Jul 29, 2016

Waziri Nape Nnauye; Angalia pia upande wa pili wa shilingi

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, akiwa katika Operesheni ya kuwasaka waharamia wanaodurufu kazi za wasanii
SERIKALI ya Awamu ya Tano imeanza kuonesha juhudi katika kuisaidia sekta ya sanaa nchini baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuingia mtaani na kukamata DVDs zisizo na stika ya TRA zinazoingia nchini kinyume na sheria pamoja na zile zinazokwepa kulipa kodi ili kuinua uchumi wa nchi na wasanii.

Waziri Nape Nnauye ameahidi kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu nchi nzima akisisitiza kuwa hatua hii ni ya mwanzo kwa kuwaonesha kuwa agizo la Rais John Pombe Magufuli, la kulipa kodi na kununua bidhaa halisi kwa kutoa risiti linasimamiwa ipasavyo.


Aidha Waziri Nnauye aliongeza kuwa wauzaji wengi wa bidhaa feki za filamu wamekiuka sheria zinazosimamiwa na Sekta ya Filamu na muziki, ikiwemo sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya Na. 4 ya mwaka 1976 inayosimamiwa na Bodi ya Filamu Tanzania, sheria ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Na. 23 ya mwaka 1984, Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999 inayosimamiwa na Chama cha Hakimiliki na hakishirikiya (COSOTA), pamoja na sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147 chini ya kanuni za stampu kwa bidhaa za Filamu na Muziki ya mwaka 2013 inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Zoezi hili limelenga kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi na wasanii ambao umekuwa unahujumiwa sana kwa kuwepo bidhaa feki za filamu zinazoingizwa nchini na kuuzwa kwa bei nafuu na kuua soko la bidhaa za ndani na kuingiza tamaduni zisizofaa katika jamii yetu unaimarika.

Naungana na Waziri Nnauye katika zoezi hili na namtakia Baraka na mafanikio, lakini namkumbusha kuwa serikali yake inapaswa kwenda mbali zaidi ya hili, vinginevyo hatutaona tija katika juhudi hizi za serikali. Serikali itafute njia ya kuwafanya wasanii kuachana na ile dhana iliyojengeka kwamba Sanaa ni kipaji. Sikatai, kwamba si kipaji, lakini Sanaa ni taaluma pia. Kwa maana kuwa Sanaa inasomewa!

Ni vigumu kwa fani yoyote ile kubakia katika kundi lisilokuwa na vigezo vya upimaji wa ubora. Kusipokuwepo vigezo vya kupima utaalamu wa fani hii, sinema zetu zitaendelea kuwa duni, zisizothaminika na hata kubakia kuwa sekta isiyo rasmi (japo tunaaminishwa kuwa imerasimishwa) ambayo haiwezi kuchangia katika maendeleo ya taifa kwa uwezo mkubwa kama inavyotakiwa.

Sekta ya filamu hasa ya Tanzania imekuwa ni kati ya sekta zisizo na vigezo vya kupima utaalamu na ubora. Ndiyo maana haishangazi kuona makampuni mbalimbali na hata watu binafsi wakikazania kuibua vipaji vya vijana bila kukazania kusomesha vipaji vya vyao. Kila mtu akijisikia anajitangaza msanii! Tena anatengeneza pesa nyingi kuliko wasanii waliokwenda shule.

Ni wakati sasa Serikali pia ilikazie jambo hili ili Sanaa ya Tanzania iwe ni taaluma na si kitu kinachofanana na taaluma, ili iweze kufikia mafanikio kama ambayo sekta nyingine zimeyapata, kwani ukichunguza utagundua kuwa wamepitia mabadiliko mbalimbali ambayo yanawawezesha kuthaminika na kutambulika kitaifa na kimataifa.

Serikali iangalie namna bora ya kuhakikisha wasanii wanapata elimu (japo kwa kuwaandalia warsha na makongamano mbalimbali kwa wale wasio na vigezo vya kuingia vyuo). Pia serikali inapaswa kuongeza idadi ya vyuo kwani kwa sasa tuna taasisi kuu tatu tu zinazotoa mafunzo ya sanaa ya maigizo kwa ngazi ya cheti, stashahada na shahada. Taasisi hizo ni; Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TaSUBa), Chuo Kikuu cha D’Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Chuo cha Ualimu Butimba kimesitisha kozi ya masomo ya sanaa. Tokea mwaka 1975 UDSM walifundisha sanaa, wakati Bagamoyo walianza mwaka 1981 na UDOM, chuo kipya walianza mwaka 2008, na walianza vizuri sana.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na maswali hasa toka kwa Watanzania bila kupatiwa majibu juu ya sekta ya filamu. Wasanii “masupastaa” katika sekta ya filamu ni watu ambao watu hujiuliza kama taaluma hiyo wameisomea au ni kwa jinsi gani ilitokea wao wakawa ndiyo watu wanaoshughulika nayo. Maswali haya ymekuja baada ya kazi wanazozalisha kuzua maswali mengi juu ya uwezo au kipaji cha waigizaji, pia aina ya migogoro inayowasilishwa katika hadithi zao.

Sanaa (ikiwemo filamu) kutokuwa taaluma kunawafanya wafanyabiashara kuwatumia wale wanaojiita “wasanii” kujipatia fedha kwa kuuza kazi zao. Na kwa sababu wasanii ni kundi linalofikiri kuwa hawathaminiki, ni wazi wameweza kutokujithaminisha kwa kujikomba kuambatanishwa na fani nyingine kama maendeleo, sayansi n.k bila kutambua kuwa sanaa kama sanaa ni maendeleo, sayansi nk.

Lakini pia inashangaza kuona hata wasomi katika fani hii wamekuwa wakiimbia sekta ya sanaa na kwenda kufanya kazi zingine na kuliacha soko la filamu kwa wasanii wasio na taaluma wala weledi. Waigizaji wa “bongo muvi” ni vigumu kuwachambua na kuwaelewa kwa misingi ya taaluma ya uigizaji kwani wanapingana na mengi sana katika fani hiyo! Ukiacha kazi mbalimbali ambazo zipo sokoni na pia zinaweza kupendwa sana na wananchi (japo zinaweza zisiwe ubora kitaaluma).

Wasomi hawa ama hawajiamini au aina ya mafunzo wanayopata katika taasisi husika yanawafanya kuwa wakosoaji wazuri kuliko kuwa wabunifu wazuri! Lakini pia inawezekana wameandaliwa kufanya kazi zao kwa utaalamu na kuzingatia kanuni lakini kwa kuwa serikali imeshindwa kuweka misingi mizuri ya soko yenye kuzingatia weledi, wamejikuta wakishndwa.

Naishauri Serikali ikijite katika kuhakikisha wasanii wanapata taaluma kwani hakuna taaluma isiyo na muongozo, mipaka, miiko na maadili katika utendaji. Hata sanaa ni moja ya taaluma. Tusifikiri kwamba, kwa vile ni saana, kila mmoja anaweza kuwa sawa – aliyesomea na mwenye kipaji cha kuzaliwa. Lazima tutofautishe vitu hivi.

Tukubali au tusikubali, pamoja na juhudi za waziri lakini ukweli ni kwamba sekta hii inaelekea mochwari kwani ubunifu unaenda ukishuka kila kukicha. Kutokubali uwepo wa wataalamu wa sanaa ndiyo kumesababisha dharau katika sanaa. Kutothamini umuhimu wa ngazi za viwango ndiyo unaoleta picha kuwa sanaa ni kazi ya kila mtu.

Suala hili kuliacha kwa wasanii na vyama vyao pekee hakuwezi kutusaidia, kwani, vyama hivi badala ya kuwa nguzo ya kufungua mijadala ya kuleta maendeleo endelevu huku vikifuata na kusimamamia sheria za nchi na hata kudai mabadiliko pale inapobidi, vimebakia kuwa mwanzo wa makundi ya chuki, fitina, ugomvi, chuki n.k.

Ikumbukwe kuwa maigizo na filamu ni sanaa za kigeni toka ulaya na huja na kanuni zake. Taaluma ya sanaa ya uigizaji ni pana sana, siyo rahisi kama wengi wanavyoichukulia kwa ‘uzoefu’ wa kuangalia yanayooneshwa na wasanii wetu katika luninga zetu!

Najua kuna sehemu tulijikwaa tangu mwanzo, maana televisheni zetu zilipoanza kuonesha maigizo na filamu za wasanii wa Kitanzania zilianza kwa kuwalipa wasanii nafasi ya kupata umaarufu, siyo malipo ya pesa baada ya kufanya kazi. Tunaweza kuania hapo.

Hili ni uthibitisho tosha wa wasanii kutoichukulia fani hii kama taaluma, na hata hali duni za wasanii wa maigizo wengi wa TV ‘waliostaafu’ au kufa masikini lakini wakiwa na majina makubwa kuliko wao wenyewe walivyo.

Kwa kawaida sanaa huwa inakusudiwa kuelimisha, kukosoa, kuburudisha na kukumbusha jamii yale yote yanayostahili kuenziwa au kuachwa. Lakini kwa kusahau kuwa sanaa ni taaluma kumekuwa hakuna fikra za kina katika hadithi za filamu zetu nyingi, hatufanyi tafiti ili kuzalisha hadithi bora na za kusisimua, pia hatuwekezi vya kutosha katika uzalishaji wenye tija kwa mlaji au msambazaji.

Matumizi ya mchanganyiko wa lugha kama yale ya hadithi za Kiswahili lakini jina ni la Kiingereza, inaashiria kuwepo ukosefu wa utaalamu, kukosa uzalendo na uelewa mdogo wa misingi ya fani husika katika utamaduni wetu.

Mwisho ni kwa watazamaji wa sinema zetu, wanapaswa kuacha uvivu wa kusema ukweli, kwani naamini kuwa wao ni watazamaji wazuri wa sinema, siyo tu za kwetu bali hata zinazotoka nje. Hivi hadithi zote wanazozijua, au filamu zote za Kizungu na Kihindi walizoziona hazijawawezesha kutambua tofauti ya nini bora na nini kibovu?


Alamsiki.

No comments: