Bayport

Bayport

fofam

fofam

imetosha

imetosha

Ads

Ads

Jul 28, 2011

TUJADILI: Upi mfumo unaotufaa wa usambazaji wa filamu zetu?

 Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Simon Mwakifwamba

IJUMAA iliyopita nilielezea udhaifu wa wasanii kutojitambua unaotokana na kulewa umaarufu, pia niliuliza swali kama sanaa zetu zilivyo leo zinaweka kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo na kuashiria historia inayolingana na mila na desturi nzuri za kizazi husika. Au kama tunaweka kumbukumbu potofu ya sanaa zetu na uasili wake kwa vizazi vijavyo?

Leo najaribu kuangalia kwa makini kuhusu mfumo wetu wa usambazaji wa kazi za sanaa (hasa filamu) kutokana na sababu kuu mbili: kwanza nimepokea meseji kadhaa za wasomaji mbalimbali zilizonisisitiza nieleze namna tunavyoweza kujikwamua katika usambazaji na namna gani tunaweza kufanikiwa kuondokana na uharamia wa kazi za sanaa.

Sababu nyingine iliyonifanya kuibua mjadala huu ambao nawakaribisha wasomaji wachangie mawazo yao, ni baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Filamu nchini (TAFF), Simon Mwakifwamba, aliyeniomba nihudhurie mkutano wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na Kamati-kazi za Filamu na Muziki unaofanyika kesho Ijumaa ndani ya ukumbi wa Baraza la sanaa la taifa (Basata), Ilala-Shariff Shamba, Dar es Salaam, mada ikiwa “mfumo wa usambazaji wa kazi za sanaa na burudani.”

Nadhani mawazo haya ya Kamati-kazi za Filamu na Muziki na ya wasomaji wangu katika jambo hili yamegongana hasa kwa kuzingatia umuhimu wa biashara hii ya filamu na muziki ambayo pia ndiyo chanzo cha ukombozi wa ajira kwa vijana.

Kilio cha kuibiwa kazi za sanaa kutoka kwa watayarishaji na wasanii kimekuwa kikisika kila mara ingawa kuna uwezekano mkubwa kwa wanaolia kutojua wanaibiwaje kazi zao kwa kuwa huwa wameshauza haki zao kwa msambazaji, hii inatokana na mfumo wetu wa usambazaji kuwa mbovu na wasanii kuvidharau vyama na mashirikisho ya sanaa wakisahau kuwa umoja ni nguvu.

Kuwa na mashirikisho ni jambo linalofanyika duniani kote. Hatuwezi kujikomboa kiuchumi bila kuungana, kinyume cha hapo tunaendelea kusikia vilio vya kuibiwa kazi huku wafanyabiashara wachache wakiendeleaa kulimiliki soko la filamu. Katika mashirikisho haya tunaweza kuelimishana ili kukabili ukosefu wa elimu ya sanaa kwa watengenezaji wa kazi za sanaa wanaolalamikiwa kutengeneza kazi za kiwango duni.

Hata suala la wasanii kutopata vipato stahili, licha ya kazi zao kusambaa sehemu nyingi ndani na nje ya nchi yetu hasa nchi za jirani. Yote hii ni kutokana na kuyadharau mashirikisho ambayo yangetuunganisha kutetea haki zetu za kimsingi za kiuchumi na kijamii. Kupambana kila mmoja kivyake hakuwezi kutusaidia, ndiyo maana sasa mashirikisho ya filamu na muziki yameamua kuja na mikakati mipya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini.

Mbali na jambo hili kuna ushauri pia ulitolewa ili kukabiriana na wimbi la wizi wa kazi za wasanii, ikiwemo usambazaji wa kazi za wasanii maeneo yote ya nchi kwa wakati mmoja mara zinapotoka (kama wafanyavyo Iran).

 Mkurugenzi Mkuu wa TRA, Harry Kitilya

Waziri wa Habari, Maendeleo ya Vijana, 
Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi

Inasemekana kuwa njia hii husaidia sana kupunguza wizi wa kazi za wasanii kwa kuwa mikanda ya picha za video, DVDs na ile ya mfumo wa sauti (CDs) hupatikana kwa wingi kila mahali na kwa bei nafuu ambayo hata mwananchi wa kipato cha chini anaweza kumudu kununua kazi hizo.

Mbinu nyingine ni ile ya kuwashirikisha viongozi mbalimbali wa dini ambao hutumia mahubiri na mawaidha yao kwenye nyumba za ibada kukemea watu wanaonunua kazi za wasanii zisizo halisi (original), na kushirikiana na jeshi la polisi, mahakama na watengenezaji wa kazi za wasanii (producers) kuhakikisha wanawakamata wezi wa kazi za wasanii na kuharibu kazi walizonazo pindi wanapowakamata pamoja na kuwatoza faini kubwa.

Ushauri huu ulitolewa na Naibu Waziri wa Filamu na Sanaa za Maigizo wa Iran, Javad Shamaqdar, wakati alipokuwa akizungumza na Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dkt. Emmanuel Nchimbi mjini Dodoma.

Sekta ya burudani nchini kwa sasa imeonekana kuvutia wengi kutokana na ukuaji wa kasi ambao umetokea katika tasnia hii. Katika kipindi hiki, kama hatutakuwa makini na mfumo wetu wa usambazaji na kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi yetu mara kwa mara, uzalishaji na thamani ya sanaa zetu kivitendo vinaweza kudorora zaidi.

Hata hivyo, sekta ya filamu nchini ndiyo imekuwa ikilengwa, ikipokea upinzani hasi kutokana na kukosekana kwa ubora wa kiufundi katika filamu zinazoandaliwa. Filamu pia zinakosolewa kwa kuelekeza nguvu nyingi kwenye mada za mapenzi na uchawi. Upatikanaji wa data za kuaminika juu ya sekta ya filamu nchini ni mdogo na hakuna utafiti kamili ambao unaeleza ongezeko la uzalishaji wa filamu katika taifa. Wala hakuna mwongozo unaofaa ambao tunaweza kuutumia kutathmini filamu zetu.

Hata hivyo, sekta za filamu na muziki zinasifika kwa kuzalisha maelfu ya ajira kila mwaka na zinaingiza mabilioni ya pesa huku serikali ikiambulia pato kiduchu. Ni wakati sasa umefika ambapo tunahitaji utashi wa kisiasa (political will) kutambua kuwa sekta za filamu na muziki nchini vinakuwa chanzo kikubwa mno katika kutuingizia pato la taifa na kuwa biashara yenye faida.

Lakini hadi sasa taasisi za fedha, hasa benki, hazitaki kuwekeza katika sekta hii, hususan filamu kwa sababu tu ya kukosekana kwa miundombinu rasmi. Kwa mfano hakuna data halisi ya makisio ya fedha zilizoandaliwa rasmi kuhusiana na sekta.

Kumekuwa hakuna mfumo rasmi wa usambazaji wa filamu nchini katika miaka ishirini iliyopita. Muundo uliopo katika sekta za filamu zilizoendelea ambapo biashara ya filamu huanzia kwenye box office (mfumo maalum unaoanzia kwenye uoneshaji sinema ndani ya majumba ya sinema) au mfumo wa sinema, baadaye hutolewa kwenye video, kurushwa kwenye vituo vya televisheni za kulipia, kisha katika televisheni za umma, na hatimaye kutolewa kama bidhaa rasmi (DVDs, VCDs, VHS) kwa matumizi ya nyumbani, mfumo ambao haupo nchini mwetu.

Uharamia limekuwa ni tatizo nchini ingawa si kwa kiwango kikubwa kama lilivyo kwa baadhi ya nchi, mfano Nigeria au Kenya. Chama cha Hatimiliki kimekuwa kikifanya jitihada mbalimbali katika kupambana na tatizo hili. Hata hivyo, watuhumiwa wakubwa wamekuwa hawaguswi na badala yake tunashuhudia wanaokamatwa ni wale wadogo wadogo.

Tunapaswa kuwa na chombo (mfano TRA) kitakachounda mfumo ambao hudhibiti aina na aina ya wasambazaji, kutoa miongozo kwa ajili ya usajili na leseni ya wasambazaji (ambayo ada fulani wanatarajiwa kulipwa), na kubainisha aina ya haki za usambazaji ambayo wasambazaji katika ngazi mbalimbali wataendelea kumiliki pamoja na udhibiti ili kuhakikisha kuwa haki hizi zinalindwa.

Chombo hiki (TRA) kiambatane na kuwepo kwa sera mpya itakayoonesha pia sifa zinazopaswa kuchukuliwa katika mkataba halali wa usambazaji ambao pamoja na mambo mengine, utalazimisha wahusika kuandikisha filamu zao kama miliki (intellectual property). Moja ya masuala ya ubunifu wa sera ya uzalishaji wa fedha na ulinzi ambayo nadhani sera inayopaswa kuwepo ni ya kutoa ufadhili kwa wamiliki wa haki za filamu.

Sera hii iende mbali zaidi ikizingatia mchakato wa utoaji wa filamu na uanzishwaji wa haki za usambazaji wa miliki. Katika mchakato huu, wasambazaji wenye leseni watatarajiwa kuwasilisha ripoti ya kila wiki ya kisheria katika shughuli zao za usambazaji ambayo inaweza kutumiwa katika kutathmini utendaji wa kifedha wa filamu. Chombo hiki kitakuwa ndiyo mamlaka pekee katika mchakato mzima isipokuwa pale itakapoelekeza kugawa kazi kwa mamlaka nyingine.

Katika mwanga wa ukuaji wa sekta ya filamu nchini na uwezo wake wa kiuchumi, pamoja na ubunifu katika sekta hii, sera hii itakuwa ya manufaa kwa kuona jinsi utekelezaji wa sera hii mpya. Naamini kabisa kuwa sera hii itafanikiwa katika kuanzisha mfumo ambao utaweka uwezo wa kiuchumi wa sekta hii.

Alamsiki...

No comments: