Sep 28, 2016

MAFUNZO KWA WAANDISHI: Pongezi kwa Bodi ya Filamu Tanzania

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Waandishi wa Filamu kwa baadhi ya waandishi hao Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

MWANDISHI mzuri wa filamu ni lazima awe na kipaji na uwezo mzuri wa kuandika. Kipaji mtu huzaliwa nacho au hukipata (adapt) katika umri mdogo kutokana na mazingira anayokulia. Uandishi mzuri wa filamu huanzia katika kuwa na uwezo wa kuumba maneno ambayo yatakuwa rahisi kueleweka pindi mtu akiyasikia.

Wakati unaandika ni muhimu sana kuzama ndani ya akili za walengwa wako ujue wanataka nini.


Mwandishi mzuri wa filamu ni yule anayefahamu ni maudhui gani yanayofaa katika kizazi cha leo yanayokwenda sambamba na watazamaji ndani ya akili zao na kuihusisha jamii moja kwa moja kwenye hadithi yake. Mafanikio yanayotokana na maudhui yanategemea sana mmenyuko wa watazamaji, na kujenga maudhui yaliyo kwenye mstari na mwelekeo wa watazamaji na matarajio yao.

Inahitajika kwa waandishi wa filamu kujihusisha moja kwa moja na mtazamo wa watazamaji katika mazingira waliyomo. Kwa matokeo haya, utafiti na uelewa wa kile wanachokiandikia ni suala la kupewa umuhimu mkubwa kabla ya kuandaa kazi husika.

Bila uelewa mzuri wa maudhui ni sawa na kufunga safari kwenda sehemu bila kufikiria jinsi ya kufika huko. Kumbuka, unachokiandika si kwa ajili yako, ni kwa ajili ya watazamaji na hadithi zao! Kama mwandishi wa filamu, usipende kuingiza kila taarifa ukasahau kuwa unaandika kwa ajili ya jicho (kuonekana) na sikio (kusikika).

Katika filamu zetu kumekuwepo malalamiko mengi kuhusu hadithi zinazotumika katika filamu zetu na aina ya uandishi wa filamu. Mara nyingi hadithi zimeonekana kujirudia au kufanana kutoka sinema moja hadi nyingine, na hata umaliziaji wake kutowafurahisha watazamaji.

Wengi wa wanaojiita waandishi wa filamu nchini wanasahau kuwa script ndiyo hatua ya mwanzo kabisa katika filamu, ni ramani ya kutuongoza kutoka kwenye wazo hadi pale filamu inapokamilika. Mwandishi wa filamu ndiye mtu wa kwanza anayeiona sinema wakati akiandika, muongozaji huja kuiona baadaye pale anapopitia script ili kuongoza upigaji picha za filamu.

Kwa hali hiyo, uandishi wa filamu ni kazi ngumu sana inayohitaji weledi wa hali ya juu. Mwandishi ndiye mtu wa kwanza anayeiona sinema, analiona kila tukio la sinema ndani ya akili yake pale anapoandika. Mwandishi anatakiwa kujua jinsi sinema inavyotakiwa kuonekana, na hata sauti (sound tracks) zinazofaa kutumika kwenye sinema yako. Ujuzi wa aina hii huitwa “visualization.”

Kwa kutambua uzito wa taaluma hii ya uandishi wa filamu, hivi karibuni Bodi ya Filamu Tanzania iliandaa na kuratibu mafunzo ya siku nne ya uandishi wa filamu kwa ushirikiano na Chama cha Waandishi wa Filamu Tanzania (TASA). Bodi ya Filamu Tanzania inaamini kabisa kuwa kwa kuandaa mafunzo hayo itasaidia sana katika kuleta mabadiliko chanya kwenye ubora wa filamu za ndani.

Pia imeahidi kutoa ushirikiano kwa wadau wakati wowote itakapohitajika ili kuboresha sekta ya filamu nchini. Na ili kutekeleza kwa vitendo ahadi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo, alikubali kuwalipia ada ya uanchama washiriki wanane ambao walikuwa bado hawajajisajili kwenye Chama cha Waandishi wa Filamu Tanzania.

Mafunzo hayo ya siku nne yalikuwa ni ya vitendo na shirikishi ambapo yaliongozwa na wakufunzi wawili kutoka nchini Marekani na yalikuwa na lengo la kuwaongezea ujuzi waandishi wa filamu nchini wapatao 65, ili waweze kuandika script zenye ubora wa kimataifa.

Takwimu za Bodi ya Filamu Tanzania zinaonesha kuwa jumla ya script 33 ziliwasilishwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, kati ya jumla ya filamu zaidi ya 1400 zilizokaguliwa kwa mwaka huo. Idadi hiyo ya script ni ndogo ukilinganisha na maombi 169 yaliyowasilishwa ndani ya mwaka huohuo kutoka kampuni za nje ambapo maombi yote sawa na asilimia 100 yaliambatanishwa na script zake.

Kwa hatua hii, nawapongeza sana Bodi ya Taifa ya Filamu kwa kuliona tatizo la hadithi zetu na waandishi, kwani bila script hakuna filamu. Pia nawapongeza kwa ahadi yao ya kuendeleza ushirikiano na wadau wa sekta ya filamu kuhakikisha sekta hiyo inakuwa chachu ya maendeleo nchini.

Ahadi iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo wakati akifungua mafunzo hayo kwenye ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dar-es-salaam.

Siku zote nimekuwa nikisisitiza kuwa wadau wachangamkie semina, warsha na mafunzo mbalimbali yanayojitokeza kwani husaidia sana kuleta mafanikio japo kwa kiasi fulani, kwani bila hivyo, inawezekana kwa maendeleo yanayokuja Tanzania, vyanzo vya maendeleo vitakosa kazi za sanaa.

Kutokana na kukosa mafunzo ya taaluma ya filamu waandishi wa filamu Tanzania wamekuwa ni watu wanaoandika kwa kulipua kazi, wasiojali ubora, wanaoshindwa kubuni na kujikuta wakiishia kunakiri hadithi za nje na hata kazi zao nyingi hazizingati mambo muhimu kwa kisingizio cha bajeti hata kwa yale ambayo hayahitaji kuwa na bajeti kubwa.

Pia waandishi wengi wamekuwa hawana uthubutu kwa sababu wamejawa na woga, jambo ambalo limekuwa linarudisha nyuma maendeleo ya sekta ya filamu. Kwa hatua hii ya Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Filamu Tanzania, wamevunja mwiko wa wasanii wa Tanzania kukwepa kuhudhuria makongamano, warsha na semina mbalimbali za filamu kwa hofu tu ya kutokujiamini.

Bodi ya Filamu Tanzania imeliona hili ambalo ni moja ya mapengo makubwa kwa sekta ya filamu ya nchi yetu, lililosababishwa na kukosa mfumo mzuri ambao ungesaidia kumuendeleza msanii wa Tanzania, hasa kutokuwepo kwa vyuo vinavyotoa mafunzo ya filamu katika ngazi mbalimbali hata kwa wale wasio na sifa za kwenda Chuo Kikuu, kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya au Afrika Kusini, maana kuendelea kukaa tukitegemea tu elimu ya darasani kuwa ndiyo suluhisho pekee katika kupata mafunzo ya weledi ni kujidanganya.

Kuna njia nyingi za kupata elimu kama hizi zinazojitokeza ambazo hutolewa kwa njia ya semina, warsha au makongamano ambazo zinaweza kuwa suluhisho japo kwa kiwango fulani na kuwafanya wasanii kufanikisha maendeleo ya sekta ya filamu nchini na kuitangaza Tanzania ipasavyo nje ya mipaka yake.

Binafsi, japo nimepata elimu ya darasani, lakini niseme wazi kuwa ni kwa kupitia makongamano, warsha na semina nimeweza kupata ufahamu mkubwa zaidi kuhusu filamu na namna ya kuandaa kazi, kitu ambacho kimekuwa kikinifanya kujiamini.

Nina imani mafunzo haya yaliyoandaliwa na Bodi ya Filamu Tanzania yatawasaidia waandishi wa filamu kufanya kazi kwa kujiamini badala ya shinikizo la woga wa soko na kutojiamini, kwa sababu tu walikuwa wamekosa kabisa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya kuandika kazi zao katika kiwango kinachokubalika!

Wengi wamekuwa hawana uhakika wa kazi zao! Kilichobaki ni wao kutegemea fadhila ya waandaaji na kulipwa ujira mdogo usioendeana na ugumu wa kazi zao, jambo lililokuwa likiwaweka katika daraja la chini kabisa. Faida kubwa ya kupata mafunzo ya taaluma ya filamu ni pamoja na kumfanya mwandishi ajitambue na aijue thamani ya kazi yake.


Alamsiki.

2 comments:

Unknown said...

Takwimu za Bodi ya Filamu Tanzania zinaonesha kuwa jumla ya script 33 ziliwasilishwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, kati ya jumla ya filamu zaidi ya 1400 zilizokaguliwa kwa mwaka huo. Idadi hiyo ya script ni ndogo ukilinganisha na maombi 169 yaliyowasilishwa ndani ya mwaka huohuo kutoka kampuni za nje ambapo maombi yote sawa na asilimia 100 yaliambatanishwa na script zake.


hapa ulimaanisha nini?

Unknown said...

naomba haya mambo, yatangazwe kwenye ma Television, na maredio. maana yanapita wengi.