Jul 4, 2012

Tupige vita matumizi ya lugha za kigeni kwenye filamu zetu

 Sinema nyingi za Tanzania zimeingia kwenye mkumbo wa kutumia majina ya kigeni

KIPINDI fulani niliwahi kuandika kuhusu suala la mila na utamaduni wa Mtanzania ambapo kwa kiasi kikubwa lilikuwa likinitatiza sana. Nilikuwa nikifikiria sana; tunaposema utamaduni na mila za Watanzania hasa tunamaanisha nini kwa Tanzania yenye zaidi ya makabila 120 ambayo kila moja lina mila na utamaduni wake? Huu utamaduni na mila za Watanzania ni upi hasa?

Haya ni maswali yaliyonitesa kila mara nilipokuwa nikiufikiria utamaduni wa Mtanzania. Lakini baada ya kufanya utafiti niligundua kuwa, neno “utamaduni” linatumika kimsingi katika njia tatu zifuatazo:
-Maonjo ya hali ya juu katika sanaa, vilevile hujulikana kama utamaduni wa juu;
-Mkusanyiko wa maarifa ya kibinadamu, itikadi na tabia ambao hutegemea sana uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kiishara;
-Ni jumla ya mitazamo, kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi, shirika au kikundi fulani.

Utata unaojitokeza kuhusu neno utamaduni wa Mtanzania, niliweza kubaini kuwa utamaduni tunaoweza kuuita hasa wa Watanzania unamaanisha lugha yetu adhimu ya Kiswahili, mwenendo mzima wa maisha katika vyakula, mavazi, ujenzi wa nyumba na tunavyofanya sherehe mbalimbali (harusi, jando, misiba na kadhalika).

Lugha ndiyo njia kuu ya mawasiliano na hubadilika kadiri jamii inavyobadilika. Kiswahili ni lugha ambayo imejitokeza kuwa kielelezo kikuu cha ndani cha jamii yetu. Imekuwa ikitumika kuelezea mila na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania. Ni sehemu ya utamaduni, ni alama ya umoja wa kitaifa na utambulisho wa jamii.

Nimeamu kuandika kuhusu jambo hili baada ya siku za karibuni Wadau wa Sanaa kuhoji uhalali wa wasanii wa filamu kutumia Kiingereza kwenye majina ya filamu zao huku wakishangazwa na kazi hizo kubeba maudhui ya kizungu zaidi.

Mjadala huu uliendeshwa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa na Baqraza la sanaa la Taifa (Basata), ambapo wadau hao walishangazwa na kitendo cha filamu nyingi kutumia majina ya Kizungu wakati hapa kwetu kuna filamu nyingi kutoka nje zinazotumia lugha za Kihindi, Kichina, Kifaransa na zinafanya vizuri.

Ile hoja kwamba, wanatumia majina ya Kiingereza ili kuteka soko la kimataifa ni ya kitoto, wakati hapa kwetu na kwingineko kuna filamu nyingi za Kihindi na Kichina zinanunuliwa kwa wingi! Tumetawaliwa na kasumba ama niite udhaifu katika kutengeneza filamu zenye ubora ndiyo maana tunatafuta visingizio, endapo tutaamua kujikita kwenye ubora wala hatutakuwa na kisingizio cha kutumia majina ya Kizungu.

Nakubaliana kabisa na wadau waliozungumza kwenye mjadala huo, filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi hivyo haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu, ndiyo maana kuna watu wanaangalia picha za Kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea.

Hali hii inajitokeza kwa kuwa sasa tumekumbwa na jinamizi linaloitesa tasnia ya filamu, ambalo ni kukosekana kwa weledi na uhalisia wa tamaduni zetu kunakosababishwa na wimbi kubwa la watu kujiingiza kwenye filamu ili kufanikisha mambo yao yaliyo nje ya maadili na utamaduni wetu.

Watengenezaji wengi kwa sasa wanachoangalia ni namna tu ya kupata pesa pasipo kuumiza kichwa, ndiyo maana hata kazi zetu nyingi tumekuwa tukikopi kutoka Nigeria ambako wao wamefanikiwa kuzitangaza kazi zao kutokana na kutumia hadithi/visa vyao na lugha yao inayowatambulisha duniani (kiingereza aina ya pidgin). Nasi ili tufanikiwe tunapaswa kutafuta utambulisho wetu utakaotusaidia kuuza kazi zetu nje ya mipaka ya nchi yetu, na utambulisho huo lazima uanzie kwenye lugha yetu adhimu ya Kiswahili.

Serikali kutoipa umuhimu tasnia ya filamu ndiyo sababu kubwa ya matatizo yote ikiwemo uchafu, matumizi ya lugha ya kigeni na tatizo la maadili tunalolishuhudia katika filamu zetu, kwani kumekosekana udhibiti wa kazi chafu. Nimekuwa nikijiuliza, kwa nini tunakosa utambulisho? Kwa nini hatuna alama ya mfano wa filamu zetu? Nini chanzo cha wasanii wetu kuigiza na kuiga maudhui na lugha ngeni kwa kisingizo cha soko?

Hapa ieleweke kuwa mapokeo ya kazi za sanaa katika jamii yoyote hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo, mtindo, muundo, maudhui na hivyo hubaki kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio ya jamii husika. Kama sanaa zetu haziakisi maisha yetu, tujue kuwa vizazi vyetu vitarithi mambo yasiyokuwa yetu.

Ni wakati sasa kwa wadau na serikali kupitia vyombo vyenye dhamana kuliangalia hili kwa mapana, vinginevyo tutajikuta tukiwa taifa lisilo na utamaduni wake. Siyo hilo tu, tutajikuta pia tukiwa taifa lenye raia wasio na mwelekeo, wasiojifahamu, wasio na fahari ya utaifa wao, wasio na umoja, mshikamano au heshima mbele ya mataifa mengine.

Ieleweke kabisa kuwa utamaduni huipa jamii utambulisho. Na utamaduni lazima uanzie kwenye lugha (angalia mfano wa Wachina, Wajapani, Wakorea na kadhalika). Sura na haiba ya jamii huweza kueleweka na kuelezeka kutokana na utamaduni wa watu wake. Utamaduni hurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kupitia lugha, sanaa na imani za kiroho. Mila na desturi wanazofuata, matamasha au sherehe wanazoendesha, mavazi yao, chakula chao na taratibu nyingine za utamaduni wanazofuata huunganisha jamii.

Utamaduni kupitia lugha yetu ya Kiswahili ndiyo chombo kinachoweza kutuongoza katika mienendo na tabia zetu. Ndiyo msingi wa maisha ya mtu binafsi. Humuwezesha kujitambua, kuwa na mwelekeo na kujichagulia falsafa sahihi ya maisha yake. Ndiyo msingi wa maendeleo na ubunifu katika jamii.

Ni wakati sasa tuamue kwa dhati (bila unafiki) kukienzi Kiswahili kwa vitendo, na njia iliyo ya haraka inayoweza kuwafikia walio wengi katika kukuza utamaduni wetu wa lugha ni vyombo vya habari, filamu zikiwemo. Hii itatusaidia hata katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi, maendeleo haya katika maana yake pana ni matokeo na sehemu ya utamaduni wa watu. Maendeleo yasiyojengwa katika misingi ya utamaduni wa jamii ni maendeleo yasiyokuwa na maana kwa jamii hiyo.

Huwa inashangaza pale mashuleni wanapofundisha somo la uraia (kwa maana ya raia kujitambua) kwa lugha ya kigeni. Sijajua lengo kubwa huwa ni nini? Watu watawezaje kujitambua kwa lugha ya kigeni? Ieleweke kuwa lengo kuu la utamaduni siyo tu kuwawezesha watu kupata vitu na huduma, bali pia kuwapa fursa ya kuchagua aina ya maisha inayowapa uhalali, furaha na raha ya kuwa binadamu katika jamii yao. Ndiyo maana nadhani hapa Kiswahili kina nafasi kubwa sana.

Hapa Tanzania tuna chombo kinachosimamia lugha ya Kiswahili, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), chombo hiki kilianzishwa mwaka 1967, miaka sita tu baada ya uhuru, kwa ajili ya kukuza Kiswahili ili kiwe lugha inayoweza kutumiwa katika nyanja zote za jamii, utawala, elimu, mafunzo na biashara. Sijajua Bakita wana mpango gani katika kusimamia jambo hili.

Tukumbuke kuwa filamu hizi tunazoziona sasa na kutochukua tahadhari zitakuja kutugharimu baadaye, pale kizazi chetu na kijacho kitakapokuwa kimeshabadilishwa kabisa mtazamo wake. Tutake tusitake, ukweli ni kwamba fani yetu ya filamu kwa sasa ipo katika hatari kubwa ya kuporomosha mfumo mzima wa maadili katika jamii zetu kwani watayarishaji na wasanii walio wengi katika tasnia hii wameshapotea njia kwa kutofuata au kutoijua miiko na maadili katika hadithi wanazoandaa, mitindo na maudhui ya hadithi yanaonekana dhahiri kupotosha kulingana na asili yetu, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.

Hali hii imesababishwa na serikali kutoizingatia sekta hii na kukosa udhibiti wa sanaa huku ikituacha tujifanyie tunavyodhani inatufaa, hili la lugha ngeni kwenye majina ya filamu zetu ni ishara tu ya hatari inayoashiria mporomoko kwa fani hii. Je, kama ni kweli hatua zipi zichukuliwe ili kunusuru au kudhibiti tatizo hili? Bakita mpo wapi katika hili? Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza mnalisemaje hili?

Tupende tusipende, lugha ya kiswahili inayo nafasi ya kuwezesha maendeleo, isichukuliwe kuwa ni njia tu ya kuwasiliana ya watu wasiokwenda shule au wasioweza kuwasiliana kwa Kimombo. Lugha hii ndiyo nguzo ya maisha katika jamii yetu na tunapaswa kuienzi ipaswavyo.

Alamsiki…

No comments: