Jun 20, 2012

Gaba Arts Centre na Basata watoa somo kwa wasanii wa filamu


Mkurugenzi wa asasi ya Gaba Arts Centre, James Gayo, akisisitiza jambo wakati akitoa mafunzo kwa wasanii wa filamu juu ya Stadi za Uandishi wa Miswada ya Sinema (Script) kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata)

Asasi ya Gaba Arts Centre na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) Jumatatu ya wiki hii 18, Juni 2012, saa 4 kamili kwenye jukwaa la sanaa waliendesha semina fupi kwa Wadau/wasanii wa filamu ili kuwajengea weledi katika eneo la uandishi bora wa miswada ya sinema (scriptwriting).

Warsha hiyo ya saa mbili ilihusu zaidi Stadi za uandishi wa miswada ya Sinema (Script writing skills), baadhi ya mambo yaliyojadiliwa ni:

- Namna ya kuendeleza wazo hadi sinema ya kusisimua (Idea to a good film)
- Namna ya kufikia hisia za watazamaji (Reaching Audience emotion)
- Ujenzi wa Action na Dialogue nzuri.
- Kutengeneza Wahusika (Characters)
- Mfumo wa hadithi, Mwanzo, kati na Hitimisho ( Ploting, beginning, middle and end)

Ilikuwa ni fursa nzuri kwa Wasanii katika kuleta mabadiliko kwenye tasnia ya filamu kwani kumekuwa na changamoto mbalimbali katika tasnia ya filamu ambazo kwa njia moja au nyingine zimekuwa kikwazo katika kufikia ufanisi unaohitajika.

Akitoa mada kwenye programu hiyo maalum, Mkurugenzi wa asasi ya Gaba Arts Centre, James Gayo, alisema kuwa muda umefika sasa kwa wasanii wa filamu kusaka maarifa ili kutengeneza sinema zenye visa vipya, zenye weledi na zisizosukumwa na matakwa au maelekezo ya wasambazaji.

“Wenzetu kutoka nje wanatamani
sana kupata vitu kutoka Afrika vyenye kuzungumza uhalisia wa maisha ya kwetu, wanataka kuona vitu vipya hivyo, katika uandishi wa muswada wa sinema suala la uhalisia na visa vyenye utofauti ni la msingi sana” alisisitiza Gayo.

Alizidi kueleza kuwa watazamaji wa sinema (filamu) huwa wana kawaida ya kuchoka pale wanapolishwa visa vya aina moja muda wote na akaonya kuwa
kama wasanii hawatajikita katika kubuni visa vipya na vyenye kugusa uhalisia wa maisha yao wadau watasusia kununua.

“Ikiwa tutaendelea kutengeneza filamu zisizo na weledi, zenye visa vilevile na zenye kusukumwa na wasambazaji au haja ya kuchuma fedha za haraka tu watu watatuchoka na baadaye soko litakufa” alionya Gayo.

Gayo ambaye amepitia mafunzo ya utengenezaji filamu katika mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani alitaja sifa za muswada (script) bora kuwa ni pamoja na kubeba wazo linalozalika kwenye jamii, visa vyenye uhalisia na vipya, utengenezaji mzuri wa wahusika na sifa zingine nyingi.

No comments: