Jul 26, 2011

Monalisa, msanii pekee wa Afrika Mashariki anayeshiriki tuzo za Nigeria Enterteinment Awards

 Yvonne Cherryl (Monalisa)

"FILAMU za Tanzania zinapendwa sana nchi za nje, lakini katika utafiti wangu nimegundua hatuna wasambazaji ambao wanatusaidia kuzifikisha huko" ni maneno ya muigizaji mahiri katika tasnia ya filamu hapa nchini Yvonne Cherryl anayefahamika zaidi kama Monalisa.

Monalisa ambaye hivi sasa amechaguliwa kushiriki katika tuzo za NEA Awards (Nigeria Enterteinment Awards) zinazotarajiwa kufanyika nchini Marekani mwezi Septemba mwaka huu, anasema kuwa bado hakuna wasambazaji ambao wamejitolea kupeleka kazi za filamu nje ya nchi.


"Miezi miwili iliyopita nilikuwa nchini Ghana, na nilikwenda huko kwa nia ya kujifunza nini wenzetu wanafanya ili na sisi tuzidi kusonga mbele kwa kujifunza kutoka kwao, lakini baada ya kuwapa filamu kadhaa ikiwamo Binti Nusa na kuziona walizipenda sana, lakini tatizo huko hazifiki" anasema.

Anasema tatizo kubwa lililopo katika kazi za sanaa hapa nchini ni kukosekana kwa wasambazaji ambao wanakuwa na kazi ya kusambaza kazi hapa nchini na hata nje ya nchi na hilo ndio tatizo linalopelekea kukosekana kwa mapato ya kazi za sanaa.

"Wasambazaji wengi wamekuwa wakiishia kusambaza kazi ndani ya nchi pekee na wengi wameshindwa kujitanua na kutoka nje zaidi hilo ndio tatizo." Anabainisha kuwa kazi za filamu hapa nchini bado hazina viwango vya kutosha, lakini ni nzuri na zinazowavutia wengi.

"Wengi wanasema filamu za Bongo hazina kiwango ni kweli, kwani kuna mambo mengi kuanzia kwenye utungaji wa hadithi yenyewe na hata utengenezaji, lakini kazi zetu ni nzuri hii inatokana na nini wanasema wenzetu kuhusu kazi zetu," anasema Monalisa.

Hata hivyo amekiri kuwepo na mapungufu mengi katika sekta ya usambazaji ikiwa ni pamoja na kazi za nje hasa Nigeria ambazo nyingi zaidi zinakuwa ni feki ukilinganisha na zile ambazo ni orijino zinazotengenezwa na kuuzwa nchi nyingine.

"Mfano mzuri ni Ghana na Nigeria, nchi hizi wasanii wake wapo makini sana katika ufanisi wao wa kazi. Na hata katika usambazaji pia wanazingatia kufuatilia na hata kulinda kazi zao.

"Mfano hapa nchini kuna kazi nyingi sana hasa za filamu ambazo zinatoka Nigeria na Ghana na kuuzwa hapa nchini, wao wenyewe wanashangaa kwanini zinazouzwa hapa nyingi ni feki, wao wana wasambazaji wao Afrika Mashariki lakini hizi feki wanashangaa zinatengenezwa wapi?"

Anasema na kuongeza kuwa wingi huu wa kazi ambazo ni feki zinatokana na watu wasio waaminifu ambao wamegeuza wizi wa kazi za wasanii ni kama kazi yao na hivyo hawawezi kuacha.

Monalisa ameishauri serikali kuwa macho na kupiga kelele kwa waharibifu wa kazi za wasanii ili kuweza kuinua sanaa hapa nchini.

"Mfano mzuri ni pale Ubungo, mida ya usiku kuanzia saa moja, kuna watu wanafanya kazi ya kuuza CD za muziki na filamu za wasanii kwa bei chee ambayo si ile ya CD halali na ambazo ni zenye ubora, kwanini watu kama hawa wanaachiwa na kuendeleza biashara za magendo hadharani?" anahoji.

Kushirikishwa NEA Awards

Baada ya kushirikishwa katika tuzo za NEA, Monalisa anasema kuwa ni faraja kwake na kwa tasnia ya filamu hapa nchini.

"Monalisa wa zamani si yule wa sasa, nimesonga mbele tena sana namshkuru Mungu kwa hilo, lakini nawaomba Watanzania waniunge mkono kwa kunipigia kura katika tovuti hii: BOFYA HAPA katika kategori ya Pan Africa Actress of the Year, ili niweze kuibuka mshindi na kuiletea heshima Tanzania.

“Mungu akinipa afya na uhai, kamwe sitawaangusha mashabiki wangu na Watanzania kwa ujumla. Nimepania kuitangaza Tanzania kupitia filamu kwa kufanya kazi bora ambazo nashirikiana na wasanii wa nchi mbalimbali wa ndani na nje ya Afrika,” anasema.

Yvonne Cherryl, Monalisa ambaye anachuana na Akofa Aiedu, Ama. K. Abebrese, Nadia Buari, Yvonne Okoro na Jackie Appiah ni Mtanzania pekee na msanii wa Afrika Mashariki ambaye ameweza kushirikishwa katika tuzo hizo kupitia filamu ya Binti Nusa, filamu ambayo ilimpa tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Filamu nchini katika tuzo za Ziff zilizofanyika mwaka jana visiwani Zanzibar.

Wasifu wake

Monalisa alizaliwa Agosti 19 mwaka 1980 wilayani Temeke, Dar es Salaam. Ana watoto wawili, wa kike na wa kiume.

Monalisa amerithi kipaji cha uigizaji kutoka kwa mama yake mzazi, Susan Lewis anayefahamika zaidi kama Natasha. Monalisa alianza uigizaji tangu alipokuwa na umri wa miaka 8. Alianza kwa kukariri masomo ya biblia, kuimba na kuigiza.

Kati ya mwaka 1983 hadi 1985 alipata elimu ya awali katika shule ya watoto ya Alliance Francaise iliyopo katika Jiji la Luanda, Angola ambako alikuwa anaishi na babu yake aliyekuwa mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akifanya kazi katika ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Baadaye alirejea nchini na kujiunga na elimu ya msingi katika Shule ya Muungano, Temeke jijini Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 1994. Aliendelea na masomo ya sekondari katika shule ya Wasichana ya Zanaki iliyopo jijini Dar es Salaam na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1998 kisha akajiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Dar es Salaam kusomea Ukatibu Muhtasi kati ya mwaka 1999 na 2000.

SOURCE: Gazeti la Mwananchi

No comments: