Aug 2, 2011

JUKWAA LA SANAA: Kampuni ya usambazaji ya Steps Entertainment yalalamikiwa

 Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego akieleza jambo

 Mwakilishi wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu, George Tailo

Baadhi ya washiriki wa Jukwaa la sanaa

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kupitia program yake ya kila wiki ya Jukwaa la Sanaa Jumatatu wiki hii imewakutanisha wasanii na Kampuni ya usambazaji wa kazi zao ya Steps Entertainment, kwa lengo la kuja na mikakati ya pamoja ya uboreshaji wa soko. 

Wakizungumza kwenye Ukumbi wa Baraza hilo, wasanii wengi walitupa lawama kwa wasambazaji hao kwa kile walichodai kwamba, wamevuruga mfumo wa usambazaji wa kazi zao hapa nchini kiasi cha kufanya wasambazaji wengine waliokuwepo kushindwa kuhimili.

Walizitaja sababu zilizosababisha kuvurugika kwa mfumo wa usambazaji wa kazi za wasanii kuwa ni pamoja na wasambazaji hao kushusha bei za CD/DVD hadi shilingi elfu moja, kutokusambaza kazi za wasanii wanaochipukia hadi zishirikishe wasanii maarufu na kutokuwepo kwa mfumo eleweka wa bei.

Pia wasanii hao wameitaka kampuni hiyo kufuata maadili ya utamaduni wa Tanzania wakati wa kusambaza kazi zao kwa jamii ili kujenga maadili mema. 

Katika  jukwaa hilo la sanaa, mada ilikuwa ni mafanikio na changamoto za soko la filamu ndani na nje ya nchi. Mmoja wa wasanii hao, Mike Sangu, alisema kampuni hiyo haifuati maadili ya nchi kutokana na wasanii wanaoigiza katika kazi zao hawana maadili kutokana na mavazi yao katika filamu hizo wanazosambaza. Kwa hiyo aliitaka kampuni hiyo kufuata maadili pindi wanaposambaza kazi zao.

Akijibu hoja hiyo Meneja wa Uzalishaji wa Kampuni ya Steps Entertainment, Ignatus Duncan (Kambarage) alisema filamu zao zote zinakaguliwa na bodi ya filamu nchini kabla hazijakwenda sokoni na kuwafikia Watanzania, hivyo wao hawapaswi kulaumiwa.

Pia Mkaguzi wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu nchini, George Tailo, alisema ni kweli kampuni hiyo inapeleka filamu kwa ajili ya ukaguzi, lakini asilimia kubwa ya filamu wanazopeleka ni zile zilizochezwa na wasanii wachanga lakini za wasanii wakubwa haziwafikii.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego, alisema kwamba, tatizo linalojitokeza ni kwa baadhi ya wasanii ama kutozingatia mikataba au kutokujua umuhimu wake hivyo kuahidi kuandaa programu maalum ya elimu ya mikataba kwa wasanii.

“Ndugu zangu kupitia Jukwaa hili nimejifunza kwamba, wasanii hatuzingatii mikataba na hata hatuoni umuhimu wake. Baraza sasa linajipanga kuwaleta wataalam mbalimbali wa mikataba na hakimiliki ili kuwajengea uelewa wasanii,” aliahidi Materego. 

Aidha,aliwaahidi wasanii kwamba, Basata kwa kushirikiana na Mashirikisho ya Sanaa nchini litaandaa utaratibu wa kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa bei unaoeleweka kwa kazi za wasanii

1 comment:

Anonymous said...

Serikali inapaswa kuwa makini na hawa wasambazaji (Steps) kwa kuwa inavyoonekana hapa kuna mchezo mchafu unafanyika. Wasanii na wadau wote wanapaswa kushikamana na kuzitambua haki zao ili kushinda vita hii. Thanx mr. Hiluka kwa kutuelimisha.