Jun 20, 2012

Dk. Mgimwa, hili la stampu za TRA na kuirasimisha tasnia ya filamu ni sawa, lakini…

 Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa

“MHESHIMIWA Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-

“Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wasanii kudurufiwa kazi zao za sanaa na kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya. Ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato itaanza kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu kwa nia ya kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo vya kudurufu kazi za sanaa (piracy of artists work) hali ambayo inadumaza ukuaji wa sanaa na vipaji hapa nchini.

“Aidha, Mamlaka ya Mapato itaweka stampu kwenye bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi na kuwawezesha wasanii kupata kipato stahili kutokana na kazi zao. Vilevile hatua hii itaiingizia serikali mapato. Kwa kuwa yanahitajika maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa hatua hii utaanza rasmi tarehe 1 Januari, 2013…”

Haya ni maneno katika hotuba yako ya bajeti kwa mwaka 2012/13 yaliyonigusa wakati ukiiwasilisha mbele ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wiki iliyopita.

Kwanza napenda kukupongeza kwa kuteliwa kushika nafasi hii nyeti ya uWaziri wa Fedha, nikiamini kuwa sasa ‘ngoma imepata mpigaji’ kutokana na weledi wako. Pili nikushukuru angalau kwa kuonesha kuutambua mchango wa sekta ya burudani (filamu na miziki) hapa nchini. Lakini ikumbukwe kwa miaka mingi sasa, wasanii na watengenezaji wa sinema miongoni mwa wadau wengine wa sekta ya burudani wamekuwa wakitoa sinema ili kujipatia riziki kutokana na kazi yao bila mafanikio. Ingawaje sekta ya filamu ni sekta yenye thamani ya mabilioni ya fedha, lakini wengi wao wameishi na kufa maskini.

Waziri, naamini kabisa hotuba yako inaashiria kuwa Serikali imekusudia kusaidia sekta ya burudani ikue na kuleta tija kwa nchi yetu, lakini nina wasiwasi kama kweli unaifahamu nguvu ya soko la filamu (the dynamics of the home-video industry). Je, unadhani piracy ndiyo tatizo pekee lililopo katika soko la filamu nchini? Hivi stampu katika mazingira ya soko la sasa ni tiba kweli kwa maendeleo ya sekta ya burudani? Unaelewa kuwa sekta ya filamu imefukarishwa kwa makusudi na watu wachache kwa maslahi binafsi?

Je, unaelewa kuwa utengenezaji wa filamu kwa soko la Tanzania unatafsiriwa kuwa sawa na biashara ya barafu inayoweza kumyeyukia aliyenayo mikononi wakati wowote? Unafahamu kuwa hali hii huwafanya watengeneza filamu wa Kitanzania wajikute wakiingia mikataba haraka ya kupata pesa japo kiduchu kabla barafu haijawayeyukia na kugeuka maji? Wakati mwingine bila hata kurudisha gharama walizoingia!

Mi nadhani ili kuleta ufanisi katika sekta hii serikali inapaswa kuziagiza mamlaka husika kuandaa takwimu za kina kuhusu soko la filamu na kuzitazama fursa zilizopo kabla ya kuamua chochote. Na yote haya yatategemea sera nzuri ya filamu itakayokuwa imeanzishwa. Serikali pia inapaswa kuandaa jopo la wataalam watakaoangalia kanuni zilizopo kwa lengo la kuoanisha na kuhuisha kiini cha sera mpya ya filamu. Sera ya filamu ndiyo hati pekee yenye kueleza kwa ufasaha uwezekano mbalimbali katika kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa filamu.

Sera hii inapaswa iende mbali zaidi ikizingatia mchakato wa utoaji wa filamu na uanzishwaji wa haki za usambazaji wa miliki. Katika mchakato huu, wasambazaji wenye leseni watatarajiwa kuwasilisha ripoti ya kila wiki ya kisheria katika shughuli zao za usambazaji ambayo inaweza kutumiwa katika kutathmini utendaji wa kifedha wa filamu.

Waziri, hotuba yako imebeba maswali mengi kuliko majibu. Hivi unadhani stampu za TRA pekee zinatosha kuleta ufanisi katika soko la filamu bila hata kuijua nguvu ya soko? Mbali na stampu hizi je, kuna mikakati gani katika kudhibiti kazi zisizo na mhuri? Je, mlaji atatofautisha vipi mhuri halali na batili? Hivi hudhani kuwa ili zoezi hili lifanikiwe inahitajika elimu kwa walaji?

Ni mechanisim gani itakayotumika kuweza kutekeleza hilo na je, msanii atahakikisha wapi kipato chake? Kwenye stampu au wapi? Nasema hivi kwa kuwa hata kazi feki nayo inaweza kuwekewa stampu na atakayenufaika ni msambazaji na TRA!

Waziri, hivi unajua kuwa mfumo wa biashara ya filamu nchini umekaa kienyeji sana? Je, mna mpango gani katika kuandaa miundombinu ya soko la filamu ili wasanii na watengeneza filamu pia wafaidi jasho la kazi zao tofauti na ilivyo sasa? Je, Serikali ikisharasimisha sekta hii, itawekeza au ndiyo itaingia kwenye mpango wa kuvuna pasipo kupanda? Sidhani kama itakuwa busara kwa serikali (kupitia Mamlaka ya Mapato) kukusanya mapato wakati haijengi miundombinu ya soko, haijengi shule zitakazowasaidia wadau wa filamu, wala haisaidii katika kutafuta soko!

Hapa hata mkikusanya kiasi gani, bado haitatusaidia kama elimu kwa wasanii na wadau wengine haitatolewa. Hivi kuna vyuo vingapi vinavyofundisha filamu? Hivi hudhani kuwa sheria hii mnayopitisha sana sana itambana msambazaji/muuzaji kuhakikisha analipa kodi lakini haitamsaidia mtayarishaji/msanii ambaye ataendelea kunyonywa kama kawaida?

Ukiiangalia kijuujuu utadhani ni jambo zuri, lakini ukweli mnatengeneza bomu kwa tasnia ya burudani, bomu ambalo limeleta mgogoro mkubwa katika nchi ya Ghana sababu ya msingi ikiwa ni ndogo tu, kazi ya Mamlaka ya Mapato si kulinda haki za wasanii bali ni kukusanya kodi. Kazi ya kulinda haki hizi iboreshwe katika vyombo vya wasanii husika ili TRA iweze kupata takwimu sahihi za kukusanya kodi.

Waziri, hivi unafahamu kuwa hata hizo DVD zinazoitwa za wizi huwa zinalipiwa kodi TRA? Kama hufahamu fuatilia utagundua, kisingizio cha TRA ni kuwa wao hawajui kipi halali na kipi si halali, kwa msingi huu TRA wamekuwa wanakusanya kodi ya kazi za wizi za wasanii siku zote.

Tunahitaji chombo chenye mfumo ambao utaweza kudhibiti aina na aina ya wasambazaji, kutoa miongozo kwa ajili ya usajili na leseni ya wasambazaji (ambayo ada fulani wanatarajiwa kulipwa), na kubainisha aina ya haki za usambazaji ambayo wasambazaji katika ngazi mbalimbali wataendelea kumiliki pamoja na udhibiti ili kuhakikisha kuwa haki hizi zinalindwa.

Chombo hiki (kama kitakuwa ni TRA au hiki nitakachokijadili baadaye) kiambatane na kuwepo kwa sera mpya itakayoonesha pia sifa zinazopaswa kuchukuliwa katika mkataba halali wa usambazaji ambao pamoja na mambo mengine, utalazimisha wahusika kuandikisha filamu zao kama miliki (intellectual property). Moja ya masuala ya ubunifu wa sera ya uzalishaji wa fedha na ulinzi ambayo nadhani sera inayopaswa kuwepo ni ya kutoa ufadhili kwa wamiliki wa haki za filamu.

Ni bora kwanza serikali ikaufahamu msingi imara unaohitaji mipango madhubuti na ya lazima katika kuiwezesha sekta ya filamu, nimewahi kushauri kuwa mngeuchunguza mfumo unaotumiwa na Afrika Kusini kupitia chombo chao maalum cha kusimamia na kuwawezesha watengeneza filamu “National Film and Video Foundation (NFVF)” kama mmekusudia kuisaidia sekta hii.

Kwa nini msianzishe chombo maalum chenye nia ya dhati kuwasaidia wadau wote katika sekta ya filamu ambacho kitakuwa na idara tano, vinginevyo mipango yenu itaishia kwenye makabrasha kama ilivyokuwa kwa mipango mingine. Ni kawaida yenu kuja na mipango mizuri lakini utekelezaji unakuwa mbovu, hali kadhalika tusingependa kuona suala hili liishie kuwa ndoto ya alinacha.

Kama hujawahi kusikia au kusoma makala zangu, nimewahi kuishauri serikali mara kadhaa kuwa tunahitaji kuwa na chombo chenye idara tano katika kuleta ufanisi kama ifuatavyo: Idara ya utoaji wa taarifa za upatikanaji wa pesa na kutoa fursa kwa watengeneza sinema. Idara ya kuandaa takwimu za kina na kutoa fursa ya kuzitangaza filamu za Tanzania katika masoko mengine ya Afrika, na duniani na hivyo kuongeza uwezekano wa kuuza kazi zetu kimataifa na kuigiza pesa za kigeni.

Idara itakayowasaidia wadau katika sekta ya filamu kupata mafunzo ya weledi (professionalism). Idara itakayosimamia mapato yatokanayo na filamu. Na Idara itakayosimamia kwa ukamilifu sheria za uharamia/wizi (piracy) wa kazi za sanaa na hivyo kuwafanya watengenezaji wa kazi hizi kutokuwa na hofu ya kupoteza mapato yatokanayo na kazi zao.

Alamsiki…

No comments: