Aug 31, 2016

Bongo Movies: Bado tuna tatizo kubwa katika uandishi wa filamu

Mwandishi wa makala haya, Bishop Hiluka, katika moja ya kazi za uandishi wa filamu

FILAMU ni chombo muhimu sana cha mawasiliano katika jamii na ustawi wa nchi yoyote, huchangia kupatikana kwa ajira kwa vijana, huchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, husaidia kuwaambia watu wengine kuhusu hadithi za jamii husika, huchangia maendeleo ya nchi na kadhalika.

Utengenezaji wa filamu si suala la mzaha, si jambo la mtu ambaye jana usiku alilala akiwa hana kazi ya kufanya na leo asubuhi kaamka akiwa na wazo la kutengeneza filamu, bila kuwa na ujuzi, nyenzo wala mtaji wa kutosha. Utengenezaji filamu ni jambo linalohitaji gharama, ni jambo la hatari (venture) linalohitaji muda mwingi na mtengenezaji wa filamu hatakiwi kuwa mvivu wa kufikiri au kupoteza muda akipiga soga na rafiki zake au kufanya mizaha.


Katika filamu zetu (ambazo zimekuwa zikijulikana kama Bongo Movie) kumekuwepo malalamiko mengi kuhusu hadithi zinazotumika katika filamu zetu na aina ya uandishi wa filaamu. Mara nyingi hadithi zimeonekana kujirudia au kufanana kutoka sinema moja hadi nyingine, na hata umaliziaji wake kutowafurahisha watazamaji.

Nakubaliana na malalamiko kutoka kwa watazamaji wa filamu za Tanzania, ni kweli tunalo tatizo kubwa sana kwenye hadithi katika sinema zetu, hasa kwa kuwa kila mtu anadhani anaweza kuandika, badala ya kuwaachia wenye taaluma hiyo ya uandishi watuandikie.

Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa script ni hatua ya mwanzo kabisa katika filamu, ni ramani ya kukuongoza kutoka kwenye wazo (concept) hadi pale filamu inapokamilika (final edit). Mwandishi wa filamu (scriptwriter) ndiye mtu wa kwanza anayeiona sinema wakati akiandika, muongozaji huiona pale anapopitia script ili kuongoza upigaji picha (shooting).

Uandishi wa filamu ni kazi ngumu sana inayohitaji weledi wa hali ya juu, ni sanaa ambayo kwanza huanzia kwenye kipaji, kisha mafunzo hufuatia. Kama mwandishi, wewe ndiye mtu wa kwanza unayeiona sinema, unaliona kila tukio la sinema ndani ya akili yako pale unapoandika. Kama mwandishi unatakiwa kujua jinsi sinema inavyotakiwa kuonekana, na hata sauti (sound tracks) zinazofaa kutumika kwenye sinema yako. Ujuzi wa aina hii huitwa “visualization.”

Visualization ni moja kati ya mbinu muhimu sana katika uandishi wa filamu, huu ni uwezo wa kuiona picha kupitia maandishi, ni ujuzi unaochukua muda kuwa nao hasa ukishaifanya kazi ya uandishi kuwa sehemu ya maisha yako. Pia kuna suala la kuandika mazungumzo (dialogue) ya wahusika, ambalo ni ujuzi wa ziada.

Katika uandishi wa filamu, kuna mambo matano muhimu sana unayohitaji kuyajua ili kuandika filamu yenye kisa/hadithi nzuri (nitakapopata nafasi nitayafafanua zaidi siku zijazo).

Watu wengi huwa hawaielewi nafasi ya waandishi wa filamu. Hudhani kuwa nafasi pekee ya mwandishi wa filamu ni kuandika mazungumzo kati ya wahusika. Hata hivyo, dhamira kuu ya makala haya ni kujaribu kuangazia kile ambacho mwandishi wa filamu hukifanya.

Waandishi wa filamu kwanza huhitaji kuyaandaa mawazo yao na kuandaa dhamira ya jumla ya mawazo yao. Halafu huhitaji kuyabeba mawazo hayo kwenye taswira halisi ya wapi eneo la tukio litatokea na kisha kufanyia kazi vipengele vya taswira hizo katika kile kinachoitwa mwongozo/muswada andishi wa filamu (screenplay).

Uandishi wa filamu ni mchakato wa kuandika mambo ambayo yatatazamika na kusikika, wakati anayefanya kazi ya kuyatengeneza mambo haya ili yatazamike na kusikika ni muongozaji wa filamu akishirikiana na mtaalam wa picha na mwanga.

Wakati mwandishi wa filamu anaandaa mazungumzo kati ya wahusika, mazungumzo haya huwa ni zaidi ya maongezi ya kawaida. Mazungumzo haya huisaidia hadithi kusonga mbele, huwatengeneza wahusika kwa undani zaidi na kuwafanya watazamaji kujikuta wakichangia hisia na mhusika.

Kwa kufupisha hadithi, kama hakuna mwandishi wa filamu, basi hakuna filamu. Ndiyo maana mara nyingi kumekuwepo na aina fulani ya wivu kwa waandishi wa filamu kwenye sekta ya filamu. Waandishi wa filamu ndiyo watu wenye wazo la hadithi, wazo ambalo ndiyo ramani ambayo filamu itajengwa kwa kuitumia, waandishi ndiyo watu wanaotoa ajira kiaina kwa mtayarishaji wa filamu, muongozaji na waigizaji wa filamu.

Mara nyingi waandishi wa filamu ndiyo watu wa kwanza kuiona filamu kwani huwa tayari wana maono/taswira ya jinsi sinema itakavyoonekana kwenye televisheni, na kwamba hufanya kazi kwa ukaribu na waongozaji ili kupata michoro maalum (story board) itakayosaidia katika uongozaji ambayo ndiyo huitoa script kwenye karatasi na kuileta kwenye televisheni.

Imekuwa ikisemwa, kwa sababu mwandishi mara nyingi huwa yuko bayana, mwenye kutaka tafsiri iliyonyooka na asiyetaka kupindisha mambo, ndiyo maana mara nyingi amekuwa akiwekwa kando wakati wa upigaji picha za sinema. Muongozaji wa filamu huwa hapendi kabisa kuelekezwa/kutafsiriwa jinsi ya kuongoza wakati wa upigaji picha za sinema, na hata waigizaji huwa hawapendi kujua kuhusu tafsiri ya maandishi ya mwandishi wa filamu kwa kuwa wanadhani yatawanyika kufanya vitu vingine huru vya ziada (free style).

Watu watataka kuona kunakuwa na uhuru wa kiubunifu wa kuitafsiri script iliyowasilishwa na mwandishi wanavyoona inafaa badala ya kuelekezwa jinsi ya kuitafsiri. Matokeo yake huitafsiri visivyo kabisa, ambavyo mwandishi wa filamu alivyokusudia, wakati mwingine kundi la waigizaji, waongozaji na watayarishaji huweza kuitafsiri script katika namna ambayo mwandishi alikusudia.

Vilevile filamu nzuri inaweza kutengenezwa kutokana na muongozaji kuitafsiri script visivyo. Hakuna njia sahihi ya namna ya kuitafsiri script. Mara nyingi wakati wa upigaji picha za sinema jicho la mwandishi hufanywa kuwa “chaguo la pili” baada ya jicho la muongozaji.

Ndiyo maana husemwa kuwa filamu “haiandikwi ikakamilika”; badala yake “huandikwa tena na tena hadi siku ya upigaji picha”. Hii maana yake ni kwamba ukishakabidhi rasimu (draft) yako ya script kwa wakala, atarudi kwako akiwa na mapendekezo mengine ambayo huleta mabadiliko, kisha ukiipeleka kwa mtayarishaji, naye atakuja na mapendekezo yake mengine yatakayotakiwa kuingizwa kwenye script hiyo.

Baadaye muongozaji atabadili baadhi ya matukio kwa kadri atakavyoona inafaa ili kumrahisishia katika uongozaji wakati wa upigaji picha, na hata waigizaji watataka kubadilisha baadhi ya mistari ili iendane na mtindo waliouzoea. Kama mwandishi wa filamu, kuiona script yako ikibadilishwa tena na tena inaweza kukuudhi kidogo.

Kila neno uliloandika kwenye filamu uliliweka kwa sababu maalum lakini sasa hawa watu wanataka mabadiliko kiasi cha kubadili kabisa mtazamo wako wa awali. Hata hivyo, kama mwandishi pia unataka kujaribu na kuhakikisha kuwa lengo lako linabakia bila kubadilika hata baada ya maboresho yote hayo.

Unaweza kufanya hivi kwa kuandaa nyaraka rahisi ambazo zitaelezea madhumuni makuu ya hadithi yako. Unatakiwa kuandaa nyaraka maalum kama “Synopsis”, “Pitch”, “Treatment” na “Outline” kabla hujaanza kuandika script yako ili kwamba kila mmoja atapaswa kurejea kwenye nyaraka hizi ili kuhakikisha kuwa script yako haibadiliki na kuharibu maana au lengo lililowekwa.


Alamsiki.

No comments: