Oct 27, 2010

Uchambuzi wa John Kitime



Mwanamuziki mkongwe na mchambuzi wa sanaa, John Kitime

Kufuatia viwango duni vinavyooneshwa na wasanii wa Kitanzania katika nyanja nyingi,  John Kitime ametoa makala kupitia mtandao wa "Wahapahapa" BOFYA HAPA wenye kichwa cha habari: 2010 Ukungu Bado Mwingi. Makala hii nimeiweka hapa kwa kuwa nadhani ni muhimu ikaendelea kusomwa kupitia vyanzo mbalimbali.

Tunaanza mwaka, kuna wanaofurahi kuna wanaowaza itakuwaje mwaka huu. Kuna wanaoona mwaka huu kuwa wa uhakika katika mafanikio, kuna wanaoogopa hata kuanza mwaka. Katika sanaa naona ukungu bado mzito.



Katika wimbo wake mmoja, Peter Tosh alisema ‘…people want to go to heaven, no one wants to die…”, tafsiri yake ni ‘…watu wanataka kwenda peponi lakini hakuna anayetaka kufa…’ Na hiyo ndiyo hali halisi katika shughuli za sanaa Tanzania na hasa muziki na filamu.

Asilimia kubwa ya wasanii watakwambia kuhusu ndoto walizonazo kama vile kuingia soko la kimataifa na kadhalika, lakini hawahangaiki kufanya utafiti wala mazoezi ya kustahili, hata juu ya kazi zao ambazo wanataka zikatingishe ulimwengu.

Bado wanamuziki wanaiba nyimbo za wenzao na kazi za wenzao na kuzirekodi tena au kuzitangaza ni zao kwa kubadili majina, kwa mfano ukiingia katika kumbi za muziki wa dansi , ni kuiga kutupu kuanzia uvaaji wa wanamuziki, wachezaji wao, aina ya uimbaji, uchezaji, na mbaya zaidi kwa kuwa karibu wote wanaiga sehemu moja bendi nyingi zinafanana utadhani zimefanya mazoezi pamoja. Kwa mtindo huu ni wazi 2010 bado ukungu mzito.

Bongo fleva imejaa nyimbo nyingi zilizonakiliwa kutoka kwa wanamuziki mbalimbali wa nje, na pia hata huku kuiga mpaka mavazi na uchezaji na hata namna ya utengenezaji wa video unafanya kazi nzima iwe ni kivuli tu cha kazi kutoka nje.

Kuna watengeneza muziki maarufu kama maproduza, ambao wako tayari kukubali kurekodi wasanii ambao walitakiwa kupewa ushauri wa kuacha kuimba. Mara nyingine waimbaji ni wazuri lakini muziki unakuwa hauna uhusiano wowote na uimbaji kutokana na mapungufu ya produza, hivyo basi kuwa na maana kwa wale tu ambao wanafahamu lugha inayoimbwa, muziki ni sifuri.

Ukijumlisha na tatizo sugu la rushwa na upendeleo katika vyombo vya habari, muziki huu ambao haukustahili kurushwa hewani hurushwa tena na tena na kuwafanya wanamuziki chipukizi kuiga makosa ambayo huwa yanaachiwa kuletwa hadharani.

Pamoja na kuweko kwa wasanii wazuri wa filamu, tatizo ambalo linaota mizizi la kuhusisha katika uigizaji watu maarufu ili kuuza filamu linaishusha hadhi kazi ya uigizaji. Uigizaji wa kila kitu toka Nigeria unaathari kubwa katika kuendeleza soko la filamu za Tanzania. 


Hivi kwani ni lazima hata wanakijiji katika filamu zetu wapake rangi kama wanakijiji katika filamu za Kinigeria. Siku hizi waganga wa jadi katika filamu zetu lazima wavae mavazi mekundu kwa vile Wanigeria wanafanya hivyo, hiki ni kichekesho mno. Hata majina ya filamu lazima yawe ya Kiingereza kwa kuwa Wanigeria wanafanya hivyo, kuna ulazima huo?

Aibu kubwa hutukuta wengi tunaoangalia Africa Magic, pia na hasa kwa vile tunajua kuwa mamilioni ya watu wanaangalia kutoka sehemu mbalimbali duniani, yale maandishi ya Kiingereza ambayo ndiyo hudaiwa kuwa tafsiri ya mazungumzo ya Kiswahili katika filamu, mara nyingi ni tafsiri mbovu na mara nyingine siyo kabisa, wasanii wa filamu mnajitoa wenyewe katika mashindano ya soko la dunia.


Serikali ijiangalie upya ushiriki wake katika utamaduni. Japo naona ukungu maana huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo ni muhimu kwa serikali baada ya uchaguzi kutokufanya kiinimacho kuhusu idara ya utamaduni. Watendaji wawekwe ili ngazi zote ziwepo, mkoani, wilayani na kadhalika.


Utamaduni ndiyo huzaa maadili, mkanganyiko wa maadili kwa sasa ni matokeo ya serikali kujiweka mbali na Utamaduni na kutegemea utajiendeleza kama hewa angani, wafanya biashara ndio walioshikilia bango la utamaduni wa Tanzania, na tafsiri za utamaduni zinapindishwa kutokana na mahitaji ya kibiashara. Ni ngumu kwa wasanii wa Tanzania kuwa na maendeleo ya jumla katika hali hii ambapo hata sera ya sekta hii haitoshelezi kabisa.

Hakimiliki imekuwa tatizo, wasanii washirikiane na vyombo vilivyopo, wito kwa wasanii wenye majina makubwa, kadri unavyokuwa juu ndio unavyoibiwa zaidi lakini hawa ndo' wa mwisho kutoa ushirikiano na vyombo vinavyohusika na haki zao.

Wasanii unganikeni. Wafanyabiashara wanawaunganisha ili waweze kuwanyonya zaidi, tengenezeni vyombo vyenu. Vyombo vya habari vinahitajika kuwa na ukweli zaidi, vichwa vya habari kama vile,’…apagawisha Manzese’ au ‘…Dar nzima wajazana onyesho la Kitime’, wakati lilikuwa na watu kiduchu linaua vikundi na si kuendeleza. 2010 ukungu mtupu.

John FKitime
0713274747
jkitime@yahoo.com  

No comments: