Oct 17, 2012

Wasanii, tumieni Jukwaa la Sanaa kutatua matatizo yenu


Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego, akisisitiza
jambo kwenye moja ya midahalo ya Jukwaa la Sanaa

NI ajabu, wasanii kulia kilio cha kuilalamikia Serikali kuwa haisaidii juhudi za wasanii katika masoko na usambazaji kwa ajili ya filamu ambazo ni kwa maslahi kwa watazamaji wa Tanzania, kilio cha kuibiwa kazi za sanaa ingawa kuna uwezekano mkubwa wanaolia kutojua wanaibiwaje kazi zao, lakini wanakwepa majukwaa ya upashanaji habari ambayo yangetumika kufikisha kilio chao na kwenda kusemea pembeni.

Hili ni jambo la ajabu sana! Ni kwewli mfumo wa usambazaji ni mbovu, lakini wasanii wanadharau majukwaa muhimu ya habari na hata vyama na mashirikisho yao wakisahau kuwa umoja ni nguvu. Ikumbukwe kuwa utengenezaji sinema ni jambo linalohitaji sana mgawanyo wa kazi. Kuna waongozaji, waigizaji, waandishi wa miswaada na kadhalika, huku msingi mkuu wa sinema yoyote ukiwa ni mwongozo (script).

Hakuna kisa kinachoweza kuifanya sinema ipendeze bila kuwepo 'storyline' nzuri. Hii inamaanisha kwamba endapo waandishi wa miongozo watafanya utafiti wa kina kwa kuwahusisha watazamaji wa kazi zao kupitia majukwaa ya habari, basi soko letu litaweza kukua zaidi na kuleta tija.


Majukwaa ya habari kama lilivyo Jukwaa la Sanaa linaloendeshwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kila Jumatatu ni jambo la kujivunia, na ni chachu ya kukua kwa Sanaa, kwani Jukwaa la Sanaa ni programu inayomfanya mtu awe na upeo wa kusema, kwa kuwa hapo hutolewa elimu, uratibu na mwongozo, hivyo wasanii wanatakiwa waitumie fursa hiyo badala ya kuikwepa.

Waandaaji wa sinema pia wataweza kujua ni nini hasa kinachoendelea katika hali halisi ya maisha ya jamii kuhusiana na hadithi wanayohitaji. Hii itatokana na midahalo na mahojiano na wadau wa sanaa na watu wengine kuhusiana na hadithi zenye kuakisi maisha halisi ya jamii ambapo pia wataweza kuandaa takwimu ya watazamaji wanapokutana nao katika dunia yao kupitia Jukwaa la Sanaa.

Tatizo ni kwamba tumeingia kwenye biashara ya filamu bila kujua vigezo muhimu vinavyoweza kutuongoza katika dhana nzima ya mafanikio ya biashara ya filamu, kama Jukwaa la Uwasilishaji (Media Delivery Platforms), lakini tunabaki kulalamika.

Nchi yoyote iliyofanikiwa katika filamu watazamaji wake huhitaji majukwaa ya habari, sehemu ambazo hukutana na waandaaji, wasanii na watendaji wengine ili kupashana habari. Falsafa hii ni muhimu kama ambavyo tunapaswa kulitumia Jukwaa la Sanaa ambalo Basata wametupa fursa kwa maana ileile ya jukwaa la uwasilishaji, siyo tu kupashana habari bali hata katika kukuza biashara ya usambazaji wa kazi za sanaa.

Jukwaa la uwasilishaji katika dunia ya kisasa haliishii tu kwenye kupeana taarifa, linakwenda ndani zaidi ya kile hasa soko la filamu linachotaka. Jukwaa husaidia kuwasilisha mawazo kwa watu katika njia itakayojumuisha mitazamo yao.

Ufanisi katika uwasilishaji huweza kuchangia utoaji haki ya kuchagua; yaani kuyaleta maudhui kwa watazamaji katika dunia yao wenyewe. Kulingana na uwezo mkubwa wa soko la Tanzania, Jukwaa la Sanaa kama litatumika ipasavyo ni nyenzo muhimu sana na muafaka kumfanikisha kwa urahisi mtengenezaji wa filamu kuendana na ushindani wa soko.

Tutake tusitake, ili tuweze kupiga hatua tunahitaji nguvu kubwa katika utoaji habari za filamu na kujenga jamii yenye wafuasi kupitia Jukwaa la Sanaa, na humo, mijadala inaweza kujadilika, kipengele muhimu kabisa cha kuleta ufahamu au kampeni ya kujitangaza.

Katika Jukwaa, watu wataweza kupata habari zaidi, kushiriki katika mijadala, kujiunga na majarida, na kubadilishana ujuzi na mawazo na watu wengine, kwa lengo la kupanua wigo mkubwa wa watazamaji.

Hivi kwa nini tunaichezea fursa nzuri kama hii tuliyoipata? Ni kweli tunajua umuhimu wa majukwaa ya kupashana habari au tunadhani ni blah blah? Tujiulize: kwa nini tasnia ya filamu Tanzania ambayo imeshamiri kwenye teknolojia ya video, bado kuna ubabaishaji katika kuhakikisha sekta hii inakua?

Kudhani kuwa watazamaji wa filamu wataendelea na mazoea ya kununua filamu kwa sababu tu zinapatikana au kusambazwa, au watanunua filamu kwa sababu tu eti fulani na fulani wamecheza ni kujidanganya. Tunahitaji kubadilika sasa.

Tunapodhani kuwa tunasukumwa na uzalendo wa kutaka kuliokoa soko letu na majangili wa kazi za sanaa huku tukipuuza jukwaa muhimu linaloweza kutufanya kupaza sauti zetu zikafika tunakokutaka ni kujidanganya. Hili jukwaa linaandaliwa na taasisi ya serikali, ni rahisi kwa serikali kusikia kilio chetu na kuyashughulikia matatizo yetu kama tutalitumia jukwaa kusema. Lakini ni vigumu kupata ufumbuzi kama tunasemea uchochoroni ambako si rasmi.

Ninachokiamini katika ukombozi wa wasanii ni kutumia majukwaa ya habari na kuwa na Umoja wa kweli, wenye nguvu utakaohakikisha kilichokusudiwa kinafanyika huku wanaoongoza wanakijua na kunakuwepo mikakati endelevu katika ustawi na maendeleo ya sanaa. Lakini badala yake wasanii wamelisusa jukwaa la upashanaji habari na kuishia kulalamikia pembeni, wakijengeana chuki, majungu na ubinafsi miongoni mwao huku wakilifanya jukwaa kuwa la wachache tu.

Kwa kutumia majukwaa ya upashanaji habari itakuwa vizuri pia kuuchunguza mfumo wa usambazaji ili kupata ufumbuzi wa kutangaza na kusambaza kazi ambao umesaidia sana kurekebisha tasnia za filamu katika nchi nyingine, ili uigwe katika sekta ya filamu Tanzania. Tunasahau kuwa filamu ni ‘brand’, kama zilivyo brand/ bidhaa nyingine, kuzitangaza na kuzisambaza ni vitu vyenye umuhimu sawa. Lakini si kuzitangaza kwa njia tuliyoizoea ya kuzua skendo ‘feki’ kwenye magazeti ili tuuze.

Kwa tasnia za filamu zilizopiga hatua, filamu za kibiashara huanza na ‘Box Office’ (mfumo maalum unaoanzia kwenye uoneshaji wa sinema ndani ya majumba ya sinema), kutolewa katika njia ya sinema, baadaye kwenye video, kurushwa kwenye vituo vya televisheni za kulipia, katika televisheni za umma, na hatimaye kwenye vyombo vingine saidizi vya habari (video games, katuni na kadhalika) na mwisho kutolewa kama bidhaa rasmi (DVD, VHS) kwa matumizi ya nyumbani.

Huu ni mfumo maalum wa kimasoko nchini Uingereza, Marekani, India na hata Afrika Kusini. Tunapaswa kuanza kujiuliza: kuna tatizo gani katika usambazaji wa filamu Tanzania? Kuanzishwa kwa teknolojia ya digitali katika video na mafanikio yake na kukubalika kimataifa kumefungua fursa mpya katika ulimwengu wa utengenezaji filamu na utaalamu unaoambatana na tasnia hii.

Ukweli kwa sasa, studio kubwa za Hollywood zinajaribu kurekebisha mgawanyo wao katika mfumo wa usambazaji ili kwenda na wakati wa teknolojia ya video, mwaka 2004 mapato yaliyotokana na mauzo ya DVD peke yake yalifikia Dola za Kimarekani bilioni 20.9 ikilinganishwa na dola bilioni 7.4 zilizotokana na tiketi za sinema kwa mwaka huo.

Leo hii, imekuwa ni mkakati wa kimasoko kutumia maonesho ya sinema kama njia ya uzinduzi kwa ajili ya kutoa DVD. Kwa kweli filamu zilizooneshwa zinafikia karibu asilimia 80 ya maktaba za video. Wengi wa watengenezaji filamu huukwepa mfumo wa sinema na kwenda moja kwa moja kwenye DVD, kama ilivyo kwa tasnia ya filamu hapa Tanzania.

Ukiachia njia nyingine inayotumiwa kwenye nchi zilizoendelea ya kujenga jamii ya watazamaji kupitia vyombo vya habari za mtandao (website) kwa kutoa makala, vipande vifupi vya filamu (film clips), njia ya jukwaa la habari ni muhimu sana kufikisha ujumbe kwa watazamaji.

Na baada ya kupashana habari kupitia majukwaa ya habari, tunapaswa kuanza sasa kuzionesha filamu kwenye matamasha ya filamu jambo ambalo linaweza kusaidia sana kuongeza wigo wa taarifa. Matamasha ya filamu husaidia kueneza taarifa miongoni mwa wapitiaji wa filamu na watazamaji, na inaweza kuongeza umaarufu wa filamu na watazamaji kuwa wengi kama mapitio yake yatakuwa ya kuvutia.

Wakati sisi tukiendelea kukaa katika ulimwengu wetu wa 'uvivu wa fikra' sehemu nyingine ya dunia inasonga mbele kwa kasi zaidi kwa kutumia majukwaa ya habari kuliko tunavyodhani.

Hii imekuwa njia nzuri yenye kuleta faida kama tunavyoweza kuona maendeleo kupitia masoko ya nchi zingine. Uwezo wa kiuchumi ni suala lililo nje ya mtazamo wetu na matarajio ya watayalishaji kuendelea kujenga maudhui yatakayoambatana na uelewa huu yanapaswa yaanze sasa kwa kutumia majukwaa ya habari.

Nawasilisha.

No comments: