May 30, 2011

Wizara kukamilisha muswada wa hatimiliki na hakishiriki

 Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Cyril Chami

Kuanzia mwaka 2006 kumekuweko na mchakato uliokuwa unaratibiwa na Rulu Arts Promoters, wa marekebisho ya sheria ya hakimiliki iliyoko ili kuondoa mapungufu yaliyopo. Kinachokwamisha sheria hii kwenda Bungeni ni Wizara husika - ya Viwanda na Biashara kuwa na kigugumizi. Hatimaye Waziri wa Viwanda na Biashara ametamka rasmi kuwa sasa wameondoa kigugumizi hicho:

Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko imethibitisha hayo kuwa iko katika mchakato wa kukamilisha muswada wa mabadiliko ya sheria ya hakimiliki na hakishiriki ili kudhibiti wizi wa kazi za wasanii nchini.


Akizungumza kwa njia ya simu, Waziri wa wizara hiyo, Cyril Chami, alilisititiza kuwa, serikali inatambua kilio cha wasanii juu ya uboreshwaji wa sheria ya hakimiliki na hakishiriki ya mwaka 1999 na kwamba, jitihada zinafanyika kufanikisha marekebisho hayo.

“Wizara inatambua kilio cha wasanii na inajali maslahi, wasanii ni kundi muhimu na tunalipa umuhimu na umakini unaostahili, kazi zao zinahitaji kulindwa na kuheshimiwa na kumekuwa na jitihada kuhakikisha hilo linafanyika,” alisema Chami.

Waziri Chami alibainisha kwamba, kuchelewa kwa mchakato wa kupitisha muswada huo, kunatokana na tofauti zilizopo kati ya makundi mawili ya wasanii, lile la muziki na wa fani nyinginezo, ambazo zitajadiliwa katika kikao baina ya wizara mbili.

Wizara hizo ni ile ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na ile ya Viwanda, Biashara na Masoko.

No comments: