Jun 6, 2017

Bibi Esther Mahlangu: Darasa zuri kwa wasanii wa Tanzania

Msanii wa Afrika Kusini, Bibi Esther Mahlangu

NI ukweli usiopingika kuwa sekta ya sanaa nchini ipo chumba cha wagonjwa mahututi, na hatua za makusudi zinahitajika kuchukuliwa (na wasanii wenyewe) kunusuru hali hii.

Nakumbuka miaka ya 1990 hadi 2000, wasanii wa sanaa ya uchoraji walitingisha sana kutokana na kazi zao za michoro. Enzi hizo wachoraji ndio wasanii waliokuwa maarufu (kwa majina yao), ingawa watu hawakuwafahamu kwa sura, kwa kuwa michoro yao ilitamba sana kwenye magazeti na majarida. Na waliweza hata kumiliki magari, japo hayakuwa ya kifahari.

Wachoraji kama James Gayo, John Kaduma, Ali Masoud (Kipanya), Adam Luta, Abdul King.O, Nathan Mpangala, Noah Yongolo, Cloud Chatanda, Paul Ndunguru, Chris Shola na wengine wengi (hata mimi nilikuwemo) walimfanya hata mtoto mdogo kutamani kuwa kama wao.

Baada ya teknolojia ya computer kuingia nchini, wengi wakaacha uchoraji na kujikita kwenye graphic designing, hivyo sanaa ya uchoraji kubaki kwa wachache, hasa wachoraji wa picha za rangi kama tingatinga n.k.

Zikaja zama za wanamuziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva) kutingisha, hata hivyo haikuchukua muda wasanii wa filamu nao wakaibuka na kushika chati. Miziki na Filamu za Tanzania zikazipiga kumbo kazi za nje, kama Nigeria, India, DR Congo n.k. hivyo, kumfanya kila kijana kutamani kuwa mwigizaji au mwanamuziki.

Lakini leo hii, hakuna msanii yeyote (wa sanaa yoyote nchini) anayeweza kusimama na kujisifu kwamba anakula halali kulingana na wingi wa jasho lake. Wote wanalalamikia mfumo kandamizi unaonyonya jasho lao.

Hata wazazi leo  hii hawapendi watoto wao wajishughulishe na sanaa maana wanajua kwamba wasanii wanahangaika na njaa. Hii ndiyo sababu mpaka leo, kila unapomuuliza msanii maarufu, alipotoka mpaka kufika alipo, atakwambia kwamba wazazi wake hawakutaka kabisa awe msanii.

Si kwa sababu ni fani mbaya la hasha! Wanaona sanaa ni kupoteza muda, ni uhuni tu! Laiti wangeona mafanikio ya wasanii, wasingewakataza watoto wao hata kidogo.

Pamoja na kuwepo fursa nyingi lakini tatizo kubwa hivi sasa linalowasumbua wasanii wetu ni dhana dhalili (inferiority complex), kwani hawajiamini tena (hasa ukiwalinganisha na wasanii kutoka Kenya, Uganda na kwingineko) eti kwa kuwa hawajui/ hawawezi kuongea Kiingereza kwa ufasaha, hivyo, kujikuta wakipoteza fursa nyingi.

Mfano ni hivi karibuni, gazeti la HabariLeo lilimkariri mwigizaji wa filamu nchini, Jackline Wolper akisema lugha ya Kiingereza imekuwa kikwazo cha yeye kuigiza na waigizaji wa nje ya nchi, na inamfanya ashindwe kufanya kazi na waigizaji wa nje ingawa wamekuwa wakija hapa nchini.

Hali hii imeufanya hata uchumi wa nchi hii kuwa tegemezi mno kwa kuwa hatuna tena wabunifu au wenye maono. Nadhani utakubaliana nami kuwa ubora wa sanaa ni kielelezo cha maendeleo ya nchi.

Wasanii wanapokuwa na maisha mazuri na wakawa wanaishi maisha ya msanii yasiyo ya kuigiza, ni dalili kuwa nchi husika ina mwamko mzuri wa kiuchumi (angalia nchi zilizopiga hatua). Utajiri wa wasanii ni utajiri wa jamii, ni utajiri wa nchi.

Sanaa ni kilainishi (grisi) cha uchumi wa sekta nyingine nyingi. Kwa maana nyingine, mafanikio ya sanaa ndiyo msisimko wa uchumi kwa taifa. Pia huitangaza nchi na kuchagiza kivutio cha wageni kutembea kibiashara au kitalii, hivyo kuipa nguvu sekta ya Utalii.

Hata Wasanii wanapotajirika, huwezesha kupanuka kwa sekta ya Uwekezaji na kutanuka kwa sekta za Ajira na Elimu. Ni ukweli usiopingika kuwa uchumi wa sanaa unaweza kuibeba jamii kwa upana wake. Pia Sanaa inapotumika vizuri hufanya kazi kama mhimili huru unaosimamia dola.

Katika nchi ambayo Bunge linatawaliwa na ushabiki wa kivyama, vyombo vya habari navyo vikawa kimya, sanaa inaweza kuwa nyenzo imara zaidi ya kuwasiliana na jamii na kuieleza jinsi mambo yasivyo sawa.

Sanaa kwa kushirikiana na vyombo vya habari na Bunge, inaweza kuwa daraja rahisi la jamii kujua kinachoendeleaa kwenye nchi yao na hata kujua udhaifu au uimara wa serikali. Hapa ni suala la namna ya kuitumia sanaa.

Mwananchi anaweza asiwe mfuatiliaji wa Bunge, hasomi magazeti na hataki kusikiliza taarifa za habari lakini akasikiliza nyimbo, akaangalia filamu au kusoma katuni na michoro mingine na kupata ujumbe.

Na ukitaka uiue jamii yoyote ile, basi haribu mfumo wake wa sanaa na wasanii wajikite kwenye mambo mengine bila kumulika matatizo ya jamii wanayoishi. Inaweza kuchukua miaka 50 kubadili fikra za wananchi lakini tungo na msimamo wa wasanii kwa mwezi mmoja, zinatosha kufanya mabadiliko makubwa kwenye jamii.

Nimalize makala yangu kwa kumtazama Bibi Esther Mahlangu, ambaye kwa sasa ana miaka 81. Bibi huyu alizaliwa mnamo 11 Novemba 1935, huko Middleburg, Mpumalanga-Afrika Kusini. Anaongea vyema lugha yake ya Ndebele, hajui lugha ya Kiingereza hata kidogo.

Gari iliyochorwa kwa ustadi mkubwa na Bibi Esther Mahlangu

Bibi Esther Mahlangu kupitia karama yake ya uchoraji, mnamo mwaka 1991 aliweza kubuni na kuchora michoro [patterns] kwenye gari aina ya BMW 525i na kuwa gari ya kwanza kutoka katika company ya BMW (Bavarian Motor Works) kuchorwa na mbunifu toka Afrika kuipitia kitengo chao cha BMW Art Car.

Ndege ya Shirika la Ndege la Uingereza inayoonesha ubunifu wa Bibi Esther Mahlangu

Mwaka 1997, kazi ya Esther Mahlangu ilitumiwa na shirika la British Airways kuchora mkia wa ndege zao, katika namna ileile ya mbinu na ubunifu alioutumia kuchora BMW 525i, ubunifu wake uliwafanya kampuni ya Fiat, kumpa nafasi ya kuchora gari yao aina ya Fiat 500 katika mji wa Turin mwaka 2007.

Bibi Esther Mahlangu amethubutu na hatimaye ameweza kuishi vizuri kwa kipaji chake ingawa hajaenda shule, na wala hajui kuongea Kiingereza kama ambavyo wengi wetu tunavyojidanganya.


Ujumbe wangu kwa Wasanii wa Tanzania: Usiogope kuchangamkia fursa kwa kuogopa kutofahamu kwa ufasaha lugha ya Kiingereza, wala usihuzunike kwa kukosa cheti. Badala yake jivunie hazina yako ya maarifa na kipaji chako, sababu kipaji kilichopakwa mafuta kinafuatwa na lugha zote ili kuleta flava na ubora.

No comments: