Jul 18, 2017

Forrest Gump: Sinema pekee yenye kuonesha Marekani wameshindwa Vietnam

Forrest Gump

NILIPOITAZAMA sinema ya Forest Gump kwa mara ya kwanza haikunivutia, nadhani ni kwa sababu wakati huo sikuwa makini kama sasa. Nilipoiangalia tena nikagundua kuwa ni ‘bonge la sinema’. Sinema hii inafundisha mengi kuhusu maisha na maana ya maisha. Kwamba maisha si mabaya kama ambavyo watu wengi wanataka yaonekane. Kwamba kijana asiye na hatia anaweza kufanikisha maisha ya wengi kwa hali yake.

Na kama hujawahi kuiona au unadhani hujaipenda nakushauri uitazame tena. Inastaajabisha kwelikweli… ni moja ya sinema bomba sana, na kwa kweli ilistahili kuzoa tuzo.
Forrest Gump ni filamu ya Amerika ya mwaka 1994 inayotokana na riwaya yenye jina hilo hilo iliyoandikwa na Winston Groom mwaka 1986. Filamu hii imeongozwa na Robert Zemeckis na imeigizwa na Tom Hanks, Robin Wright, Gary Sinise, Mykelti Williamson, na Sally Field.

Hadithi yake inaelezea mambo ya miongo kadhaa katika maisha ya Forrest Gump, mtu aliyekuwa na akili chini ya kiwango cha kawaida (IQ 75) lakini ana moyo-mzuri, huruma na shujaa wa Alabama, ambaye anashuhudia baadhi ya matukio ya nusu ya mwisho wa Karne ya 20 huko Marekani; hasa, kipindi cha kati cha kuzaliwa kwake mwaka 1944 na 1982.

Picha za sinema hii zilipigwa mwishoni mwa mwaka 1993, hasa katika maeneo ya Georgia, North Carolina, na South Carolina.

Sinema hii ilitolewa rasmi Julai 6, 1994, ilipata mafanikio makubwa kibiashara kwa kazi zilizotoka mwaka huo, na kuwa sinema ya kwanza iliyofanikiwa sana ya kampuni ya Paramount Pictures tangu iungane na Viacom. Imeingiza zaidi ya dola za Kimarekani milioni 677 duniani kote.

Mwaka 1995 ilishinda Tuzo sita za Oscar (Academy Awards): Sinema Bora, Muongozaji Bora (Robert Zemeckis), Mwigizaji Bora (Tom Hanks), Script Bora iliyotokana na Riwaya (Eric Roth), Best Visual Effects, na Filamu iliyohaririwa vizuri.

Pia ilipata tuzo nyingine nyingi na kuteuliwa katika tuzo kibao, ikiwa ni pamoja na Golden Globes, People’s Choice Awards, na Young Artist Awards, kati ya nyingi nyingine.

Mwaka 1996, mgahawa bora wa Bubba Gump Shrimp Company, ulifunguliwa kutokana na filamu hii na tangu wakati huo umeenea maeneo mengi duniani.

Mnamo 2011, Maktaba ya Congress iliihifadhi filamu hii kwa Msajili wa Taifa wa Filamu za Marekani kama “kumbukumbu ya kiutamaduni na kihistoria”.

Stori yake inaanzia pale Forrest Gump anaposimulia hadithi ya maisha yake kwa watu waliokaa karibu naye kwenye benchi huko Savannah, Georgia mwaka 1981.

Katika siku yake ya kwanza shule, Greenbow, Alabama, Forrest Gump anakutana na msichana aitwaye Jenny Curran. Licha ya uwezo wake mdogo akili, lakini uwezo wake wa kukimbia unamfanya kupata nafasi ya masomo kupitia soka.

Baada ya kuhitimu chuo, anajiunga jeshini, ambapo anapata rafiki, askari mwenzake aitwaye Bubba, ambaye anamshawishi Gump kufanya biashara ya uduvi (dagaa kamba) vita vikiisha.

Walikwenda vitani Vietnam, wakashambuliwa na Bubba akauawa katika mapigano. Forest Gump anaweza kuokoa askari wengi wa kikosi chake, ikiwa ni pamoja na Luteni wake, Dan Taylor, ambaye anapoteza miguu yake yote. Forest Gump anapata tuzo ya ‘Medal of Honor’ kwa ujasiri wake.

Wakati Gump akitibiwa jeraha la risasi kwenye makalio yake, anagundua ana kipaji katika mchezo wa ping pong. Anapata umaarufu kwa kucheza ping pong. Katika mkutano wa huko Washington, D.C., Gump anaungana tena na Jenny Curran.

Anaporudi nyumbani, Gump anatumia mapato hayo kununua boti ya kuvulia uduvi, akitimiza ahadi yake kwa Bubba. Baadaye anaungana na Luteni Dan, na siku moja kimbunga Carmen kinapiga na kuharibu boti zote isipokuwa boti yao pekee na wao wanapata kiasi kikubwa cha uduvi.

Gump anatumia mapato yake kununua meli kubwa ya kuvulia uduvi. Dan anawekeza katika kampuni ya Apple Computer (ambayo Forest Gump anadhani ni kampuni ya matunda).

Kisha Forest Gump anarudi nyumbani kumuona mama yake katika siku za mwisho. Kuna mengi sana ya kujifunza katika sinema hii, ikiwemo historia na utamaduni wa Wamarekani.


Waongozaji wawili walipewa fursa ya kuiongoza filamu hii kabla hajachaguliwa Robert Zemeckis huku Terry Gilliam alikataa ofa hii. Barry Sonnenfeld aliunganishwa kwenye filamu hii, lakini aliondoka kwenda kuongoza filamu ya Addams Family Values.

No comments: