Oct 27, 2010

FILAMU ZA KITANZANIA: Ni kweli tuna wakosoaji wa filamu? (3)

 Darasa la ufundishaji wa mafunzo ya filamu (workshop in filmmaking)

NI Ijumaa nyingine, naamka asubuhi na mapema, nawahi usafiri wa kuelekea Posta, kisha naelekea Upanga ambako kipo kituo cha utamaduni cha Ujerumani (Goethe Institut) kunakofanyika mafunzo ya utengenezaji wa filamu (workshop in filmmaking). Mafunzo yaliyoanza wiki mbili zilizopita na yanahitimishwa leo. Mimi ni mmoja wa vijana waliochaguliwa kuhudhuria mafunzo hayo ya nadharia na vitendo yanayoendeshwa na wataalamu waliobobea katika tasnia ya filamu kutoka Ujerumani na Ufaransa kwa ushirikiano wa balozi za Ujerumani na Ufaransa, na kuratibiwa na Goethe Institut na Alliance Francaise.


Nafika kwenye eneo la mafunzo na kuingia darasani mnamo saa tatu asubuhi, mara napokea meseji tatu mfululizo kutoka kwa watu nisiowafahamu, mmoja kati ya walionitumia meseji anaandika ujumbe kunishukuru kwa kuwa nimekuwa namuelimisha kupitia hoja zangu, na wawili wananishutumu vikali, eti kwa kuwa najifanya mjuaji sana wakati sijui lolote. Nazidharau meseji hizo kwa kuwa kwanza siwajui hao waliozituma ingawa nashindwa kuelewa wamepata wapi namba yangu. Wakati nikiwa bado natafakari mara inaingia meseji nyingine kutoka kwa binti aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Happy, huyu ananiomba nimtumie namba ya Kanumba. Nazidi kushangaa zaidi, lakini naamua nimpigie simu nimuulize alikoipata namba yangu. Kabla sijaweza kupiga simu inaingia meseji inayonizindua, hii ni meseji inayotoka kwa rafiki yangu Afrika Salim, msomaji wa makala zangu anayesoma Chuo Kikuu cha Dodoma.

Hapo hapo nakumbuka kuwa leo ni Ijumaa, siku ambayo gazeti la Kulikoni linatoka. Napata hamasa kuwa kumbe ujumbe wangu umefika nilikokusudia na natamani nitoroke darasani nikalitafute gazeti la Kulikoni. Nikiwa bado natafakari zinaingia tena meseji zingine mbili, moja ikitoka kwa kiongozi wa chama cha waongozaji wa filamu Tanzania (Tafida) akinitaka nihudhurie kikao cha waongozaji wa filamu siku ya Jumamosi asubuhi pale Kinondoni. Meseji nyingine inatoka kwa mtu ambaye hakujitambulisha jina lakini aliyeonesha kukerwa sana na makala yangu. Pia nakumbana na vituko vya watu wanaopenda kubipu mithili ya wendawazimu. Naamua kuzima simu kwa kuwa nashindwa kufuatilia mafunzo darasani.

Kesho yake, Jumamosi napata tena meseji kadhaa, moja ikitoka chama cha waongozaji wa filamu ikinikumbusha umuhimu wa kuhudhuria kikao, nyingine ikiwa ni namba ninayoshindwa kuielewa ni ya nchi gani inanitaka eti nisimchague mmoja wa wagombea urais wa chama fulani kwa sababu ni muongo, mnafiki na anataka kuitumbukiza nchi kwenye vita, nakumbuka kuwa nilisikia kwenye vyombo vya habari kuhusu ujumbe huo, naufuta kwenye simu yangu kwa kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote na sipendi kabisa kujihusisha na siasa, kwangu mimi siasa ni 'si hasa', yaani uongo mtupu na ndiyo iliyotufikisha hapa. Ujumbe huo unanifanya nimchukie mtu aliyenitumia kwa kuwa rais nitakayemchagua Oktoba 31 tayari namjua wala sihitaji mtu kunipangia. Saa nne kasoro dakika kumi na saba ndipo inapoingia hii meseji ninayoikusudia leo.

Nimeseji iliyotumwa na msomaji mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha kwangu lakini alitumia namba ya simu 0784 413270 na ujumbe wake uliandikwa hivi; “That's too subjective Mr. Hiluka. Wewe pia huna tofauti na hao 'critics' kwani unatumia nafasi ya gazeti kulinda kazi zako. Washauri wakasome watapata wawekezaji. Wanapowalinganisha na Wanigeria... wenzao wanasoma film & art, it's good thing wajue tatizo ni nini!”

Ujumbe huu unanifanya nikumbuke kisa nilichokisikia miaka mingi iliyopita wakati huo nikiwa darasa la tano; kisa cha viumbe wawili, dume la simba na dume la nyani waliokuwa wakienda kwenye sherehe. Dume la nyani kama kawaida yake lilikuwa likitembea taratibu, simba akamcheka sana nyani huku akimuuliza kwa mwendo wake atafika saa ngapi waendako. Nyani alimjibu simba kuwa mwendo si kitu cha maana ni kujua uendako. Simba akamwambia nyani kalagabaho na kutimua mbio kuwahi sherehe mkia juu, nyani aliendelea na safari yake kwa mwendo wa taratibu akiamini kuwa atafika aendako. Alipofika njia panda kwa mbali akaona kitu chekundu kikitingishika, aliposogea akamkuta simba akiwa kalala chali ametapakaa damu kifuani, nyani akamuuliza simba kulikoni? Simba alimjibu nyani kuwa alipokuwa akikimbia hakujua kama mbele yake kulikuwa na kisiki na hivyo kimemchana kifua, nyani akamkumbusha simba kuwa mwendo si kitu cha maana ni kujua uendako... simba alikufa papo hapo kwa aibu.

Sijajua msomaji wangu alikusudia nini aliposisitiza kuiga kutoka kwa Wanigeria. Tuige usomi wao au sinema wanazotengeneza? Mimi sioni kitu kinachoashiria usomi kwenye kazi zao nyingi ingawa zipo chache nzuri.

Msomaji anaposema kuwa watengeneza sinema wa Tanzania wakisoma watapata wawekezaji nashindwa kumuelewa, wawekezaji gani hawa wanaosubiri kina Kanumba wasome ili wawekeze wakati kuna utitiri wa vijana wasomi waliomaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam idara ya Sanaa (FPA) na vyuo vingine ambao wapo tu mtaani na wameshindwa kutengeneza sinema kutokana na mfumo mbovu uliopo! Kwa nini wawekezaji wasiwekeze kwa vijana hawa kama suala ni kusoma kwanza ndipo wawekeze!

Msomaji huyu na wakosoaji wa filamu za Kitanzania wanaong’ang’ana na mifano ya kisomo bila kujua matatizo halisi kwenye tasnia hii ni kutowatendea haki watengenezaji wa filamu wa Kitanzania, walipaswa kuwatia moyo kwa kuwa wamethubutu japo mazingira na mfumo ni mbovu na wametekeleza sera ya kujiajiri kama Rais Kikwete anavyotaka.


Msomaji huyu bado anaendeleza mfumo mbovu uliopo nchini wa 'wasomi' kujijengea ukuta wa 'sisi wasomi na wao hawakusoma' badala ya kujenga daraja litakalowaunganisha wadau wote ili kuhakikisha tasnia hii inakua. Kwa taarifa tu ni kwamba filamu zimegawanyika katika makundi mawili; commercial films (filamu za kibiashara) na artistic films (sinema za miradi kama vile malaria, ukimwi n.k).

Unapozungumzia sekta ya filamu katika nchi yoyote unazigusa filamu za kibiashara ambazo hapa Tanzania ndizo zinazopondwa kwa kuwa zinaonekana kwa watu na wala huzigusi filamu zinazotengenezwa kwa makusudi ya NGO fulani kwa kuwa mwisho wake ni kuishia kwenye makabrasha au maktaba. Sasa wewe kama Mtanzania msomi unapoanza kuwabagua Watanzania wenzako kwa kigezo cha usomi wako na kuwabeza wanapotengeneza sinema mbovu siioni mantiki ya usomi wako kwa kuwa hauisaidii jamii.

Kauli ya “washauri wakasome” si ya kizalendo na inanifanya nimuone msomaji huyu kuwa anajitoa kabisa kwenye jukumu la kuielimisha jamii, watengeneza sinema wakiwemo, utadhani yeye si Mtanzania! Wakasome wapi wakati hatuna vyuo vya filamu? Hata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hawafundishi filamu. Asilimia kubwa sana (kama siyo wote) ya watengeneza sinema wanatoka kwenye familia zinazoishi chini ya dola moja ya Marekani, sidhani kama wanaweza kulipia masomo ya filamu ambayo kwa vyovyote inabidi wakayasome nje ya nchi tena kwa gharama kubwa. Pia suala la utoaji wa mafunzo na gharama za mafunzo kwa watengeneza filamu ni jambo linalopaswa kufanywa na serikali, bila msaada wa serikali au wawekezaji hakuna kinachoweza kufanyika.

Sipingi kabisa kuhusu suala la kusoma kwani naujua umuhimu wa kwenda shule. Lakini tujiulize ni kisomo tu ndiyo tatizo lililopo kwenye tasnia ya filamu hapa Tanzania?

Mbona matatizo yapo mengi sana na makubwa kuliko hata hili la usomi? Hayo msomaji huyu hayaoni au hayajui? Matatizo kama kushuka kwa thamani ya shilingi yetu mara kwa mara (gradual dip in the value of theTanzanian shillings) kunasabisha kudorora kwa tasnia ya filamu, sijui kama msomaji analijua hili.
Mengine ni pamoja na ukosefu wa mitaji (lack of finance) kwa watengeneza sinema, kukosekana kwa mfumo mzuri wa kuwawezesha kupata msaada wa mitaji (financial springboard), kukosekana kwa soko la uhakika (marketing support) la kuuza kazi za sanaa, kukosekana kwa fursa ya kupatiwa mafunzo watengeneza sinema, sheria dhaifu kuhusu uharamia (piracy) wa kazi za sanaa, hatuna sera ya filamu na mengine mengi.


Namshauri afuatilie mfumo unaotumika Afrika Kusini kupitia chombo chao 'National Film and Video Foundation (NFVF)' kabla hajakurupuka kunishutumu. Mfumo wao umewawezesha watengeneza sinema wa Afrika kusini ambao hawakubahatika kupata elimu ya taaluma kuwezeshwa na kupatiwa mafunzo ya weledi (hili ni somo maalum nitalizungumzia siku nyingine).

Pia namtaka msomaji akatafute kitabu kinachoitwa “WHAT THEY DON'T TEACH YOU at FILM SCHOOL: 161 strategies for making your own movie no matter what” kilichoandikwa na watu makini, kama atashindwa kukipata aniambie nimuazime cha kwangu asome labda ataelewa ninamaanisha nini. 




Washiriki wa workshop ya filamu iliyofanyia Goethe Institut 
wakijadili jambo wakati wa mapumziko

Mimi nilidhani msomaji huyo angeshauri katika suala la kuwatafuta wawekezaji ili wawekeze katika utoaji wa mafunzo ya vitendo (workshops in filmmaking) ya utengenezaji wa sinema. Kwa nini zisianzishwe NGOs za kusaidia utoaji wa mafunzo ya filamu? Badala yake wanaelekeza nguvu nyingi kwenye NGOs za ukimwi au kwa kuwa zinawaingizia chochote.

Msomaji huyu atambue kuwa kwenda shule na kupata elimu ya nadharia tu hakutoshi kutengeneza sinema nzuri kama ilivyo kwa Wanigeria ambao anataka tuwaige. Nchi hii imekosa mfumo mzuri kwa kuwa tumeonekana kukosa kabisa malengo (lack of vision). Bila malengo, watu wetu wataangamia kabisa (perish)… mfumo mzima wa maisha ya Watanzania umetawaliwa na siasa. Ndiyo maana wasomi wanakimbilia kwenye siasa maana ndiyo inayolipa, na watu hawataki kuambiwa ukweli. Mimi sitaki kuwa mnafiki.

No comments: