Oct 8, 2012

Filamu ya Chungu ni somo kwa waandaaji filamu nchini

Dk. Vicensia Shule, mtayarishaji wa filamu ya Chungu

Filamu ya Kitanzania iliyoandaliwa na Mtanzania na kuongozwa na Mtanzania mwaka huu imeibuka na tuzo ya filamu bora Tanzania katika tuzo zilizotolewa na waandaaji wa tamasha la 15 la maonesho ya Kimataifa ya Filamu kwa Nchi za Majahazi (ZIFF).

Filamu hiyo ya Chungu iliibuka kidedea katika tuzo hizo baada ya kufanikiwa kuwa filamu bora huku pia ikitoa mwigizaji bora wa Tanzania, Richard Mshanga, maarufu kama Masinde ambaye katika filamu hiyo alitumia jina la She Mdoe.


Filamu ya Chungu imezungumzia mazingira ya kijamii hususan masuala ya kishirikina ambapo She Mdoe alikuwa akituhumiwa kama muuaji wa vikongwe kwa tuhuma za kichawi.

Chungu imeandaliwa katika Mkoa wa Tanga eneo la Bumbuli ikiandaliwa na Kampuni ya Shule & Co. na muandaaji wa filamu hiyo ni Dk. Vicensia Shule ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sanaa na Maonesho, na imeongozwa na Kimela Bila.

Kwa kauli yake, Vicensia Shule anasema kuwa katika kuitengeneza filamu hii alikuwa akifanya utafiti, na hii ni filamu yake ya pili ya utafiti katika masuala ya filamu nchini, aliamua kuingia katika fani ya uandaaji wa filamu ili kufahamu changamoto mbalimbali zinazoikabiri tasnia ya filamu.

Pia aliongeza kuwa: Filamu yake ya kwanza ya utafiti ilijikita katika upande wa kutambua tabia za waandaaji, waongozaji wa filamu na tabia za wasanii nchini. Hususan katika mazingira yao ya kazi na maisha yao kwa ujumla na filamu hii ya Chungu ikawa
sehemu ya pili ya utafuti wake huku mara hii akihitaji kujua mazingira ya wasambazaji na kipato kinachotokana na kazi hiyo pamoja na kipato kinakwenda kwa wasanii wenyewe.

Mhadhiri huyo alisema kwamba asingeweza kuandika ripoti nzuri kuhusu tasnia ya filamu nchini bila kuingia katika kazi hiyo kwani kwa kufanya hivyo imemsaidia kujua maisha anayoishi muandaaji wa filamu pamoja na kipato chake, pia amepata kujua maisha ya msanii na muongozaji pamoja na vipato vyao.

na hakuishia hapo, pia amefanikiwa kujifunza maisha anayoishi msambazaji na kwamba baada ya kujua changamoto hizo zote sasa anajipanga kutengeneza filamu itayoweza kuleta mabadiliko katika tasnia ya filamu nchini huku pia akijiandaa kuandika ripoti itakayoweza kutoa njia za kutatua changamoto hizo.

No comments: