Oct 9, 2012

Nafasi muhimu kwa Watanzania kujitangaza kupitia Tuzo za Filamu Afrika (AMVCA)


Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania, Barbara Kambogi, akizungumza katika semina fupi ya wadau wa Tasnia ya Filamu nchini pamoja na waandishi wa habari

Mashindano ya Tuzo za Filamu Afrika (AMVCA) yatakayofanyika jijini Lagos, Nigeria Machi 9 mwakani na kushirikisha wasanii na watengenezaji wa filamu barani Afrika yalizinduliwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika hafla iliyoshirikisha makundi mengi ya filamu nchini.

Hafla hii imekuja kufuatia matukio mengine mawili yaliyofanyika mjini Lagos na Nairobi, ambapo AfricaMagic na Multichoice Africa walitangaza mpango wao mpya unaojulikana kama ‘Tuzo za Chaguo la Watazamaji wa AfricaMagic’.


Tangazo hilo la kusisimua lilitolewa wakati wa sehemu ya kisa muhimu cha onesho lililofanyika usiku katika gazeti maarufu la AfricaMagic, linalooneshwa kwenye luninga kwa watazamaji wa DStv katika nchi 47 za Afrika.

Ikiwa imetengenezwa kuadhimisha kipaji cha Afrika katika filamu na televisheni, mbele na nyuma ya kamera, tuzo hizo zitakuwa na vipengele kadhaa muhimu, ambavyo watazamaji watachagua washindi wao moja kwa moja pamoja na vipengele kadhaa vilivyopangwa kitaalamu.

Tuzo hizo zitahusu filamu zilizotengenezwa kwa lugha za Kiingereza, Kiswahili, Kihausa na Kiyoruba zilizotungwa kati ya Mei Mosi, 2011 na Aprili 30, 2012. Aidha jumla ya vipengele 26 vitashindaniwa katika mashindano hayo na kwamba washindi katika kila kipengele watapatikana kwa kupigiwa kura na watazamaji wa filamu barani Afrika sambamba na maoni ya majaji walioandaliwa kwa ajili ya tuzo hizo.

Vipeengele vitakavyoshindaniwa ni pamoja na ‘Msanii Bora wa Kike’, ‘Msanii Bora wa Kiume’, ‘Filamu Bora ya Kiswahili’, ‘Filamu Bora ya Mwaka 2012’, ‘Mwandishi Bora wa Filamu’, ‘Mchekeshaji Bora’, ‘Msambazaji Bora wa Filamu’, ‘Muongozaji Bora wa Filamu’.

Mwisho wa wasanii kutuma kazi zao ni Oktoba 31. Wasanii wa Tanzania wana nafasi kubwa ya kuchukua tuzo nyingi ikizingatiwa kuwa katika kituo cha AfricaMagic asilimia 80 ya filamu zinazorushwa ni za Tanzania.

Hata hivyo washindi wa vipengele vyote vinavyoshindaniwa watapata tuzo maalum za heshima na kwamba, hapatakuwa na zawadi za fedha.

No comments: