Jul 27, 2017

Hakuna shaka Tanga ndio kitovu cha burudani Tanzania



NAUKUBALI sana mkoa wa Tanga, una historia nzuri katika burudani na unaaminika kuwa ndio kitovu cha burudani katika nchi hii, kuanzia kabumbu, muziki, sinema na kadhalika. Tanga ni jiji lililo ufukoni mwa Bahari ya Hindi.

Jina la mji wa Tanga linaaminiwa kutokana na neno “tanga” yaani kitambaa kikubwa kinachokingamishwa kwenye mlingoti wa jahazi, ilipewa jina hilo kwa sababu kisiwa cha Toten ilipo hori ya Tanga kina umbo linalofanana na kitambaa cha aina hii.


Tanga ni miongoni mwa mikoa michache nchini yenye historia kubwa ya soka la Tanzania. Ni ngumu kuzungumza historia ya soka la nchi hii bila kuutaja mkoa wa Tanga, ambako waliwahi kupita wachezaji wakubwa na kucheza hadi timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

Pia wachezaji kadhaa wa mkoa huo wamewahi kutamba katika klabu kongwe za Simba na Yanga za Dar es Salaam baada ya kuwika katika klabu zao za Tanga za African Sports na Coastal Union. Historia ya soka la Tanzania haijawaacha Tanga, japo wenyewe wanaonekana kutojali hali waliyonayo sasa kwenye medani ya soka.

Katika muziki, Tanga ina historia nzuri kimuziki na sifa zake zilianza kusikika kuanzia enzi za utawala wa Wajerumani, ambapo shule ya kwanza ya serikali ilijengwa hapo enzi hizo hizo za Wajerumani, kisha mji uliendelea kukua sana kutokana na kilimo cha katani, na hivyo kukusanya vijana toka kila kona ya nchi kwenda kutafuta kazi katika mashamba makubwa ya katani wakati huo.

Tanga ukawa mji ambao kutokana na uwingi wa vijana wakati huo, shughuli za burudani ya muziki nazo zilifikia kiwango cha juu kuliko sehemu nyingi Tanzania.

Ukizungumzia historia ya muziki wa dansi, huwezi kukwepa kuzungumzia Tanga, kwani historia inaeleza kuwa kabla ya kuanza vikundi vya muziki wa dansi kulianzishwa klabu za kucheza dansi. Klabu hizo zikitumia muziki wa santuri, wanachama wake walicheza na hata kushindana kucheza muziki kwa mitindo mbalimbali ya kigeni ikiwemo waltz, tango, chacha, rhumba na kadhalika.

Klabu za kwanza nchini zilianzia Tanga. Kulikuwa na klabu kama Young Noverty miaka michache baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, wakati huo nchi ya Tanganyika ikiwa changa kabisa. Mtindo huu wa vilabu vya dansi ulienea na baadaye kuingia Dar es Salaam na miji mingine iliyokuwa imeshaanza wakati huo.

Vilabu hivi ndivyo baadaye vikaanzisha vikundi vya kwanza vya muziki wa dansi. Hata majina ya vikundi hivyo vya kwanza yalihusiana na klabu za burudani za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Coast Social Orchestra, na kadhalika. Hivyo mji wa Tanga ulikuwa katika ndoto za vijana enzi hizo.

Kati ya klabu hizo kulikuweko klabu iliyoitwa Young Nyamwezi, kama jina lake lilivyo ilikuwa ni klabu ya vijana kutoka Unyamwezini. Hatimaye mwaka 1955 klabu hii ilianzisha bendi yake iliyoitwa Young Nyamwezi Band, bendi hii ilikuja kukua, na baada ya Uhuru ilibadili jina na kuitwa Jamhuri Jazz Band.

Hakika kwa vijana waliokuwa wapenzi wa muziki miaka ya 1960 na 70 ilikuwa lazima uifahamu Jamhuri Jazz Band, muziki wake ulijulikana Afrika Mashariki nzima. Bendi hii ilikuwa ikibadili mitindo ya upigaji wake na kupiga katika mitindo ya ‘Toyota’ na hatimaye ‘Dondola’.
Ukiongelea filamu, Tanga ndiyo mkoa wanaotoka magwiji wa filamu za kizazi kipya waliothubutu kuandaa filamu miaka ya tisini japo mazingira yalikuwa magumu. Japo wengi wanadhani filamu ya ‘Girlfriend (2003)’ ndiyo ilifungua ukurasa wa Bongo Movies, ni filamu ya 'Shamba Kubwa (1995)’ ya Mwl Kassim El-Siagi wa Tanga ndiyo iliyofungua milango ya filamu za kibiashara Tanzania.

Kipindi kile teknolojia ilikuwa bado ndogo na vituo vya televisheni ndo kwanza vilikuwa vimeanza, kwani wakati huo kulikuwa na vituo vya CTN, DTV na ITV tu, ambavyo hata hivyo vilirusha matangazo yake jijini Dar es Salaam.

Filamu ya ‘Shamba Kubwa’ ndiyo iliyowaibua wasanii ambao wamekuja kutamba katika ulimwengu wa filamu; kama Hassan Master, Jimmy Master, Kaini na Amina Mwinyi, na iliteka wengi.


Baadaye zilifuatia sinema za ‘Love Story Tanganyika na Unguja (1998)' ya Amri Bawji, ‘Kifo Haramu’ ya Jimmy Master, ‘Dunia Hadaa (2000)' ya Mwl Kassim El-Siagi, na ‘Augua (2002)' ya Amri Bawji. Zote hizi zilitengenezwa na magwiji kutoka Tanga.

Filamu hizi zilitengenezwa katika mfumo wa VHS (analogia), na hata uhariri wake ulitumia akili zaidi kutokana na teknolojia ya wakati huo kuwa ya kiwango kidogo, lakini ziliweza kuvutia sana kutokana na maudhui na msuko mzuri wa hadithi zake.

Filamu zingine zilizotengenezwa Tanga ni ‘Shahidi’ ya Amri Bawji, ‘Fimbo ya Baba’ na ‘Chukua Pipi’ ambazo zimetayarishwa na Shirika la Uzima Kwa Sanaa (UZIKWASA) la Pangani Tanga. Zipo pia ‘Ua la Matumaini’ na ‘Habari Kubwa’ za Mwl Kassim El-Siagi.

Ukiuacha mji wa Dar es Salaam, ni mji wa Tanga ndio ulikuwa na majumba mengi ya kutazama sinema. Katika mji wa Tanga kulikuwa na majumba ya sinema ya Majestic, Novelty, Regal na Tanga Cinema.


Hapa sijagusia kuhusu mkoa wa Tanga kujaaliwa warembo wenye kujua kumliwaza mwanaume akaliwazika, ndio maana inasemwa ‘Tanga ndiko mapenzi yalikozaliwa!’ Sijui kama nitakosea nikisema Tanga ni ‘Los Angeles’ ya Tanzania. Yupo atakayebisha?

No comments: