pia kuathiri ukuaji wa kawaida wa ubongo wa mtoto. Uchunguzi wa athari za sauti na picha za ponografia katika utendaji wa kawaida wa ubongo unaonesha kwamba kutazama ponografia huathiri kabisa uwezo wa kawaida wa kufikiri.

Pia hudhuru ubongo wa watoto unaoathiriwa kwa urahisi kwa sababu hufanya wasione mambo kihalisi na hudhuru afya yao ya kiakili na ya kimwili, na huwazuia kupata furaha.
Ponografia huathiri mitazamo na tabia. Ujumbe wake unavutia hasa kwa sababu si halisi na hivyo unaifanya ionekane kuwa yenye kusisimua zaidi kuliko mambo halisi. Watu wanaotazama ponografia hutarajia mambo yasiyo halisi ambayo huharibu mahusiano.

Ponografia inaweza kuwafanya wenzi wa ndoa wakose kuwa wanyofu na wakose kuaminiana, sifa ambazo ni muhimu katika ndoa. Kwa sababu ponografia hutazamwa hasa faraghani, mara nyingi humfanya mtu atumie hila na uongo. Wenzi wa ndoa huhisi kwamba wamesalitiwa. Hawaelewi kwa nini mwenzi wao havutiwi nao tena.

Mapambano ya kuacha mazoea ya kutazama ponografia hayapaswi kuchukuliwa kijuujuu tu; yanaweza kuwa mapambano magumu. Dk. Victor Cline ambaye ametibu mamia ya watu wenye mazoea ya kutazama ponografia asema hivi: “Ahadi hazitoshi. Haitoshi kuwa na makusudio mema. Mtu mwenye mazoea ya kutazama ponografia hawezi kufaulu peke yake bila kusaidiwa.”

Dk. Cline asema kwamba hatua ya kwanza ya tiba ni kumhusisha mwenzi wake ikiwa amefunga ndoa. Anadai kwamba “Tiba hufaulu haraka ikiwa wote wawili wanahusishwa. Wote wawili wameumia. Wote wanahitaji msaada.”

Ikiwa mtu ni kapela (hajaoa au kuolewa), mara nyingi rafiki mwenye kuaminika au mshiriki wa familia anaweza kumuimarisha. Haidhuru ni nani anayehusika katika tiba hiyo, Dk. Cline hueleza sheria moja thabiti: Sema waziwazi kuhusu tatizo hilo na unapotumbukia tena katika mazoea hayo. “Siri ‘huua’,” yeye anasema. “Huleta aibu na dhamiri mbaya.”


Alamsiki.

No comments: