Oct 23, 2017

Wasanii vunjeni ukuta wa fikra

Peter Tosh
Filamu ya Off Side
“EVERYBODY want to go to heaven, but nobody want to die…” hii ni nukuu kutoka kwenye wimbo wa Equal Rights wa aliyekuwa mwanamuziki mahiri wa reggae duniani, Peter Tosh. Maneno hayo ambayo tafsiri yake kwa lugha ya Kiswahili ni “Kila mtu anataka kwenda peponi, lakini hakuna anayetaka kufa…”

Sikuwa shabiki wa muziki wa reggae, ila nilipolazimika kusikiliza reggae nilipenda nyimbo za Lucky Dube na Peter Tosh. Wanamuziki wote wawili kwa sasa ni marehemu.

Ukiusikiliza kwa makini ujumbe ndani ya wimbo wa Equal Rights, utagundua kuwa ni chemsha bongo ya aina fulani. Maneno ya Peter Tosh katika wimbo huu yanaakisi hali halisi ilivyo katika shughuli za sanaa Tanzania, hasa muziki na filamu.

Ukiongea na wasanii wengi wa Tanzania watakwambia kuhusu ndoto walizonazo, kama vile kuingia kwenye soko la kimataifa na kadhalika, lakini hutawaona wakihangaika kutafuta taarifa au maarifa, kufanya utafiti au mazoezi yanayostahili juu ya kazi zao ambazo wanataka zikatingishe ulimwengu.

Pamoja na kuwepo fursa nyingi pia tatizo kubwa linalowasumbua wasanii wengi ni dhana dhalili (inferiority complex), kwani hawajiamini eti kwa kuwa hawawezi kuongea Kiingereza kwa ufasaha kama wenzao toka Kenya, Uganda na kwingineko.

Wapo waliowahi kukiri kuwa lugha ya Kiingereza ni kikwazo kwao kuigiza na waigizaji wa kutoka nje ya nchi.

Japo katika muziki tunajivuna kuwa na wasanii mahiri wanaoutangaza vyema muziki wa bongo fleva nje ya mipaka yetu, kama Ali Kiba, Diamond Platnumz na wengine, lakini kumekuwepo malalamiko ya kuibiana nyimbo na kukosa ubunifu kwa wengi.

Bado wanamuziki wengi wamekumbwa na skendo za kuiba nyimbo za wenzao na kuzirekodi tena au kuzitangaza kuwa ni kazi zao kwa kubadili majina.

Muziki wa Bongo Fleva umejaa nyimbo nyingi zilizonakiliwa kutoka kwa wanamuziki mbalimbali wa nje, na si hivyo tu bali wamekuwa wakiiga mpaka mavazi na uchezaji na hata namna ya utengenezaji wa video unafanya kazi nzima iwe ni kivuli tu cha kazi kutoka nje.

Mara nyingi hata baadhi ya watengeneza muziki, maarufu kama maproduza, wako tayari kukubali kuwarekodi wasanii ambao walitakiwa kupewa ushauri wa kuacha kuimba.
Mara nyingine waimbaji ni wazuri lakini muziki unakuwa hauna uhusiano wowote na uimbaji wao kutokana na mapungufu ya produza, hivyo basi kuwa na maana kwa wale tu ambao wanafahamu lugha inayoimbwa.

Ukijumlisha na tatizo sugu la rushwa na upendeleo katika vyombo vya habari, nyimbo ambazo hazikustahili kurushwa hewani hurushwa mara kwa mara, hivyo kuwafanya wanamuziki chipukizi kuiga makosa.

Jambo hili la mapungufu linafanyika si kwa muziki wa bongo fleva tu bali hata kwenye muziki wa dansi, kwa mfano, ukiingia katika kumbi za muziki wa dansi, ni kuiga kutupu kuanzia uvaaji wa wanamuziki, wachezaji wao, aina ya uimbaji, uchezaji, na mbaya zaidi kwa kuwa karibu wote wanaiga sehemu moja bendi nyingi zinafanana utadhani zimefanya mazoezi pamoja.

Ukija kwenye filamu pia ni matatizo matupu. Filamu zetu (Bongo Movies) nyingi zinaaminika kukopi hadithi na visa vya filamu nyingine za nje.

Pamoja na kuweko kwa wasanii wazuri wa filamu, tatizo lililoota mizizi la kuwahusisha katika uigizaji warembo maarufu ili kuuza filamu limechangia kuishusha hadhi kazi ya uigizaji.

Pia uigaji wa kila kitu kutoka Nigeria umeathiri kwa kiwango kikubwa katika kuendeleza soko la filamu za Tanzania. Huwa najiuliza: hivi kwani ni lazima hata wanakijiji katika filamu zetu wapake rangi kama wanakijiji katika filamu za Kinaijeria?

Je, waganga wa jadi katika filamu zetu lazima wavae mavazi mekundu na kujichora kwa vile Wanaijeria wanafanya hivyo? Hata majina ya filamu lazima yawe ya Kiingereza kwa kuwa Wanaijeria wanafanya hivyo?

Yaani hatukuishia kukopi stori tu, tumekopi hadi majina ya filamu zilizowahi kutoka, na mbaya zaidi tukaiga hadi cover za filamu hizo jambo ambalo limetutia aibu kubwa miongoni mwa mataifa mengine. Ingawa tumekuwa waigaji lakini hiki kimekuwa kichekesho mno.

Aibu kubwa hutukuta sisi tunaosafiri nje ya nchi au kuangalia sinema kwenye chaneli za nje, hasa kwa vile tunajua kuwa mamilioni ya watu wanaangalia kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Halafu kuna yale maandishi ya Kiingereza ambayo hudaiwa kuwa ndiyo tafsiri ya mazungumzo ya Kiswahili katika filamu zetu, mara nyingi tumetia aibu kwa tafsiri mbovu, maana mara nyingine hayaleti maana iliyokusudiwa kabisa, jambo linalozifanya kazi zetu kujitoa zenyewe katika mashindano ya soko la dunia.

Yote haya yametokana na wasanii kuwa na ubinafsi na kupenda kufanya kazi kibinafsi badala ya kushirikiana. Ili tupenye soko la dunia tunapaswa kuuvunja ukuta wa fikra (ubinafsi, uvivu na dhana dhalili).

Wajerumani walijikuta kwenye mtanziko mkubwa wa kuhitilafiana mitazamo, wa Magharibi wakawa na mitazamo inayokinzana na wa Mashariki... wakashindwa kabisa kupatana, na mwisho wakajenga ukuta wa kuwatenganisha.

Ukuta ule haupo tena, ulibomolewa baada ya miaka mingi kupita lakini ni baada ya kujitambua kwamba ukuta wa mawe ulikuwa ni matokeo ya ukuta wa kifikra na kimtazamo. Walivunja ukuta wa fikra kwanza kabla ya kuvunja ukuta unaoonekana..
Waisrael wanajenga ukuta kuzunguka Ukanda wa Gaza kujikinga na Wapalestina. Hii ni dhana iliyojengeka mioyoni mwao lakini kuna siku ukuta huo utavunjwa.

Trump anataka kujenga ukuta mpakani na Mexico, ni dhana iliyo mawazoni mwake na anataka kuifanya iwe halisi. Atajenga sasa lakini kuna siku itafika ukuta huo utabomolewa.

Tuvunje ukuta wa fikra sasa maana ukuta ni kitu kinachotokana na dhana. Dhana huzaliwa, hukua, hubadilika na hata kufa pia. Hivyo nawashauri wasanii kuuvunja ukuta wa fikra badala ya kuanza kumtafuta mchawi.

Alamsiki.


No comments: