Aug 29, 2011

NAOMI: Filamu ya mwisho ya marehemu Tabia

Marehemu Dalillah Peter Kisinda (Tabia)

 Kava la filamu ya Naomi (part 2)

TASNIA ya filamu nchini mwetu imezidi kukua na kuendelea kuua soko la filamu kutoka Nigeria ambazo mwanzoni mwa miaka ya 2000 zilikuwa zimeliteka soko la nchi yetu. Tofauti na ilivyokuwa miaka michache iliyopita, kwa sasa takriban, filamu mbili mpya za Kitanzania hutoka kila wiki na hali inaonesha kwamba idadi hiyo itazidi kupanda miaka michache ijayo, hasa kama watengeneza filamu wa Tanzania wataboresha zaidi kazi zao.

Moja ya filamu inayosubiriwa kwa hamu ni ya Naomi, iliyotayarishwa na mmoja wa Watunzi mahiri wa hadithi nchini na mtengeneza filamu, Hamisi Kibari.

Kibari anasema tayari wameshasambaza mabango ya filamu hiyo ambayo ndiyo filamu ya mwisho kushiriki marehemu Dalillah Peter Kisinda, aliyetamba na kundi la Kidedea akijulikana kwa jina la ‘Tabia’.

Kila kitu kimekamilika na tulikuwa tunabishana na wenzangu kuhusu tarehe nzuri ya kuingiza filamu yetu sokoni. Tumepanga iwe wiki ya kwanza mwezi ujao wa Septemba,” anasema Kibari.

Kibari anayeshirikiana na Bishop Hiluka ambaye ni mtaalamu aliyebobea katika utengenezaji wa sinema nchini, anasema kilichomuondoa sokoni ni kutolipwa vyema kazi yake ya mwisho aliyoitoa mwaka 2007 ya Mtoto wa RPC sehemu ya Pili, lakini akasema kwa sasa amekuja na nguvu mpya, mkakati tofauti na hatorudi nyuma.

Nilipouza Mtoto wa RPC namba moja, nililipwa vyema malipo yangu lakini tatizo likaja kwenye namba mbili. Kwa kweli ilini-discourage (ilinikatisha tamaa) hadi nikaamua kwanza nikae pembeni. Kwa kifupi nilizichukia hata filamu zenyewe,” anasema Kibari.

Mtunzi huyo amesema kitu kingine kilichokuwa kinamkatisha tamaa ni tabia ya msambazaji mmoja mkubwa kufanya mambo ambayo ni kinyume na taaluma ya filamu kama vile kulazimisha kila filamu iwe na namba moja na namba mbili hata kama msingi wa hadithi yake hauruhusu hilo.

Na hili kwa kweli ni wizi mtupu. Kwa vile soko limejikuta likiaminishwa kwamba sinema huwa na sehemu mbili, part I na II na sisi tumelazimika kufanya hivyo katika Naomi lakini kwa namna inayokubalika kitaaluma,” anasema.
Anasema baada ya kukaa muda mrefu akiwa nje, ameamua kurudi na ana hakika ataliteka soko muda si mrefu baada ya kufanya utafiti na kugundua udhaifu uliopo.

Kuna udhaifu mkubwa upande wa hadithi na hapo ndipo mimi ninataka kupafanyia kazi… Zipo filamu chache nzuri nimeziona lakini nyingi kwa kweli hazinivutii kwa upande wa hadithi ingawa mambo mengine kama locations (maeneo), mavazi na hata upigaji wa picha na uhariri wanajitahidi,” anasema Kibari na kuongeza kwamba hafurahishwi na mavazi yenye ukakasi ya baadhi ya wacheza filamu wa kike ambayo wao wamejitahidi kuyaepuka katika Naomi.

Kuna filamu nilipata aibu sana kuziangalia na wanangu sebuleni kabla ya kuzikagua… Mimi na Hiluka tutajitahidi sana kuliepuka hilo. Tutaleta filamu ambazo familia itaziangalia bila ukakasi wowote,” anasema Kibari ambaye anaisambaza filamu hiyo ya Naomi peke yake.

Amesema, yeye na Hiluka, licha ya kuwa watunzi, wana kisima cha hadithi ambazo bado kimejaa tele.

Mimi ninazo hadithi nyingi na pia ninaweza kuchukua wazo dogo la mtu na kulikuza kuwa hadithi kubwa. Kwa mfano, hivi sasa tunajiandaa kushuti filamu nyingine iitwayo Mzimu wa Maisara ambapo nimechukua wazo dogo sana la mtu mmoja anayeitwa Sydney Madenge lakini hata yeye ameshangaa kwa jinsi nilivyolitengeneza na kuwa kisa kitakachowashitua waangaliaji wa sinema,” anasema na kuongeza kwamba hata katika Naomi sehemu ya kwanza imetungwa na mtu mwingine, yeye akakuza wazo hilo kwa namna yake kwa kuandika namba mbili.

Ukiangalia namba moja inakutosheleza kabisa na hata ukiangalia namba mbili pekee bila kuona namba moja unatosheka. Huu ndio utakuwa mtindo wetu sisi na hata taaluma inatufundisha hivyo,” anasema.

Amesema ingawa kuna mahala wamelazimika kufuata soko lilivyoharibiwa, lakini kadri watakavyokubalika watabadilisha msimamo huo.

Hatuna sababu ya kulazimisha filamu ziwe mbili kwa kuzikata katikati. Inatakiwa hadithi ndiyo iamue urefu ama ufupi wa sinema,” anasema.

Kibari amesema udhaifu mwingine ambao anauona na anataka kupambana nao hata kama itamchukua miaka kadhaa ni watu kudhani kwamba filamu nzuri lazima zitokane na majina fulani ya watu.
Kuna wakati haya yanayoitwa majina makubwa wanafanya vizuri kweli lakini filamu zao nyingi si nzuri kama ambavyo mtu ungetegemea. Mbaya zaidi wanalazimisha kuigiza wao hata mahala ambapo hawafai na angelifaa mtu mwingine. Kwa mfano, niliwahi kuona wanalazimisha kuigiza kama wanafunzi… Wewe ulishaona wapi mwanafunzi wa kawaida ana kitambi, ana nywele zenye mawimbi… uliona wapi?” Alihoji

Kibari anasema kwa kuanzia na Naomi, yeye na Hiluka wanataka kuanza mkakati wa kuwafanya Watanzania wagundue kwamba filamu nzuri si majina ya watu bali mambo makuu sita; hadithi nzuri, muongozo (script) ulioandaliwa kitaalamu, washiriki waliochaguliwa vyema na si majina yao bali kumudu kuvaa uhusika, muongozaji mahiri (director), upigaji picha mzuri na uhariri makini.

Inanisikitisha sana kusikia mtu ukimwambia kwamba tunaandaa filamu, anaanza kukuuliza, yumo fulani, yumo fulani… Jamani, filamu hata kama majina ya watu yanaweza kuwa muhimu lakini hayapo katika vigezo vya kuifanya filamu iwe nzuri,” anasema.

Kibari anasema kwamba hata kama mpaka sasa baadhi ya filamu za hao wanaoitwa wenye majina zinafanya vizuri ni kutokana na ama kutangazwa sana kulinganisha na zinazowashirikisha wasanii wachanga ama kutokana na kasumba iliyopo sasa ya kuamini katika majina.

Tunataka kujaribu kuua hii dhana… Si kwamba hatutashirikisha majina makubwa kwa sababu hata katika Naomi wamo, lakini hatutakuwa watumwa wa hilo,” anasema Kibari.

Kuhusu filamu ya Naomi, Kibari amewataka watu kuinunua kwa wingi ili kuanza kuona uhondo mpya unaokuja, hatua ambayo itamwezesha kuandaa vitu vikali zaidi.

Tumeipiga Naomi katika bajeti finyu kidogo, lakini ninamini watazamaji wakituunga mkono kwa kuinunua kwa wingi bila kutuibia basi watakuwa wametusaidia kutuwezesha katika kuboresha kazi zatu zijazo,” anasema.

Kibari amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kununua nakala halali ili kusaidia kukuza kipato cha wasanii na Watengeneza picha nchini.

Kwa kweli filamu ingeweza kusaidia sana katika soko la ajira na kuongeza mapato ya serikali kama serikali itasimamia tasnia hii vizuri kwa kuzuia wizi wa kazi za sanaa, lakini ninachosikia zaidi kutoka kwa viongozi wetu ni porojo,” anasema Kibari akiahidi kulizungumzia hilo kwa kina katika mazungumzo yajayo na gazeti hili.

Mbali na Mtoto wa RPC, Kibari ambaye pia ni Mhariri wa Gazeti la kila wiki la Kulikoni ameshatoa filamu za Usikose Mazishi Yangu na Usiku wa Taabu. Kabla ya kuhamishiwa Kulikoni aliwahi kuwa Mhariri Mshiriki wa Nipashe na pia aliwahi kuwa Mhariri wa gazeti la Komesha ambalo kwa sasa halipo.


SORCE: NIPASHE Septemba 1, 2011



No comments: