May 4, 2011

Changamoto zinazoikumba tasnia ya filamu Tanzania

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Magolyo Maige

 Steven Kanumba katika movie ya This Is IT

INASEMWA kwamba eti tasnia ya filamu nchini Tanzania inazidi kukua siku hadi siku, kwani mtayarishaji wa filamu wa Tanzania anaishije leo ukitofautisha na miaka ya nyuma? Ni nani anayetoa fedha kuimarisha tasnia hii? Kama kweli tasnia imekua mbona hali halisi ya soko la filamu inabana sana uwezekano wa kuibuka kwa wasanii, watayarishaji au waongozaji wapya?...

Naamini kuwa filamu za kibongo zinakubalika sana katika ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo ya ukanda wa Maziwa Makuu, lakini vipi kuhusu maisha ya wasanii wa Tanzania, je, wanapata stahili yao na wanaishi kwa kutegemea filamu pekee? Naomba majibu yako tafadhali”.

Haya ni maswali magumu niliyotakiwa kuyajibu na mmoja wa wasomaji wa makala zangu aliyejitambulisha kwa jina la Boniface Kurwa, mkazi wa Kibaha-Mikongeni akitaka kupata ufafanuzi kuhusiana na dhana nzima ya kukua kwa tasnia ya filamu hapa nchini kama ambavyo amekuwa akisikia.

Kukua kwa tasnia ya filamu hapa Tanzania pia kumewahi kusemwa na Rais Jakaya Kikwete wakati alipokuwa akilizindua Bunge la Kumi, mjini Dodoma. Pamoja na kuzisifia sinema za Tanzania Rais Kikwete pia alisema kuwa filamu za Tanzania zimeanza kuitangaza vyema Tanzania katika medani ya kimataifa kutokana na kuonekana katika kituo cha runinga cha Africa Magic.

Nimewahi kuandika makala iliyokuwa na swali kama kweli soko la filamu hapa nchini linakua na nikaeleza jinsi ninavyotofautiana na wengine kuhusu kukua kwa tasnia yetu. Lakini kwa faida ya wengi nitajaribu kuyajibu maswali ya msomaji wangu huku nikijaribu kukwepa kurudia niliyowahi kuyaandika hapo nyuma kwani tayari yamehifadhiwa kwenye tovuti zangu.

Ni kweli, kinadharia tasnia ya filamu hapa nchini imekua sana, kwa kigezo cha sinema zetu kuuzwa sana mitaani, huku wanawake na vijana ndio wakiwa wateja wakubwa wa sinema hizi. Pia ukipata bahati ya kutembelea nchi kama Kenya, Congo DRC, Rwanda na Burundi kwa mfano, na wakagundua kuwa wewe ni Mtanzania utakuwa katika wakati mgumu sana kwani utaulizwa maswali mengi kuhusu filamu na wasanii wa Kitanzania na wengi wao wakitaka uwape maelezo mengi kuhusu hizo filamu na wasanii.

Katika makala zangu nimekuwa nikisisitiza sana kuwa sekta ya filamu hapa nchini kama ilivyo katika nchi zilizoendelea imesheheni utajiri mkubwa sana wa utamaduni na uchumi. Tatizo kubwa tulilonalo ni mfumo uliopo, pia tasnia hii bado haijarasimishwa na hivyo kusababisha wadau wake waendelee kuwa masikini wa kutupwa huku serikali nayo ikikosa mapato.

Kwa miaka mingi sasa, wasanii na watengenezaji wa sinema miongoni mwa wadau wengine wa sanaa wameendelea kutoa sinema nyingi hapa Tanzania ili kujipatia riziki kutokana na kazi yao bila mafanikio. Ingawaje ukweli unaendelea kubakia kuwa sekta ya filamu ndiyo sekta yenye thamani ya mabilioni ya fedha, lakini wasanii na watengeneza sinema wengi wa Kitanzania wameishi na kufa maskini.

Tasnia ya filamu hapa nchini bado inahodhiwa na kundi dogo tu la wafanyabiashara ambao ndiyo wenye maamuzi ya mwisho kama sinema yako iuzwe au la, na huwezi kuingiza filamu yako sokoni bila kuwemo majina au picha za 'masupastaa' fulani wanaoaminika 'kuuza', vinginevyo weka filamu yako nyumbani uangalie na familia yako. Hili kwangu ni jambo ninalolitafsiri kama kichekesho cha mwaka.

Hawa wanaoitwa au kujiita 'Masupastaa' wa Kibongo ukitaka kuwashirikisha kwenye sinema yako, hupatikana kwa gharama kubwa ambazo mara nyingine huweza hata kuzidi fedha za maandalizi mengine, kitendo kinachoashiria king'ora cha hatari kwa muandaaji mdogo wa sinema kuingia kwenye hasara.

Watayarishaji waliojiingiza kwenye biashara ya filamu na kuamua 'kukomaa' kwa kuwashirikisha wasanii chipukizi au wapya katika fani wengi wamejikuta wakipata hasara kubwa kwa vile sinema zao hukosa soko na wala haziwezi kupata msaada wa matangazo (Promosheni) kwa urahisi.

Unapoizungumzia tasnia yoyote ya filamu duniani unazungumzia maandalizi na utengenezaji wa filamu ambao umegawanyika katika hatua tano kuanzia kwenye hatua ya mwanzo kabisa ya uandaaji wa filamu,
Development: hatua hii huanzia kwenye wazo (concept) na kuishia kwenye drafti ya mwisho ya muongozo au mswaada andishi (final draft) wa sinema.

Baada ya hapo huingia hatua ya pili inayojulikana kama Pre-production: maandalizi maalum kabla ya kuanza uzalishaji (upigaji picha), hatua ambayo waigizaji (cast) na watendaji (crew) wanapotafutwa, pia maeneo huandaliwa au kutafutwa. Na hatua ya tatu hujulikana kama Production: hapa ndipo uzalishaji hufanywa kwa kupiga picha za filamu.

Hatua ya nne huitwa Post-production: ambapo filamu inahaririwa, kutiwa sauti na nakshi zingine ili kuiboresha. Na hatua ya mwisho ni Sales and distribution: katika hatua hii sinema huingizwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa.

Kwa hiyo tunapoongelea tasnia ya filamu kukua tunaligusa zao lililokamilika (final product) kwa maana ya filamu iliyokamilika. Biashara ya filamu hapa nchini bado imeendelea kutegemea sana utashi wa wasambazaji kuikubali filamu utakayowapelekea, kwani hapo ndipo wanapoweza kutoa malipo mliyokubaliana na wao kuendelea na kazi ya usambazaji au waamue kukutosa.

Wameamua kuifukarishwa makusudi tasnia ya filamu kwa sababu hali iliyopo inawanufaisha, hivyo wanajitahidi 'kubana' ili hali iendelee kuwa hivi na waendelee kuwanyonya walio wengi.
Naamini lengo la tasnia yoyote ya filamu duniani ni kujaribu kujenga mazingira ya sekta ya filamu kujitegemea (self-sustaining), ambapo zitatengenezwa filamu kwa fedha kidogo kuliko zinazopokewa kutoka kwa watazamaji, kwa maana ya kujipatia faida nzuri. Si kama ilivyo hapa nchini ambapo mtengenezaji wa filamu hana uhakika kama atarudisha pesa zake.

Kinadharia kama nilivyosema awali, soko la filamu linakua lakini katika hali halisi ni kinyume chake. Tasnia ya filamu inazidi kuparaganyika. Huwezi kupima maendeleo ya soko la filamu kwa kutazama watu wawili au watatu wanaoendesha magari ya kifahari huku idadi kubwa ya wasanii na watengeneza filamu wakiwa bado hohehahe kwa kanuni wa wataalam wa takwimu ya “Head in the oven and legs in the freezer, the average is comfortable!

Kipimo bora cha kuangalia kama tasnia ya filamu inakua ni kufuatilia mapato na makusanyo ya kodi (revenue) kupitia filamu, au kumbukumbu za mapato kwenye tasnia ya filamu. Kwa mfano tasnia ya filamu ya Nigeria (Nollywood) inachangia pato la dola za Kimarekani milioni 450. Tasnia ya filamu nchini Afrika Kusini inaingiza Rand 7.7 bilioni. Nani anaweza kuniambia Tanzania inachangia kiasi gani cha mapato kupitia filamu?

Kama tasnia hii itarasimishwa kwa maana ya kusajiliwa kwa kazi za sanaa, kuwa na jina la biashara, zikifanywa kikampuni, zenye leseni ya biashara, zenye eneo/mahali maalum pa kufanyia kazi, zilizo kwenye kumbukumbu inayoeleweka, zinazotofautisha mali ya biashara na binafsi, ukiongeza na idadi ya Watanzania ambao ni zaidi ya milioni 42, na idadi ya watu takriban milioni 90 katika Jumuia ya Afrika Mashariki lilipo soko letu, kunakuwa na soko zuri na faida kubwa katika kazi hizi, bila hata kutegemea watazamaji walio nje ya Jumuia ya Afrika Mashariki.
Cha kusikitisha, hii si kitu kwa wakati huu, kutokana na sababu kadhaa, hasa mfumo uliopo, ukosefu wa miundo mizuri ya usambazaji na utofauti wa sera miongoni mwa nchi za Jumuia, hasa katika suala la lugha juu ya changamoto za uharamia wa kazi za sanaa.

Wakati faida ya kuirasimisha sekta ya filamu kujitegemea ndilo linalopaswa kuwa lengo, filamu inaweza kuwa kitu muhimu sana inayostahili msaada na ufadhili kutoka serikalini, sekta ya utalii na taasisi za kitamaduni.

Hata yale mapungufu yanayotajwa sana katika tasnia ya filamu nchini ya uigizaji wa filamu za Kitanzania kwa wasanii wengi kushindwa kuvaa uhusika, upungufu wa vitendea kazi, maeneo ya kuigizia na hata ukosefu wa taaluma katika sanaa hiyo yatakwisha kwa kuwa watengenezaji wataweza kuwalipa vizuri watendaji wenye taaluma tofauti na ilivyo sasa ambapo wanawakwepa.

Alamsiki.

No comments: