Sep 21, 2010

Serikali ina dhima ya kuokoa sekta ya filamu-2


Msanii nyota wa kike wa filamu za Bongo, Irene Uwoya

Ninapatashida kidogo kutokana na ukweli kwamba watengenezaji wa filamu wanaoinukia na hata wengi waliopo kwenye soko hili hapa nchini kukosa mfumo mzuri wa kuwawezesha kupata msaada wa mitaji (financials pring board) kwa kazi zao. Hata hivyo, kwa mtazamo wangu, nashauri serikali ijayo kuangalia kwa makini jinsi tunavyoandaa miundo ya kihazina (funding structure) katika kampuni na kazi zetu kabla haijaamua kuelekeza nguvu zake katika kusaidia sekta hii.

Endapo ningepata nafasi ya kuwa mshauri wa Rais katika masuala yanayohusu sekta ya filamu; ningemuomba afikirie sana kuhusu serikali yake kuanzisha mpango maalum wa kutoa mikopo/ruzuku kwa watengenezaji wasinema ambao hawafikiriwi kabisa na mabenki yetu.

Hii ni kwa sababu, sekta hii inalipa sana na inaweza kuchangia pato la taifa hili iwapo tu sinema tunazotengeneza zitawezeshwa na kutengenezwa kwa umakini zaidi. Ukweli ni kwamba, sinema ikiwezeshwa inaweza kudumu kwenye soko kwa muda mrefu sana (lifetime property), huku mabenki yakimiliki 30% ya hisa na kushikilia (hold) haki ya kumiliki (copyright) sinema hiyo hadi (mkopo) uliotolewa utakapolipwa.

Kwa hiyo, serikali ijayo inapaswa kuziagiza mamlaka husika kuandaa takwimu za kina kuhusu soko la filamu na kuzitazama fursa zilizopo. Ipo haja kubwa kwa Rais ajaye kuifahamu nguvu ya soko letu la filamu (dynamics of the home video industry).

Ni muhimu sana kwa rais ajaye (kama kweli atakuwa na nia ya kuiboresha sekta hii kama alivyoanza kuonyesha rais wa sasa) kuufahamu msingi imara unaohitaji mipango madhubuti na ya lazima katika kuiwezesha (empower) sekta ya filamu hapa Tanzania. Litakuwa jambo la busara zaidi kama Rais ajaye kuwaagiza wasaidizi wake kuuchunguza mfumo unaotumika nchini Afrika Kusini katika kuisaidia sekta ya filamu nchini mwao kupitia chombo maalum cha kusimamia filamu “South African Filmand Video Foundation”. Ikumbukwe kuwa sekta ya filamu inaiingizia Afrika Kusini pato la zaidi ya Rand 7.7 bilioni.

Serikali ijayo inapaswa kuangalia uwezekano wa kuanzisha chombo kitakachokuwa na uwezo wa kuzitangaza kazi zetu kitakachoitwa “Filmand Video Promotions Board”; katika chombo hicho kiwepo kitengo maalum kitakachohusika na utoaji wa taarifa za upatikanaji wa pesa (funding information) na kutoa fursa kwa watengenezaji wa sinema.

Kiwepo kitengo maalum kitakachoandaa takwimu za kina na kutoa fursa ya kuzitangaza kazi zetu katika masoko mengine ya Afrika Mashariki, Kati, Kusini mwa Afrika, na hata maeneo mengine ya dunia na hivyo kuongeza uwezekano wa kuuza kazi zetu kimataifa na hivyo kuigiza pesa za kigeni. Kiwepo kitengo maalum kitakachowalazimisha wadau katika sekta ya filamu kujipatia mafunzo ya fani husika (professionalism). Kiwepo kitengo maalum kitakachosimamia mapato (revenue generation) yatokanayo na filamu. Serikali yoyote iliyofanikiwa katika sekta ya filamu (kwa mfano Marekani) ina kitengo cha aina hii.

Kiwepo kitengo maalum kitakachosimamia kwa ukamilifu sheria za uharamia/wizi (piracy) wa kazi zetu na hivyo kuwafanya watengenezaji wa kazi hizi kutokuwana hofu ya kupoteza mapato (economic reward) yatokanayo na kazi zao. Rais ajaye anapaswa kutambua kuwa, dhumuni la makala yangu si kuitaka serikali yake ituanzishie chombo kingine cha Kiserikali cha maamuzi na ukiritimba (bureaucratic) kwenye sekta hii. Chombo cha aina hii kisiwe kikwazo endapo, kama nilivyotangulia kusema (…kielelezo “paradigm”kutoka kwenye utungaji sheria “legislating” hadi kwenye kuisaidia, kuisimamia na kuitangaza “promoting”sekta ya filamu) ambacho kitakuwa chombo cha maamuzi cha Kiserikali.

Tumeonekanakukosa kabisa malengo (lack of vision). Bila malengo, watu wetu wataangamia kabisa (perish)…Neno “perish” ambalo ndiyo tafsiri halisi ya neno “kuangamia” linatokana na lugha ya Kiebrania (Hebrew) likiwa halina maana ya kuangamia (kufa). Maana yake halisi ni watu kuumbuka (go naked) na kufukarika (kuwa fukara wa kutupwa).

Hata hivyo, hatuhitaji kuielewa lugha ya Kiebrania ili tuweze kuiona hali halisi ya sekta ya filamu hapa nchini ilivyo kwa sasa. Sekta hii imefukarishwa kwa sababu wajasiriamali wa soko la filamu wanafanya kazi kwa nguvu zote kuzalisha sinema lakini hawapati kile wanachostahili kukipata japo kwa uchache. Sekta hii imefukarishwa kwa sababu ukimtazama mtayarishaji wa sinema zaTanzania hana hadhi kabisa ya kuitwa mtayarishaji wa sinema (producer), hasa unapoangalia suala la mapato na ushawishi wake kisiasa (political influence).Tutaendelea hivi hadi lini na mchezo huu wa kumtafuta mchawi na kutupiana lawama (blame game)? Serikali haitusaidii, mabenki hayatukopeshi, na soko lenyewe limeparaganyika… blah,blah,blah…

Lakini, inatupasa sote kutafuta tafsiri halisi ya neno malengo (vision) na mapato (economically rewarding) katika kuandaa mwongozo (roadmap) utakaotuongoza kwenye mafanikio ya soko letu. Kwa msaada kutoka serikali, tunahitaji kuwa na vyombo madhubuti katika kusimamia kazi zetu. Vyombo kama Copyright Society of Tanzania (Cosota), TRA, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), n.k. vinahitaji kuangaliwa upya kwa makini ili viweze kwenda na wakati na kusimamia kazi zetu kikamilifu.

Uwezo halisi wa kufanya kazi kwa uthabiti ni kuwekeza nguvu kwenye malengo ‘vision’ katika kuangalia jinsi tulivyoamua kuisukuma mbele ajenda hii kisiasa. Tunahitaji sekta hii ya filamu kuchukuliwa kama sekta nyeti sana, kwanza na Rais, Serikali yake kupitia kamati za mipango, na Bunge la Jamhuri. Tunahitaji Rais, Mawaziri, Wabunge, na Wakuu wa Idara ambao hawataishia tu kusifia kazi zetu kwenye hotuba zao (tunawasikia sana wakati huu wa kampeni) na kuonesha kutambua umuhimu wa sekta hii; tunahitaji wataalamu (professionals) watakaopata mamlaka ya kisiasa, kuhimiza utungaji wa sheria na kuzisimamia kikamilifu, na kuhakikisha kuwa tunakuwa na nyenzo bora zitakazosaidia katika kuboresha maendeleo ya sekta hii.

Sekta hii ni muhimu sana. Ni kuichukulia sekta hii ya filamu kwa umakini zaidi kisiasa (seriously politically). Ili kauli za Rais Kikwete zitimie, Rais ajaye anapaswa kuanzisha makubaliano maalum ya kisiasa (political consensus) yatakayokuwa na ajenda kuu ya kuhakikisha kuwa wadau pamoja na sekta nzima ya filamu nchini vinakua, kisiasa na kiuchumi.

Naomba kutoa hoja.

No comments: