Jul 18, 2017

Soko la filamu Tanzania halijafa bali mfumo ndiyo mbovu (1)

Msanii Jacob Steven maarufu kama JB akipokea Tuzo kutoka kwa Msambazaji wa filamu, Dilesh Solanki wa Steps Entertainment

KATIKA sekta za filamu kwenye nchi zilizopiga hatua, biashara ya filamu huanza na Box Office (mfumo maalum unaoanzia kwenye uoneshaji sinema ndani ya majumba ya sinema 'theatres') au kutolewa katika njia ya sinema.
Baadaye hurushwa kwenye vituo vya televisheni za kulipia, baadaye kwenye vyombo vya habari saidizi (video games, mitandao maalumu ya kupakua filamu, katuni n.k.), kisha katika televisheni za umma na mwisho kutolewa kama bidhaa rasmi (DVD) kwa matumizi ya nyumbani.

Huu ni mfumo maalumu wa kimasoko katika studio kubwa za filamu, iwe ni Uingereza, Marekani, India, China, au hata Afrika Kusini na nchi zingine zilizopiga hatua. Ni mfumo unaotumika katika mkondo mkuu (main stream), ambapo studio kubwa huwekeza na kusambaza kazi zilizotegenezwa kwa bajeti kubwa.


Sinema ya Neno la Mwisho inayomuelezea Marehemu Steven Kanumba
Tanzania kwa sasa kilio kikubwa cha wasanii wa filamu ni soko la filamu za ndani kufa au kupooza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo, filamu kutoka nje ya nchi, wafanyabiashara wachache wa Kiasia kulihodhi soko n.k.

Ukweli ni kwamba tunalo tatizo la kimfumo, ambalo kama litatatuliwa, kisha tukarekebisha kasoro kadhaa zilizopo, tutaweza kufanya biashara kwa kiwango ambacho hakijawahi kuonekana.

Kwa sasa huu mfumo wa kukimbilia kutoa filamu zetu kwenye DVD umepitwa na wakati, na hata deki za kucheza Dvd zimepungua au pengine hazitengenezwi tena kutokana na kukua kwa teknolojia.

Kwa mujibu wa tafiti, watazamaji wengi hupenda kwenda kuangalia sinema kwenye kumbi za sinema (haijalishi ni kumbi rasmi au zisizo rasmi, kama mabanda ya video), ndio maana tunahitaji kubadilika na kuachana na mfumo wa kukimbilia kutoa filamu kwenye Dvd.

Tafiti zinaonesha kuwa wanaokwenda kuangalia sinema kwenye kumbi (hasa mabanda ya video) kulingana na umri ni: Asilimia 50 ya watazamaji ni wenye umri kati ya miaka 10-24, asilimia 30 ni wenye umri kati ya miaka 25-34, asilimia 15 ni kati ya watu wenye umri wa miaka 35-49 na asilimia 5 tu ya watu wenye umri zaidi yamiaka 50.

Kwa takwimu kama hizi (japo sio rasmi) tunapaswa kuuangalia upya mkakati wa kimasoko kutumia maonesho ya sinema kama njia ya uzinduzi badala ya kutoa DVD.

Hatuna namna yoyote tunayoweza kutumia kuukwepa mfumo wa sinema na kwenda moja kwa moja kwenye DVD, hasa kwa kuwa hivi sasa wengi wanaangalia sinema kwenye mitandao maalum ya kupakua (download) sinema. Tukisharekebisha mfumo wetu ndipo tuangalie masuala mengine yatakayowafanya watazamaji wetu kurudisha imani yao kwenye kazi zetu.

Watazamaji wa filamu hawanunui filamu kwa sababu tu zinapatikana au kusambazwa. Na hawanunui filamu kwa sababu tu eti fulani na fulani wamecheza. Kutokana na utafiti wangu, kuna vigezo muhimu viwili ambavyo vinaweza kutuongoza katika dhana nzima ya mafanikio katika usambazaji filamu; (Maudhui/Mahitaji ya Watazamaji (Content/Audience Connection) na Jukwaa la Uwasilishaji (Media Delivery Platforms).

Kwa miaka kadhaa, sekta ya filamu Tanzania imeshuhudia utofauti mkubwa kati ya maudhui katika hadithi zetu na kile watazamaji wanachokihitaji, na matokeo yake yameendelea kuyumbisha mikakati ya soko na sera za usambazaji. Maudhui lazima yahusishwe moja kwa moja na mahitaji ya watazamaji ili kuwe na nafasi ya mafanikio kwenye soko. Maudhui yanayofaa katika kizazi cha leo ni yale yanayokwenda sambamba na watazamaji ndani ya akili zao na kuihusisha jamii moja kwa moja.

Mafanikio yanayotokana na maudhui yanategemea sana mmenyuko wa watazamaji, na kujenga maudhui yaliyo kwenye mwelekeo na matarajio yao, hivyo, inahitajika kwa wasanii wetu kujihusisha moja kwa moja na mtazamo wa watazamaji katika mazingira waliyomo. Ndio maana utafiti ni suala la kupewa umuhimu mkubwa kabla ya kuandaa kazi husika.

Kabla hadithi yako haijawafikia watazamaji, tayari mtazamaji atakuwa na picha ya kipi anataka kukiamini na kama hadithi yako imeandaliwa katika mtazamo mzuri, mtu wa aina hiyo huamini na hununua kazi bila kusita.

Kama hadithi itaifikia jamii ya watazamaji ambao mtazamo wao utalingana na kisa chako, wigo wake utapanuka, watu watapeana taarifa kwa njia ya neno kwa neno (ambayo ni njia ya ufanisi zaidi kwa mkakati wa soko) na hujenga nidhamu ya utazamaji wa filamu.

Hakuna hadithi inayofanikiwa kama watazamaji hawapati kitu wanachokiamini - na kwa wastani wa filamu 100 za Kitanzania, watazamaji hawataona kila kitu wanachohitaji, watachukua na kuchagua kati ya filamu nyingi wanazoziona ili kuridhisha matakwa yao.

Kuwaelewa watazamaji ni hatua moja muhimu sana katika mchakato wa biashara ya filamu. Kubainisha maudhui ili yaendane na matarajio yao ni muhimu sana. Kama huwezi kuambatanisha maudhui yako yaende sambamba na mtazamo wa watazamaji, basi, hadithi itapuuzwa.

Kama mtayarishaji wa filamu, suala la kwanza unatakiwa kuwajengea msingi watazamaji katika maudhui uliyoyakusudia, ukielewa kwamba unaweza kuwa bosi kwenye kampuni yako ya production; LAKINI UNACHOKIFANYA SI KWA AJILI YAKO! NI KWA WATAZAMAJI NA HADITHI ZAO!

Kuandaa hadithi iendane na ladha ya watazamaji - hasa kwa kuelewa kuwa watazamaji hawataki kubadilishwa mitazamo yao, bali wanataka kuimarisha mitazamo yao (they want it to be reinforced) - itakusaidia kuanzisha mijadala kuhusu masuala muhimu kwa watazamaji wako.

Kwa leo nausitisha mjadala hadi baadaye nitakapouendeleza kuhusu namna ya kutumia jukwaa la uwasilishaji kama mfumo mzuri wa biashara ya usambazaji filamu.


Nakaribisha maoni.

No comments: