May 11, 2011

Tasnia ya filamu Tanzania bado ni sekta ya 'kuganga njaa'

Wasanii wa maigizo kama hawa wa kundi la ABY la Buguruni Malapa wanahitaji kuwezeshwa ili kufikia malengo yao


FILAMU kama zitachukuliwa kwa umakini mkubwa zinaweza kuwa chanzo kikubwa na muhimu sana katika kujenga taifa na zinaweza kutumika kama jukwaa la kuchochea mijadala nchini kote, lakini bahati mbaya bado tasnia hii hapa nchini imekuwa inakabiliwa na changamoto kadhaa.

Tasnia hii imekuwa ni sekta ya kujikimu, licha ya ukuaji wa haraka unaoonekana. Ukweli ni kwamba bado mavuno halisi ya tasnia hii katika kukuza pato la Taifa na hata watayarishaji walio wengi bado hawajafanikiwa kupata matokeo mazuri kiuchumi kupitia filamu.


Pia bado tasnia hii ya filamu inabakia kuwa aina ndogo ya sekta ambayo imekuwa mfano wa “ili mradi mkono uende kinywani”, huku watayarishaji na wasanii wakiwa wanaitumia ili kujaribu kuweka mambo yaende sawa mezani. Kamwe haijawahi kuwa sekta endelevu ambayo taifa linaweza kujivunia.

Ingawa kumekuwepo juhudi nyingi kutoka kwa wadau mbalimbali kutaka sekta hii ikue na iweze kuleta tija, lakini juhudi hizo bado hazijaweza kutoa mavuno stahiki katika kile tunachoweza kuita pato linalotokana na uchumi wa kweli wa tasnia ya filamu.

Hali halisi ya soko la filamu la Tanzania linaifanya hatma ya wasanii wengi kuishia kulipwa pesa kiduchu (peanuts) ambazo wala haziwasadii kujiendeleza bali kwa mlo wa siku chache. Pia watayarishaji wengi wamekuwa wanapendelea kuwatumia wasanii walewale (hasa wakongwe) katika kila sinema kwa kuogopa kwamba nyuso mpya 'haziuzi', kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kimekuwa kikiathiri sana ukuaji wa vipaji.

Bahati nzuri kwa Tanzania, na nchi ya Rwanda, ingawa hazimo katika ngazi moja na mataifa ya Magharibi au Afrika ya Kusini, lakini zimekuwa na mafanikio kiasi katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Tafiti nilizowahi kufanya zimeonesha kuwa filamu zinaweza kuwa chombo muhimu sana cha kijamii na kiutamaduni kwa ajili ya kujenga umoja miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Watazamaji wa Kitanzania kati ya wana-Afrika Mashariki wameonekana kuzipenda sana sinema zao pamoja na kuwepo kasoro nyingi na wamekuwa na hamasa kubwa. Kama zilivyo sinema za Nigeria ambazo alama yake kubwa ya kibiashara ni Kiingereza chao aina ya Pidgin, Kiswahili cha kisasa cha Tanzania kinazipa utambulisho wa kitaifa filamu zetu.

Ili kuiendeleza sekta ya filamu, serikali ya Tanzania na wadau, kwa dhati kabisa wanapaswa kulisaidia Shirikisho la Filamu Tanzania ili kuwawezesha watayarishaji na wasanii kupata mafunzo ya kitaalam kwa njia ya warsha na semina ili kuongeza uwezo wao.

Pia Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza inapaswa kuwa macho zaidi na kuhakikisha kuwa filamu zote zinakaguliwa kabla hazijaingia sokoni kwa sababu ya unyeti wa maudhui yake ili kulinda maadili ya nchi hasa kwa taifa kama letu linaloendelea.

Taarifa zozote zinazopatikana hazipaswi kuchukuliwa kiutani au kama 'anasa' kama ilivyo katika nchi zilizoendelea, Bodi ya Ukaguzi kiwe ni chombo kwa ajili ya maendeleo, uzoefu wa kitamaduni na kwa ajili ya kuleta maana katika maisha yetu ya kila siku.

Makala zangu kadhaa zilizopita zilileta tafsiri tofauti kwa baadhi ya wasomaji kwamba nilionekana wazi kuipinga Bodi ya Ukaguzi kwa “kuirushia mawe”, lakini ukweli ni kwamba sina ugomvi wowote na bodi wala mtendaji yeyote ndani ya bodi bali kama mwanaharakati wa masuala ya filamu, nina jukumu la kuhakikisha maadili ya Taifa yanalindwa.

Kamwe hatutakiwi kukaa tu na kusema filamu ni burudani tu, hapana; siamini kabisa katika kaulimbiu hii. Naamini kuwa tunapaswa kuona filamu, mbali ya kuwa ni burudani lakini kama chombo maalum kwa ajili ya maendeleo ya Taifa kwa sababu ndivyo imekuwa ikitumiwa na nchi nyingine zilizoendelea.

Ili kujihakikishia soko katika Afrika, Ulaya na hata Marekani, filamu zetu zinapaswa kukaguliwa kwa umakini zaidi na kusajiliwa na Chama cha Hakimiliki (Cosota). Pia lazima ziwe zilizotokana na script nzuri, zilizotengenezwa kiufundi, zenye ubora na utaalam wa kitaalam. Pia hazitakiwi kutengenezwa kwa mtindo uliozoeleka sasa wa sehemu mbili (Part 1 na 2) kitu kinachoshusha ubora wa filamu husika.

Jumamosi ya wiki iliyopita nilipata mwaliko wa kuwa mzungumzaji kwenye kipindi cha moja kwa moja cha asubuhi “Baragumu” kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten, ambapo mada kuu ilikuwa changamoto zilizopo katika tasnia ya filamu hapa nchini.

Kwa kweli katika kipindi hicho sikutegemea kabisa kama hoja nilizoanzisha zingeweza kuibua mjadala mpana sana kiasi cha waandaaji kuona haja ya kunialika tena kwenye kipindi kama hicho wiki chache zijazo ili kumalizia yale niliyoyaanzisha. Lakini niseme tu ukweli, Watanzania wanazipenda sinema zetu ingawa wanakatishwa tamaa na kasoro zilizopo kwenye filamu ambazo hazionekani kutafutiwa ufumbuzi.

Niliweza kuhisi uchungu na hasira walizokuwanazo wadau pindi wakipiga simu kuchangia kwenye mada hiyo, lakini nawaomba watambue kuwa changamoto ni nyingi zinazoikabili tasnia yetu, mbali ya kukosa ufahamu wa namna ya utengenezaji wa filamu kwa watayarishaji wetu, uelewa mdogo wa wasanii, ukosefu wa miundo ya soko la kuuza kazi, tatizo lingine kubwa ni ukosefu wa mitaji.

Mtaji limekuwa ni tatizo kubwa linaloumiza vichwa vya watayarishaji wa filamu kwa muda wote tangu Watanzania walipoanza kufanya filamu mpaka sasa.

Angalia sinema za Marekani, India au Afrika Kusini utaona jinsi zinavyoashiria uwekezaji mkubwa katika filamu zao, mavazi, mandhali ya kuvutia, ufundi, uongozaji na kadhalika, vyote hivi ni kutokana na uwekezaji. Wazalishaji wangapi wa Kitanzania wanaweza kumudu kutumia japo robo ya robo ya robo (1/64) ya kinachotumika Ulaya, India, au Marekani?

Tasnia ya filamu Tanzania ipo katika mparaganyiko mkubwa mno kutokana na ukosefu wa fedha katika sekta ya filamu, kitendo kinachochangia kikundi kidogo cha watu fulani kulihodhi soko la filamu huku serikali ikijua na bila kuchukua hatua.

Kwa takriban miaka 10 sasa kilio cha wasanii na watayarishaji wa filamu, mbali ya wizi wa kazi zao kimekuwa ni ukosefu wa mtaji wa kutengeneza filamu, ingawa mwezi Septemba 1998, ulianzishwa Mfuko wa Utamaduni na Serikali, ambao hata hivyo haukuwa na ufanisi kwa kuwa uligubikwa na matatizo lukuki.

Madhumuni makuu ya mfuko huo yalikuwa kuimarisha na kuiwezesha sekta ya Utamaduni (filamu zikiwemo) kuchangia kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa kuhamasisha jamii kujituma kufanya shughuli za utamaduni zenye kuchochea ubunifu, kuzingatia ubora wa bidhaa na huduma, kuongeza kipato katika kaya na kuhimiza ajira za kujitegemea.

Tangu mwaka 1998 ulipoanzishwa Mfuko, Mawaziri wote waliopita Wizara ya Utamaduni wameshindwa kuandaa mkakati mzuri wa kusaidia upatikanaji wa pesa au kusaidia Mfuko kwa ajili ya watengeneza filamu kwa maendeleo ya Taifa, kwa sababu hakuna yeyote kati yao aliyeifahamu vizuri nguvu ya sekta ya filamu.

Pia kulikuwepo madai ya ufisadi au kutotumia pesa zilizotolewa na wahisani kwa ajili ya kuwawezesha wasanii na wadau wa utamaduni katika kufanikisha malengo. Walionufaika aidha walikuwa wanajuana na wahusika au ni ndugu, marafiki au maswahiba wa kibiashara. Binafsi sina uhakika katika hilo.

Lakini wakati nafanya utafiti kuhusu tasnia ya filamu nilielezwa na mmoja wa wajumbe wa bodi ya Mfuko kuwa maombi yaliyotumwa kwao yalikuwa mengi kuliko pesa iliyotolewa, ila maombi kadhaa yaliambatana na 'memo' kutoka kwa wakubwa kutaka kiasi kikubwa cha pesa. Ili kuhakikisha kuwa watu wengi wanawezeshwa, watendaji walilazimika kutoa fedha kwa watu wenye maombi ya pesa ndogondogo ambazo hata hivyo hazikuweza kuleta tija katika kazi zao.

Mfuko wa Utamaduni uliopaswa kutoa 'grants' kwa wasanii na wazalishaji katika sekta na tasnia ya sanaa nchini, ulifanya wachache kujinufaisha kinyume na sheria ingawa ushahidi wa wazi katika hili sina lakini kimazingira ushahidi upo.

Inasemekana kuwa serikali ambayo ilikuwa na jukumu la kuchangia katika mfuko huo haijawahi kufanya hivyo mpaka wafadhili walipoamua kujiondoa kwani pesa walizokuwa wanachangia zilianza kufanya kazi tofauti na kile kilichokusudiwa.

Tasnia ya filamu hapa nchini itaendelea kuwa sekta ya kuganga njaa kama hali itaachwa kama ilivyo ingawa serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inajaribu kuangalia namna itakavyoweza kuingiza mapato kupitia tasnia za filamu na muziki.

Kwa kweli ubunifu katika sekta ya burudani na sanaa - filamu - katika nchi karibu zote za Afrika umekuwa unakwazwa na ukosefu wa fedha jambo ambalo limekuwa ni tatizo kubwa katika jitihada za kukuza na kuendeleza sekta.

Ili tasnia ikue pande zote, serikali na sekta binafsi zinapaswa kuwa na sera nzuri, kinyume na ilivyo sasa ambapo hawana sera nzuri za sekta na wala hawafikirii kuipa kipaumbele tasnia hii. Hata hivyo, sekta hii imekuwa chanzo cha pato la mabilioni ya dola kwenye mabara mengine.

Alamsiki.

No comments: