Oct 23, 2017

Muziki wa Singeli: ni mapinduzi mapya au kifo cha muziki?

Mwanamuziki Msaga Sumu

Mwanamuziki Sholo Mwamba
MUZIKI wa Tanzania unabadilika sana, wasanii wengi wamekuwa wakibuni mitindo ya aina mbalimbali ili kuzifanya kazi zao ziende mbali na kuvuta mashabiki wa muziki nchini na duniani kwa ujumla.

Miaka ya nyuma muziki wa dansi ndiyo ulikuwa ulishika hatamu, muziki huu ulioanza kama klabu ambapo watu walialikana kucheza aina mbalimbali za muziki wa kizungu mtindo maarufu uliojulikana kama ballroom dancing. Kisha taratibu ukaumbika ukifuata muziki wa soukous kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (rumba ya Kikongo) na tokea hapo ikawa inaitwa ‘rumba ya Tanzania’.

Katika wakati huo pia muziki wa taarab, wa Waafrika wa Pwani, haukuachwa nyuma. Ni muziki uliotokana na tamaduni nyingi, hasa muziki wa Waarabu na Wahindi, na ni uimbaji wa mashairi uliofuata muziki wa bendi.

Baadaye miaka ya 1990 ukaibuka muziki wa Hip hop, ambao baadaye ukapata jina la Bongo Fleva, uliotokana na hip hop kutoka Marekani, ikiwa na ongezeko la athira ya muziki wa reggae, R&B, afrobeat, dancehall, na mitindo ya asili ya Kitanzania kama vile taarab na dansi.

Wakati bongofleva ikitamba baadhi ya wasanii wakaja na aina mpya ya muziki wa mduara, uliochanganywa kutoka muziki wa taarab, dansi na mitindo ya asili.

Kiasili, mduara ni muendelezo kutoka kwa muziki wa kikundi cha zamani cha Sunburst, ambacho miaka ya 1970 kilikuwa maarufu, hasa kwa nyimbo za kitoto kama ‘Ukuti’. Kikundi hiki kiliwahi kutamba na wimbo wao wa Banchikicha.

Lakini kwa kuwa muziki hubadilika na kuja na vionjo tofauti, hivi sasa nchini tuna muziki wa singeli unaotokana na mchanganyiko wa ladha mbalimbali kama Taarab, Mduara, Bongo Fleva, Mchiriku na Vanga (mdundiko) la Kizaramo ambalo ndilo limezaa muziki huu.

Muziki wa singeli uliibuka kutoka uswahilini na kutapakaa nchi nzima na ulianza kutishia mustakabali wa muziki wa bongo fleva, hasa hip hop.
Muziki huu ulianzia katika shughuli za harusi au maulidi - hasa mkesha maarufu kama "vigodoro", ukakua na kuenea kwa kasi kubwa, hasa jijini Dar es Salaam, ukajizolea mashabiki lukuki na kufanikiwa kuzalisha vipaji kadhaa.

Pamoja na umaarufu wake, bado ni vigumu sana kwa mtu wa makamo kuuelewa muziki wa singeli, tena pale atakaposhuhudia wakiwa wanatumbuiza katika majukwaa lazima aseme hawa vijana wanashtua kidogo vilevi ndiyo wapate mzuka wa kuimba.

Ukiachilia mbali mashabiki wa muziki huo, hata asilimia kubwa ya wasanii wa muziki huu wakiwa wanatumbuiza wanakuwa na hulka ya ajabu pindi wawapo jukwaani, hata kama unaupenda lakini hamu huisha pale tu mambo yanapokuwa yanaenda kinyume na muziki wenyewe.

Tangu kuibuka kwa muziki huu nimekuwa najiuliza kama unaweza kuwa mapinduzi mapya badala ya kuwa kaburi la muziki. Kama aina ya muziki mwingine uliowahi kutamba hapa nchini kama mchiriku, mduara n.k. na kupotea, nina shaka hata singeli inaonesha kupitia hatua za mwisho za kufa na kuiacha bongo fleva kama ilivyokutwa!

Jambo la kwanza la kuzingatia katika muziki huu kuendelea kubaki kwenye chati kama Bongo Fleva na Afropop zilikofikia ni aina ya mashairi yanayoandikwa katika nyimbo zenyewe, na hii itasababisha kuwafikia hata watoto na watu wa rika mbalimbali nchini.

Siyo lazima kuandika kwa lugha za kigeni ili wananchi pamoja na watu wa mataifa waelewe, la hasha! Kuandika kwa maadili na mistari itakayogusa jamii ndiyo nguzo kubwa ya kuweza kuufikisha mbali sana muziki huu kwa kuzingatia tu kwamba kilichoandikwa hata mtoto anaweza kukitamka.

Nyimbo za Mapenzi siyo mbaya ila kuna walio chini ya umri wa miaka 18, vipi kuhusu wao? Nini wanajifunza kutokana na aina hizi za nyimbo? Je, vipi kama wakiwa wanaimba na kufuatisha mistari hiyo mbele ya wazazi na ndugu zao wa karibu?

Suala jingine ambalo ni la msingi ni muonekano wa Wasanii wenyewe, kwani wamekuwa wakivaa mavazi yanayotia hasira mbele ya jamii inayowazunguka, hivyo, kuleta tafsiri mbaya kwa watazamaji na mashabiki mbalimbali nchini.

Kiufupi, wananchi amekwishaupokea muziki huu japo siyo kwa mikono miwili ila kwa jitihada mbalimbali ambazo watafanya wasanii hawa lazima wafikie lengo na huenda ukawa muziki mkubwa sana tofauti na unavyofikiriwa.

Suala la matumizi ya vilevi pia ni la kuangaliwa kwa makini, kwani wasanii wa Singeli wengi wao wamekuwa wakikiri kutumia vilevi tofauti kama vile bangi, ugoro pombe kali n.k., ili kuweza kuleta ‘amsha amsha’ katika majukwa wanayopanda.

Hili ni moja kati ya vitu vitakavyoushusha muziki huu kiwango kwa asilimia kubwa na huenda ukachukiwa kuliko hata aina zingine za muziki hapa nchini.
Wasipoangalia wasanii wa Singeli wataishia kusema WanaBongo Fleva wameloga ingawa ni wao wenyewe wanajiloga kwa kutokuupa heshima muziki wao.

Ikumbukwe pia hata miaka hiyo Bongo Fleva ilivyokuwa ikianza muziki ulionekana kuwa ni uhuni na ni kitu kinachofanywa na wavuta bangi mpaka kusababisha wazazi kuwakataza watoto wao wasijihusishe kabisa na muziki huo.

Cha msingi sasa ni kujiwekea malengo katika muziki wao na kuhakikisha hawafanyi mambo yasiyoipendeza jamii kama wakati ule wa muziki wa Mchiriku na Mnanda ambao ulikuwa ni muziki wa fujo, pombe na aina zote za ‘ushenzi’ zilikuwa zikifanyika huko.

Muziki ni ajira, malengo, ubora na heshima hivyo lazima tu wayasimamie haya ili kuweza kutoboa, vinginevyo tutarajie kifo cha muziki huu mapema.


Alamsiki.

No comments: