Oct 24, 2012

Tunahitaji mabadiliko ya kweli na si blah blah


Watanzania wana mapenzi na sinema au michezo ya TV 
kama inavyoonekana kwenye picha hii

NI Jumapili tulivu inayoambatana na mvua ya rasharasha. Watu kadhaa wamejazana kwenye chumba kimoja katika nyumba moja wakiangalia filamu ya kusisimua ya Kitanzania. Tukio (scene) katika filamu hiyo linaanzia pale sebuleni. Ni tukio ambalo linaonekana kuvutia kiasi; linaikamata dunia ya wapenda sinema na kuwafanya watazamaji hawa waamini kuwa wanachokiona ni cha kweli.

Katika tukio hilo la kwenye filamu, sebule inaonekana ni ya kuvutia sana. Vitendea kazi vyote vinavyohitajika kuonesha uhalisia kwenye tukio hilo vimeongezwa. Anaonekana Mama mwenye nyumba akiwa amekaa kwa raha mustarehe kwenye kochi sebuleni kwake. Amevalia nguo nzuri na jozi ya ndala yenye rangi sawa na nguo yake. Katika mkono wake, ameshika gazeti; haonekani kulisoma lakini analitumia tu kwa ajili ya kusukuma muda uende mbele.

Hili ndilo tukio linaloifungua filamu ambayo imeshaingia katika soko, na inauzika kama njugu huku ikipewa ‘promo’ kubwa na magazeti pendwa nchini.

Watayarishaji wa filamu hii wanatabasamu wakihesabu pesa zao, lakini wakati huohuo waigizaji walioigiza kwenye filamu hii wanapokea script nyingine kutoka kwa watayarishaji wengine tofauti ambao wamewaona kuwa wanafaa kupewa majukumu katika sinema zao kufuatia kufanya vyema kwenye sinema hii.

Matukio katika filamu hii yanaendelea, mara, kuna tukio kubwa la kisinema linaonekana: kwenye kioo cha televisheni (screen) anaonekana msanii mmoja mkongwe: na maandishi yaliyoandikwa ‘Miaka 20 baadaye…’

Lakini haichukui muda kwa watazamaji kugundua kwamba ingawa inasemwa kuwa matukio hayo yanatokea baada ya miaka ishirini lakini bado mazingira ni yaleyale na hayajabadilika, hakuna chochote kilichobadilika. Makochi bado ni yaleyale; nyumba bado iko vilevile; mtu bado ni yuleyule (kwa maana ya umri); mavazi bado ni yaleyale; hata mwanamke aliyeonekana sebuleni kashika gazeti bado kavaa jozi ileile ya ndala!

Miaka ishirini baadaye! Watazamaji, kwa hasira, wanaacha kutazama filamu hiyo, mmoja anabadilisha stesheni ambapo sasa wanaangalia matukio ya wiki katika kituo kimoja cha televisheni.

Hii ndiyo tasnia ya filamu ya Tanzania. Karibuni katika ulimwengu wa sekta ya filamu ya Tanzania. Tasnia yenye nguvu Afrika Mashariki na katika nchi za maziwa makuu, lakini inayoonekana kukosa mwelekeo ambao ungeweza kuzifanya filamu zionekane kuwa zimeandaliwa kikamilifu.

Kwa miaka mingi, sekta ya filamu ya Tanzania imeshuhudia kile kinachoweza kuitwa mapinduzi (japo si kamili), angalau katika miaka kumi iliyopita. Kutokana na ongezeko la filamu za Kitanzania majumbani katika miaka ya elfu mbili (baada ya kuzipiga kumbo filamu za Nigeria), mtayarishaji wa filamu nchini amelazimika kupitia hatua moja hadi nyingine, ambapo leo, kama weledi ungezingatiwa nadhani angekuwa katika hatua sita tofauti kuelekea mbele.

Hadi sasa, nje ya Tanzania, hasa katika nchi zinazotuzunguka za Afrika mashariki na za Maziwa Makuu, bado kazi zinazotamba ni zile za watu kama Ron Mulvihill na Marehemu Nganyoma Ng’oge, Profesa Martin Mhando, Profesa Amandina Lihamba na Geoffrey Mhagama.

Hata hivyo, kuna baadhi ya kazi za zama hizi zinazofurahiwa mno, zama ambazo zimeshuhudia wakiibuka watu mahiri kama Mwl. Kassim Al Siagi, Amri Bawji na marehemu Hammie Rajabu. Ingawa filamu zao zilitengenezwa katika mfumo wa analogia (VHS), lakini zimeweza kusisimua hadi leo.

Watayarishaji hawa wa filamu walijitahidi sana kuhakikisha wakisimulia hadithi kuhusu Tanzania, Afrika na watu wake, japo baadhi zilihusu mapigano. Baada ya hapo, miaka ya hivi karibuni mwelekeo wa tasnia ya filamu umeonekana kubadilika mno.

Watayarishaji wa filamu nchini wameonekana kukosa kabisa mafunzo ya msingi ya namna ya kutengeneza kazi zao katika kiwango kinachokubalika licha ya kazi zao kukubalika kwenye jamii ya Kitanzania. Kwa mujibu wa tafiti ninazoziamini, watayarishaji wengi wa filamu nchini ni wabinafsi na wanaowekeza kidogo na kutarajia wavune mara dufu kwa mara moja.

Ubinafsi wao umekuwa ukisababisha filamu za Tanzania zionekane kuwa ni kitu kisichozingatia au kuhitaji taaluma yoyote. Watu wanalipua kazi watakavyo na wanafanya mambo bila kuzingatia utaalam. Wanafanya mambo ili mradi wanajua kuwa watauza na kupata pesa, basi.

Ubinafsi wao umekuwa ni sababu kuu ya kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa sehemu inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Si ajabu kuona anayejiita mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza filamu, ndiye huyo huyo aliyeandika script, ndiye muongozaji mkuu, ndiye muigizaji mkuu, ndiye atakayehariri na kadhalika.

Ni wakati sasa tunahitaji kufanya mapinduzi ya kweli ya tasnia ya filamu na wala tusisingizie bajeti. Mapinduzi yatatuweka kwenye ramani nzuri duniani, ili twende sambamba na nchi za Francophone au Afrika Kusini. Ziko wapi hazina zetu tunazoweza kujivunia katika ulimwengu wa filamu? Ni lini tutashuhudia filamu zetu au wasanii wetu wakipita kwenye zuria jekundu katika matamasha ya filamu ya kimataifa au kwenye tuzo kubwa duniani?

Mwalimu wangu (mentor) aliwahi kuniambia kuwa ninapofikiria kufanya kazi yoyote ya ubunifu lazima nikumbuke kuwa binadamu amezungukwa na matabaka makubwa manne katika maisha ili kuufikia ufanisi wa kazi, matabaka hayo ni: (1) Easy to do; (2) It’s difficult; (3) impossible; na (4) beyond imagination.

Easy to do: hii ni hatua ambayo kila mtu huona kuwa jambo alilokusudia kulifanya ni rahisi na linaweza kufanyika kirahisi tu, ni kama ambavyo watengeneza filamu wa Kitanzania wamekuwa wakifanya kwa kurahisisha kazi zao bila hata kujali weledi wakiamini katika matangazo ‘promo’.

It’s difficult: ni hatua ambayo unaanza kuhisi ugumu fulani kwenye kazi yako na kuanza kuona kuwa ipo haja ya kujali weledi kwa kuanza kuwatumia baadhi ya wanataaluma. Kuna watu huanza kukata tamaa katika hatua hii na kuacha kuendeleza vipaji vyao ambavyo pengine vingewasaidia.

Impossible: ni hatua ambayo utaona kuwa kitu ulichokusudia hakiwezekani, ni kama ambavyo tunaona kuwa haiwezekani kabisa siku moja sinema ya Kitanzania kuwa na ubora kama wa sinema za Hollywood. Au haiwezekani kwa wasanii wa Tanzania siku moja kuwa kama mastaa wengine wa tasnia zilizoendelea.

Beyond imagination: mara nyingi hatua hii inasimama katika ulimwengu wa kufikirika. Ukiishi katika dhana/hatua hii na kuamini kila mtu atakuona umechanganyikiwa. Hii ni hatua ambayo unapaswa kufikiria mambo ambayo kwa wengine yataonekana si ya ulimwengu huu. Kwa mfano; kuwekeza nguvu ukitaraji kutengeneza sinema itakayochukua tuzo ya Oscar.

Hivi kama mtu mmoja angesimama mwaka 1964 (wakati Mandela anaingia gerezani) na kusema kuwa siku moja Mandela atakuwa rais wa Afrika Kusini angeonekanaje, ni mwendawazimu? Kachanganyikiwa? Na vipi kama mtu mwingine angesimama takribani miaka kumi tu iliyopita akaiambia dunia kuwa Barack Obama (mtu mweusi) atakuwa rais wa Marekani angeonekanaje pia? Kapandwa wazimu au anaota ndoto ya mchana?

Lakini leo yote yamewezekana. Kwa nini tusifikirie kuwa kwa kutumia weledi siku moja sinema ya Tanzania itachukua tuzo ya Oscarau wasanii wetu siku moja watapita kwenye zuria jekundu pamoja na kina Will Smith? Kwa sasa huu nao ni wendawazimu, au siyo? Hii ndiyo ‘beyond imagination’, na kila mmoja anapaswa kuishi katika hatua hii huku akizingatia sana katika ubunifu na kujali ubora.

Kwa wenzetu Afrika Kusini, hazina kubwa katika taji la sekta ya filamu ya nchi hiyo ni filamu ya Tsotsi, kazi iliyofanywa na Gavin Hood, iliyoigiza kuhusu vijana waporaji wa Soweto, karibu na Johannesburg, ambayo ilishinda tuzo ya Oscar katika kipengele cha filamu za lugha ya kigeni mwaka 2006.

Si hiyo tu, wana filamu nyingine iliyowahi kuteuliwa kushiriki tuzo ya Oscar ya Yesterday, iliyochezwa na Leleti Khumalo, na ilishawahi kushinda katika tuzo mbalimbali za kimataifa, na U Carmen E Khayalitsha, iliyopigwa katika lugha ya Xhosa ambayo ilishinda tuzo ya Golden Bear mwaka 2005 katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Berlin. Filamu hizi zimetia chachu kwa watengenezaji wa filamu wa Afrika Kusini kuwa wabunifu na wenye kujali ubora (wanaoishi katika beyond imagination).

Faida za ukuaji wa sekta ya filamu ziko wazi, hasa linapokuja suala la kuingiza fedha za kigeni, ushiriki katika uzalishaji na matokeo ya makampuni ya kimataifa katika uwekezaji wa moja kwa moja wa mamilioni ya shilingi katika uchumi.

Tunahitaji kuona siku moja mastaa wa filamu nchini wakiishi maisha mazuri tofauti na ilivyo sasa. Kwa sasa fani hii imekuwa ikiingiza fedha nyingi tofauti na ilivyokuwa awali, lakini maslahi hayo huishia kwa wasambazaji na watayarishaji/wasanii wachache ambao hawashikiki.

Wasanii kwa sasa wamejijengea majina kwenye jamii ya wapenzi wa filamu kufikia kiwango ambacho bila wao kazi hazinunuliki madukani na baadhi ya maprodyuza wameeleza kuwa wengine hata kutokea sura zao ni biashara tosha hata kama wameigiza upuuzi. Lakini nini hatima yao? Kuuza sura bila mafanikio? Mimi nadhani tuanze mabadiliko sasa na tuachane na blah blah.

Naomba kuwasilisha.

No comments: