Jul 2, 2012

Wasanii maarufu wamepamba tamasha la filamu Tanga

Umati wa watu waliohudhuria tamasha la filamu jijini Tanga

Sehemu ya wasanii nyota katika tamasha hilo

Nyota  mbalimbali wa filamu nchini, akiwemo Wema Sepetu, Jacqueline Wolper, Irene Uwoya, Jacob Steven 'JB' na Vicent Kigosi 'Ray' kwa mara ya kwanza wamepanda kwenye jukwaa moja la tamasha la filamu linalofanyika jijini Tanga lililoanza Jumamosi hadi Julai 6 mwaka huu.

Katika tamasha hilo kumekuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wa Tanga wanaoimba ngoma za asili kama baikoko, mdumange na msanga.



Vilevile kuwa wakiwa Tanga, wasanii hao walitembelea Hospitali ya Mkoa ya Bombo na kutoa misaada ya vyandarua kwa wodi ya wazazi na watoto ili kuwakinga na ugonjwa wa malaria. Kikundi cha taarab cha Tanzania Moto kinachoundwa na wanamuziki waliong'ara East African Melody na Zanzibar Star wamekuwa watasindikiza tamasha hilo.

Mbali na akina Wema, wasanii wengine waliothibitisha kushiriki ni Jacky Pentezel 'Jacky wa Chuz', Aunt Ezekiel, Rich Rich, Sandra, Steve Nyerere, Chick Mchoma, na Issa Mussa 'Cloud'.

Akizungumza jana, Meneja wa kinywaji cha Grand Malt ambao wanadhamini tamasha hilo, Consolatha Adam, alisema Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), imetumia zaidi ya Sh. milioni 90 ili kuandaa tamasha hilo ambalo lengo lake ni kuwakutanisha wadau wa filamu na mashabiki wao.

Alisema kuwa kupitia tamasha hilo wananchi watahamasishwa zaidi kupenda kazi za wasanii wa nchini na vile vile wasanii hao watabadilishana mawazo na mashabiki wao.

"Lengo letu ni kulikuza tamasha hili ambalo linafanyika kwa mwaka wa nne na tunaamini itakuwa ni faraja kwa wadau wa sanaa kukutana na wasanii wanaowaona ana kwa ana na kujifunza kupitia kazi zao," alisema Consolatha.

Mwenyekiti wa Bongo Movie, JB, alisema kuwa wanawashukuru waandaaji wa tamasha hilo na kwamba, wanatarajia kuteua wasanii watatu chipukizi watakaofanya nao kazi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: