Sep 14, 2016

Tutumie filamu na nyimbo kuhamasisha uzalendo

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu, Bi Joyce Fisso
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo . Nape Nnauye akipata maelezo juu ya utamaduni wa kucheza bao kwenye kituo cha Utamaduni wa kisukuma Bujora
TUNAELEKEA kutimiza miaka 55 tangu tuwe huru, lakini bado jamii ya Kitanzania imeendelea kupoteza maadili, mila na tamaduni zake kila kukicha. Baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana iliundwa mwaka 1962, rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alitamka wazi kuwa Utamaduni ndiyo kiini na roho ya Taifa, na nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.


Miaka takriban hamsini na tano ya uhuru tunazidi kushuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili huku sekta za sanaa na utamaduni zikionekana kutopewa kabisa kipaumbele na serikali, bila kujali kuwa sekta hizi zimesheheni utajiri mkubwa ambao ungeliingizia taifa hili mapato, ingawa tuna wizara inayohusika sanaa na utamaduni.

Nikashangaa sana kuona badala serikali ikielekeza nguvu kubwa sana katika kutafuta kile kilichoitwa vazi la taifa (ambacho kimsingi walikuwa wanatafuta kitambaa cha taifa) utadhani ndiyo suluhisho na mmomonyoko huu wa maadili na kupotea kwa tamaduni zetu!

Kwa sasa ingalau inatia moyo, hasa baada ya serikali (kupitia wizara na idara zake) kuanzisha mchakato wa kuwepo kwa sera tatu: ya utamaduni (kusimamia utamaduni), ya filamu (kusimamia filamu) na ya sanaa (kusimamia muziki, sanaa za ufundi na za maonesho), ili kuleta tija katika sekta hizi.

Hapo kabla tulikuwa tukiaminishwa kuwa sera ya utamaduni pekee ilitosha kuwa muarobaini wa matatizo yaliyomo kwenye sekta. Sera ya Utamaduni iliyopo sasa ilizinduliwa mnamo Agosti 23, 1997 mjini Dodoma, ikiwa ni hatua ya pili muhimu baada ya ile ya kwanza ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962.

Huku wizara inayosimamia utamaduni ikiwepo, hatukuwa tukiona mipango yoyote ya kimaendeleo ambayo ilikuwa inabuniwa au kutekelezwa ili kujenga moyo wa uzalendo kwa jamii. Utamaduni umekuwa haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inadhaniwa kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.

Serikali kutoipa umuhimu sekta ya sanaa/utamaduni ilileta madhara makubwa katika taifa ambayo kila mtu ameyashuhudia; ndiyo sababu ya uchafu na tatizo la maadili katika filamu na nyimbo zetu lilikuwa kubwa, kwani kulikosekana kabisa udhibiti wa kazi chafu.

Kilichoshangaza zaidi ni wizara kujiingiza katika mchakato wa kutafuta vazi ambalo waliamini kuwa ndilo lingekuwa suluhisho la maendeleo ya nchi na uzalendo kwa vijana! Niliwahi kuandika nikionya kuwa kama wizara inaamini hivyo ilikuwa inafanya kosa kubwa sana, kwani kulikuwa na malalamiko mengi ya kukosekana kwa maadili katika filamu na nyimbo zetu lakini haijawahi kufikiria kuunda kamati!

Hebu tujiulize; kwanini tunakosa alama ya mfano wa filamu zetu? Hivi tutaendelea kujidanganya hadi lini kuwa alama ya filamu zetu ni Kiswahili kinachozungumzwa wakati lugha hii inazungumzwa pia katika nchi zingine kama Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo, Uganda na kwingineko? Na bahati mbaya sana ni kwamba ikajengeka kasumba ya kutumia majina ya Kizungu kwenye filamu zetu!

Kwa nyakati tofauti pia nimewahi kuwasikia viongozi wa serikali wakilalamikia kuhusu maadili katika filamu hizi. Kila kukicha ni filamu za mapenzi peke yake zinazotawala kwenye soko letu au hadithi zisizo na asili yetu tulizonakili kwa wenzetu zenye vitendo na maudhui ya jamii za nje. Wizara haikuwahi kufikiria kutafuta tiba ya kuunda kamati (kama ilivyofanya kwenye kinachoitwa vazi) ili watayarishaji wa filamu na wasanii na watayarishaji wabanwe kutumia visa vyetu wenyewe na aina ya mavazi yetu. Vipi tuachwer kuendelea kuiga kutoka kwa wenzetu?

Kwa kweli haya ni maswali muhimu na inabidi kila mdau aliye kwenye sekta ya filamu na sanaa kwa ujumla anapaswa ajiulize. Hadi sasa tumekwisha pita njia potofu na kukipoteza kizazi chetu, maana njia tunayoenda nayo sasa katika filamu zetu ni ile iliyojengwa juu ya msingi wa wimbi la utandawazi inayoakisi utamaduni wa Kimagharibi.

Tukubali au tusikubali, ukweli ni kwamba sekta ya filamu imechangia kwa kiwango kikubwa hatari ya kuporomosha mfumo mzima wa maadili katika jamii zetu, kwani watayarishaji na wasanii walio wengi katika sekta hii wameshapotea njia kwa kutofuata au kutoijua miiko na maadili katika hadithi wanazoandaa, mitindo na maudhui ya hadithi yanaonekana dhahiri kupotosha kulingana na asili yetu, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.

Naishauri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo (nikiamini Waziri Nape Nnauye ni msikivu na anayeitakia mema sekta hii) kufikiria kuwa na kamati ya kuhakikisha maadili kwenye filamu na muziki yanazingatiwa na kuhimiza uvaaji wa mavazi ya aina fulani, na kubatilisha kabisa ule mchakato uliotumia nguvu kubwa kutafuta vazi linaloitwa la Taifa, ambalo hata sijui limeishia wapi!

Kwanini tusiwatumie wasanii wetu kuvaa mavazi tunayoyataka ili kuzitambulisha jamii zetu? Ni kama ilivyo kwa nchi za Ghana, Nigeria, Afrika Kusini, ambazo hazijawahi kuwa na kamati ya kutafuta mavazi bali tumeyajua mavazi yao kwa sababu yamekuwa yanatumiwa sana na wasanii wao, kiasi cha kuonekana ni mavazi ya taifa, hata hivyo si kweli kwamba ni mavazi ya taifa, hayo ni mavazi yanayovaliwa na makabila makubwa katika nchi hizo.

Nina imani na Waziri Nape Nnauye, maana pamoja na kuhubiriwa kuhusu maadili na utamaduni lakini serikali haikuwa ikiizingatia sekta hii na hivyo kukosa udhibiti wa sanaa huku ikiwaacha wasanii wajifanyie wanachodhani kinawafaa, jambo lililokuwa linaashiria hatari kubwa ya mporomoka wa kutisha, si kwa fani husika bali kwa jamii nzima ya Tanzania.

Nitashangaa kama Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, itataka kulazimisha/ kuendeleza mchakato wa watu kuvaa hilo vazi lililokuwa linalotafutwa, na kushindwa kuangalia mambo kwa upana wake!

Ninachoamini ni kuwa sanaa ya filamu ni zao la matokeo ya juhudi za mtayarishaji na watendaji wengine katika kazi ya filamu na wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu na hii kama tanzu muhimu ya utamaduni si kitu kilichoibuka tu.

Hivyo jambo muhimu na la msingi hapa ni kwa Serikali na wadau wote kuzingatia, kuzitambua na kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria. Sanaa ya filamu ni kazi ya ubunifu yenye ufundi na mvuto, inapaswa kutopoteza ubunifu, uasili na kukosa mbinu bora ya uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.

Wizara ijaribu kuangalia sana suala la mzalishaji wa filamu anayeumiza kichwa kutafuta mtaji na kuandaa bajeti ya filamu - uandaaji hadi kukamilika - lakini bado hana sauti wala nguvu sokoni, hili ndilo linalochochea mmomonyoko huu wa maadili, kwa kuwa mtayarishaji anatengeneza filamu kwa matakwa ya msambazaji, ambaye yeye anaangalia soko tu.

Mtayarishaji wa filamu nchini huwa anafanya kazi kwa shinikizo la woga wa soko! Hana uhakika wa soko lake na endapo atakuwa jeuri basi kuna hatari ya filamu yake kutosambazwa, hivyo kinachobaki kwake ni kuweka mikono nyuma awapo mbele ya msambazaji ili filamu yake isambazwe!

Kwa hali hii maadili yanazidi kupotea kwa kuwa mnunuzi wa mwisho bado hujikuta anafuata mkumbo wa nguvu ya msambazaji bila kujali ubora wa filamu, kuanzia kwa mwandishi wa filamu, muigizaji, muongozaji, mazingira na taaluma ya filamu yote! Ananunua filamu kwa mazoea ya majina na hadithi!

Hadi sasa filamu nyingi za Tanzania au michezo ya kuigiza katika runinga ni vitu vilivyopoteza mwelekeo kwani leo hii inafuata mifumo na mtiririko wa kigeni zaidi kama filamu za Nigeria, Ufilipino na kwingineko. Yote hii inasababishwa na wavamizi kwenye fani hii waliodhani kuwa mtu akikosa kazi ya kufanya basi kimbilio lake ni kwenye sanaa hasa filamu. Hapa ndipo wizara ingeunda kamati ya kushughulikia mambo haya kwa kuwa athari zake ni kubwa kuliko kukosa vazi linaloitwa la taifa.

Matokeo yake tumejikuta tukiwa na idadi kubwa ya watayarishaji filamu, waandishi wa filamu, waongozaji filamu na waigizaji bandia wasio na misingi wala kanuni za fani husika, jambo lililosababisha filamu za Tanzania kuwa sawa na Big G inayoisha utamu muda mfupi baada ya kutafunwa, huku watu wenye taaluma na misingi wakitupwa nje ya soko kwa kuwa sanaa siku hizi imekuwa ni biashara isiyozingatia na kufuata maadili ya Taifa.


Alamsiki…

No comments: