Jul 18, 2012

Tasnia ya filamu Tanzania: Tumetokea wapi na tunaelekea wapi?

 Jacklin Wolper akiwa na tuzo yake

KATIKA wasanii mastaa ambao wangepaswa kuishi maisha mazuri nchini kwa sasa, ni wale wa filamu ndio wangepaswa kuwa wanashikilia chati za juu kutokana na jinsi kazi zao zinavyotengeneza fedha nyingi. Kwa mujibu wa takwimu, kazi za wasanii hao zimekuwa zikiingiza fedha nyingi katika miaka ya karibuni tofauti na ilivyokuwa awali, lakini masilahi hayo hutofautiana kwani wapo baadhi ambao hawashikiki.

Wasanii wa filamu wamejijengea majina maakubwa kwenye jamii ya wapenzi wa filamu kufikia kiwango ambacho bila wao kazi hazinunuliki madukani na baadhi ya waandaaji wa filamu hizi wamekuwa wakieleza waziwazi kuwa wengine hata kutokea sura zao tu kwenye sinema ni biashara tosha hata kama wameigiza upuuzi!

Lakini tasnia hii ya filamu nchini haikuibuka hivi hivi tu, imeanzia mbali, enzi zile za Kampuni ya Filamu Tanzania (TFC), ambapo sinema zilizokuwa zikitengenezwa zilikuwa katika mfumo wa filamu, hizi hata hivyo hazikuwa filamu za kibiashara. Baadaye sana katika miaka ya tisini ndipo zilipoanza kuibuka sinema za kibiashara. Filamu ya 'Shamba Kubwa' (1995) iliyotungwa na kuongozwa na Mwl. Kassim Al Siagi wa Tanga ndiyo iliyofungua milango ya filamu za kibiashara hapa nchini.

Ikumbukwe kuwa katika miaka hiyo teknolojia ilikuwa bado ndogo na vituo vya televisheni ndo kwanza vilikuwa vimeanza. Wakati huo kulikuwa na vituo vya CTN, DTV na ITV tu ambavyo hata hivyo vilikuwa vikirusha matangazo yake hapahapa jijini Dar es Salaam.

‘Shamba Kubwa’ ndiyo filamu iliyowaibua wasanii ambao baadaye wamekuwa mahiri katika ulimwengu wa filamu, kama Hassan Master, Jimmy Master, Kaini na Amina Mwinyi, ni filamu iliyoteka wengi kwa wakati ule japo teknolojia ilikuwa bado ndogo sana ukilinganisha na hivi sasa.

Baadaye zilifuatia sinema nyingine kama ‘Love Story Tanganyika na Unguja (1998)' ya Amri Bawji, ‘Kifo Haramu’ ya Jimmy Master, ‘Dunia Hadaa (2000)' ya Mwl. Kassim Al Siagi, na ‘Augua (2002)' ya Amri Bawji iliyodhaminiwa na Mfuko wa Utamaduni.

Filamu hizi zilitengenezwa katika mfumo wa analogia (VHS), na hata uhariri wake ulitumia akili zaidi kutokana na teknolojia ya wakati huo kuwa ya kiwango kidogo, lakini zilivutia sana kutokana na maudhui na msuko mzuri wa hadithi.

Utengenezaji wa filamu enzi zile kwa kweli ulikuwa ukitufanya tushindwe hata kuwa na zaidi ya sinema mbili za Kitanzania katika soko letu kutokana na ukweli kwamba teknolojia ilikuwa ndogo, hakukuwa na msisimko wala hakukuwa na soko la kuuzia kazi zetu. Sinema zetu zilikuwa zikihifadhiwa kwenye mikanda mikubwa. Lakini polepole, tukahama na kuyaacha masanduku yale makubwa ya mikanda maarufu kwa jina la VHS na kuhamia kwenye CD maarufu kwa jina la VCD/DVD, ambazo kwa sasa hutufanya kupeana, kuzikusanyaji, kuzihifadhi na kuazimana sinema zetu kirahisi zaidi.

Hata hivyo, kwa wafuatiliaji wengi wa tasnia hii ya filamu, sinema hizi zinaweza kuwa ngeni kwao kwa kuwa wakati huo hatukuwa na mfumo wa usambazaji na hivyo zilikuwa zikioneshwa kwenye majumba ya sinema. Ni filamu ya Girlfriend ndiyo iliyotingisha tasnia ya filamu na kuwafanya watazamaji wa filamu nchini kuanza kutamani kuwa na sinema zao. Wengi wanadhani kuwa sinema hii ndiyo sinema ya kwanza ya kibiashara hapa nchini.

Baadaye zilifuatia sinema nyingine nyingi kama Sabrina, Masaa 24, Fungu la Kukosa, Nsyuka na nyingine nyingi zilizowaburudisha watazamaji japo zilikuwa na makosa ya hapa na pale ya kiufundi, msuko wa hadithi na maudhui.

Mabadiliko yaliyotajwa ya mfumo wa analogia (VHS) kwenda digitali (DVD) yameleta matokeo chanya katika ufungaji wake, uhifadhi wake na kuazimana, hivyo kuongeza wigo wa soko la sinema zote za Kitanzania katika maeneo mengi ya duniani, hasa katika maeneo ambayo jamii ya Waafrika Mashariki na Waafrika wengine wanakopatikana.

Pamoja na juhudi ambazo baadhi yetu tumekuwa tunazifanywa za kutaka ziwepo juhudi za kuvutia wawekezaji zaidi na zaidi ambao wanaweza kuwa msaada mkubwa katika tasnia hii, bado kuna kikwazo kikubwa kinachosababisha kuzipunguza juhudi hizi na kwamba; kiwango cha uigizaji bado kimeendelea kuwa cha chini mno kwa kiasi kikubwa, na kufanya udhalilishaji kuongezeka kwa kiwango kikubwa, hasa kwa mabinti.

Haitakuwa haki, hakutakuwa na uwiano au utakuwa ni ukosefu wa fadhila kusema kwamba, kwa ujumla, hakujawahi kuwepo maendeleo katika tasnia hii japo kidogo au maboresho katika tasnia kwa njia na namna ambavyo script zimekuwa zikifasiriwa na waigizaji wa Tanzania.

Pamoja na mambo mengi ambayo yamekuwa yakifanyika ambayo yanafanywa ili kusukuma mbele uzalishaji (matumizi ya vifaa vya kisasa vya Hi-tech), ubunifu na namna kazi zinavyoandaliwa tayari kwa kuuzwa (packaging), ni sababu moja tu tunayoitarajia kuboresha kazi zetu sambamba katika kiwango cha uigizaji. Cha kushangaza, waigizaji wengi wa Kitanzania bado wanaruka juu ya rada duni sana.

Suala la kushangaza, tuzo kadhaa zimekuwa zikiandaliwa nchini ili kuwatuza waigizaji hawa ambao kiukweli kazi zao bado hazijaweza kuboreka. Tuzo hizi ni kama vile za kupeana tu ili tusivunjane moyo. Wakati fulani huwa najiuliza... kwa nini hatuandai warsha za mafunzo na semina kwa waigizaji hao kama kweli tumedhamiria au tunataka kuwatuza? Kiwango chao kidogo cha uigizaji na mahitaji yao ambayo badala ya kukimbilia kuwapa tuzo ambazo pengine hazitawasaidia sana zaidi ya kuwafanya wavimbe kichwa, basi tuangalie namna ya kuwasaidia kuboresha kazi zao ili waweze kuuza kimataifa.

Ukweli, kutokana na kukosa mafunzo ya taaluma ya filamu, si waigizaji tu bali hata watengenezaji wa filamu nchini wamekuwa ni watu wanaolipua kazi, wasiojali ubora, wanaoshindwa kubuni na kujikuta wakiishia kunakiri kazi za nje na hata kazi zao nyingi hazizingatii mambo muhimu kwa kisingizio cha bajeti hata kwa yale mambo ambayo hayahitaji bajeti kubwa.

Pia kukosa mafunzo kumewafanya kutokuwa na uthubutu kwa sababu wamejawa na woga, jambo ambalo limekuwa linarudisha nyuma maendeleo ya tasnia hii. Wasanii wa Tanzania wamekuwa wakikwepa kuhudhuria makongamano mbalimbali yatakayowakutanmisha na wataalamu nadhani kwa hofu tu ya kutokujiamini.

Nchi yetu imekosa kabisa mfumo mzuri ambao ungesaidia kumuendeleza msanii wa Tanzania na hatuna vyuo vinavyotoa mafunzo yanayojikita kwenye filamu tu kama ilivyo kwa jirani zetu Kenya au Afrika Kusini, lakini bado siamini kuwa kuendelea kuitegemea serikali itusaidie au elimu ya darasani ndiyo suluhisho pekee katika kupata mafunzo ya weledi.

Kuna njia nyingi za kupata elimu kama semina, warsha au makongamano ambazo zinaweza kuwa suluhisho japo kwa kiwango fulani na kuwafanya wasanii kufanikisha maendeleo ya tasnia ya filamu nchini na kuitangaza Tanzania ipasavyo nje ya mipaka yake.

Tuzo tunazowapa sasa inawezekana, katika mawazo ya waigizaji hao au wanaamini kuwa, wao ni bora lakini kumbe linapokuja suala la kuonekana kwenye skrini, wanabakia kuwa ni watu wenye kiwango duni na wanaoboa siku zote japo wamepewa tuzo. Kama kweli, tunahitaji kuona ukuaji mkubwa wa sekta ya filamu nchini, ni lazima tuangalie zaidi namna tunavyoweza kuboresha kazi zetu kwa kutumia teknolojia na kuzingatia maendeleo ya binadamu.

Safari ya tasnia yetu ya filamu kwa kweli imekuwa ni ndefu mno na hatujui lini tutafika kwenye maendeleo, au mapambano yetu ya kuhakikisha kuwa na sisi tunapata kutambuliwa kimataifa na kukubalika bado yanaendelea ingawa kwa kiwango hafifu. Lakini hadi pale tutakapoamua kufanya tathmini kwa waigizaji wetu, namna tunavyowapata ili washiriki kwenye kazi zetu na miundo ya mafunzo katika tasnia, uboreshaji katika uzalishaji wa kazi na kutokuachwa nyuma na teknolojia.

Sekta ya filamu Tanzania imesafiri njia ndefu sana hasa tunapoangalia katika suala la muda, lakini linapokuja suala la ukuaji ili kujilinganisha na maendeleo ya haraka katika sekta za filamu za nchi zilizoendelea duniani, inaonekana wazi kuwa tunayodai ni mafanikio tuliyoyapata ni sawa na fizikia ya muda wa safari... Hakuna uhalisia kabisa!

Hivi tumekwenda umbali upi? Ukweli tunaonekana kusimama palepale katika jiwe lile lile lisilotembea (unmovable stone).

Alamsiki…

No comments: