Sep 21, 2010

Ripoti ya warsha ya TAIPA


Yustus Mkinga, Mtendaji Mkuu wa Cosota

TAARIFA YA WARSHA KUHUSU WIZI WA KAZI ZA SANAA ILIYOFANYIKA UKUMBI WA KITUO CHA UTAMADUNI CHA UFARANSA ALHAMISI TAREHE 19 AGOSTI 2010

Chama cha Watengeneza Filamu na Vipindi vya Luninga na Radio (TAIPA)/UMOJA AUDIOVISUAL E.A. LTD/ na KITUO CHA UTAMADUNI CHA UFARANSA (ALLIANCE FRANCAISE), waliandaa warsha juu ya WIZI WA KAZI ZA SANAA “COPYRIGHT INFRINGEMENT (PIRACY)” iliyofanyika siku ya Alhamisi tarehe 19 Agosti 2010 kuanzia saa 3 asubuhi katika ukumbi wa Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa.



Warsha hiyo ilihudhuriwa na washiriki 40 kutoka taasisi/wakala wa serikali, kampuni, vikundi vya sanaa, wasanii binafsi na vyombo mbalimbali vya habari.


John Lister Manyara akiwa kazini, 
anayeonekana kwa mbali ni Simon Mwapagata (Rado)

Watoa mada kutoka wawakilishi wa sanaa ya muziki, filamu, COSOTA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Tume ya Ushindani na (Fair Competition Commission); wote walionesha umahiri na uelewa wa hali ya juu kwa kila mada walizoziwasilisha kuhusiana na kadhia ya wizi wa kazi za sanaa. Mwakilishi wa chama cha kutetea haki za waandishi, wachapishaji na wachapaji (KOPITAN) alipewa fursa ya kukitambulisha chama hicho ambacho kimeanzishwa hivi karibuni ili kusimamia haki zao. Washiriki wote walijifunza mengi juu ya hatua zinazochukuliwa na taasisi/wakala wa serikali, kampuni, vikundi vya sanaa, wasanii binafsi na vyombo mbalimbali vya habari ili kulinda haki za kazi hizo za sanaa.

Hata hivyo, mbali na juhudi hizo, bado kulidhihirika kwamba nguvu zaidi zinahitajika katika kufanikisha mapambano ya kuwakomboa wasanii, watengenezaji na wasambazaji wa kazi za sanaa ili wapate malipo/mapato stahiki kutokana na kazi zao. Katika kuhitimisha warsha hiyo maazimio kadhaa yalipitishwa na washiriki, nayo ni:


Sehemu kubwa ya umma – wakiwemo wasanii wenyewe - haijuwi chochote kuhusu COSOTA wala Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, hivyo basi washiriki waliiomba COSOTA kuendesha kampeni kamambe nchi nzima ili kuuelimisha umma pamoja na wasanii kuhusu Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki. Vyombo vya habari (luninga, redio na magazeti) navyo pia viliombwa kufanya kazi hiyo kama moja wapo ya majukumu ya vyombo hivyo katika kuuelimisha umma. Elimu hiyo pia ijumuishe masuala ya madhara ya kununua kazi feki za wasanii – muziki, filamu na machapisho mbalimbali ambayo, mbali na kutokuwa na ubora wa viwango, lakini pia husabisha kukosekana kwa mapato stahiki (kodi) kwa upande wa serikali na (mrahaba) kwa upande wa wasanii.


COSOTA ishirikishwe katika vituo vya forodha (bandarini na mipakani) katika uingizaji bidhaa za kazi za sanaa nchini kama vile zinavyoshirikishwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (Tanzania Food and Drug Authority) kwa bidhaa za chakula na dawa; Shirika la Viwango Tanzania (Tanzania Bureau of Standards) kwa bidhaa zenye viwango vinavyotambulika kimataifa; pamoja na Tume ya Ushindani wa Biashara (Fair Competition Commission – FCC) kwa bidhaa bandia. 


COSOTA au BASATA wasajili na kutoa leseni kwa maduka/maktaba yanayouza/kukodisha CD/DVD za muziki/filamu, vibanda vya “kideo” vinavyoonesha sinema na majumba ya starehe/kumbi zinazopiga muziki.
 

Kwa kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (Tanzania Revenue Authority) imepata mafanikio makubwa katika kukusanya kodi kwa upande wa sigara na pombe kali kutokana na kuamuru matumizi ya ukanda wa lakiri (Bandroll/hologram) kwa watengenezaji/waagizaji wa bidhaa hizo, washiriki walipendekeza ama TRA au COSOTA waanzishe utaratibu huo huo kwa kazi za sanaa. Hii itasaidia kupambanua kati ya bidhaa (CD/DVD) halisi na zile feki. 

Kutokana na vitisho dhidi ya maisha ya watendaji wa serikali na taasisi zake
(COSOTA/TRA/FCC) wakati wa kufanya misako ya bidhaa feki, serikali ihakikishe inawapatia ulinzi madhubuti na wa kutosha watendaji hao na isiwe na huruma kwa maharamia hao wanaodiriki hadi kuwatishia maafisa wake.
 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (Tanzania Revenue Authority) ilipendekeza wasanii wote wasajili kazi zao pamoja na thamani ya kazi hizo na Mamlaka hiyo ili wakati wa kufanya msako iwe rahisi kutambua bidhaa zilizosajiliwa na zile zisizosajiliwa pamoja na thamani ya kazi hizo. Hii itawezesha TRA kupata thamani halisi ya kazi hizo kwa ajili ya kutoza kodi na pia kutoa adhabu kwa wale wanaoiba kazi za wasanii.
 

Wasanii wote wasajili kampuni au taasisi zao kisheria ili iwe rahisi kutambuliwa na serikali pamoja na taasisi zake.
 

Kuishajiisha serikali kuhuisha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ili adhabu kali zitolewe kwa wezi wa kazi za sanaa kwani kwa sheria ilivyo sasa, adhabu zinazotolewa ni ndogo sana kiasi kwamba maharamia wanaoiba kazi hizo hawashindwi kumudu kuzilipa.
 

Kuihimiza serikali kuhakikisha kwamba Jeshi la Polisi na Mahakama wanasimamia sheria hizo kwa ukamilifu.
 

Wasanii, watengenezaji na wasambazaji wa kazi za sanaa walihimizwa kupunguza gharama za uzalishaji bidhaa hizo ili bei nayo ipunguwe kwa mlaji wa mwisho katika kukabiliana na ushindani wa bidhaa feki – ambazo kutokana na ubora wake hafifu, bei za bidhaa hizo nayo huwa chini. Bidhaa feki pia husababisha wasanii kukata tamaa kwani huona jasho lao halilipi na hivyo huacha shughuli hizo na kuua vipaji vyao.
 

Jeshi la Polisi lisiwe linawakamata watengenezaji na wasambazaji wa kazi feki tu, bali pia liwakamate watumiaji (walaji) wa kazi hizo pale wanaponunua bidhaa hizo, ili kupunguza, kama siyo kuondoa kabisa mahitaji (market demand) ya bidhaa feki.
 

Kama Tume ya Ushindani wa Biashara (Fair Competition Commission – FCC) inaweza kukamata makontena kwa makontena ya bidhaa bandia wakati yakiingizwa nchini kupitia vituo vya forodha ( bandarini na mipakani), kwenye maghala ya kuhifadhia mizigo na mpaka madukani na kuziteketeza bidhaa hizo, kwa nini wasifanye hivyo kwa bidhaa za kazi za sanaa ( DVDna CD) za filamu na muziki? Suala la bidhaa feki limesambaa sana katika kazi za sanaa – kwa mfano: DVD na CD za filamu na muziki zinazoingizwa nchini kutoka nchi za mashariki ya mbali. Wasanii, watengenezaji na wasambazaji wa kazi za sanaa wanahimizwa kushirikiana kwa karibu sana na Tume ili kukabiliana na wizi wa kazi hizo.
 

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lisimamie kwa karibu sana ili kuona kwamba mbali na kuwasajili wasanii kama linavyofanya hivi sasa, lakini pia liwasajili na kutoa leseni kwa watengenezaji na wasambazaji wa kazi za sanaa.
 

Wasanii wenyewe wahakikishe wana elimu ya kutosha kuhusu tasnia zao – filamu, muziki, uandishi, uchoraji na kadhalika; Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki na wafuate maadili ya taaluma zao ili kazi wanazotengeneza ziwe za viwango vya juu, na hivyo basi kuvutia katika soko, siyo la ndani tu, bali hata ziweze kuuzwa katika soko la nje ya nchi.

Kwa kuwa suala hili la wizi wa kazi za sanaa limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu sasa; na kwa kuwa hakuna mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na juhudi hizo ambazo hata hivyo zinastahili pongezi kwa taasisi/wakala wa serikali, kampuni, vikundi vya sanaa, wasanii binafsi na vyombo mbalimbali vya habari, hivyo basi ninatoa rai kwenu washiriki kwamba kilio chetu juu ya wizi wa kazi za sanaa tukifikishe kwa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kumuomba aziongezee nguvu juhudi zinazofanywa na vyombo mbalimbali vya dola katika kupambana na wizi wa kazi za sanaa, kwani mbali na mapungufu kadhaa ya kisheria na kiutendaji, moja ya maelezo katika warsha hiyo ilikuwa kwamba watendaji wa serikali wamejikuta wakitishiwa hata maisha yao na maharamia hao, katika utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za majukumu yao.

Katika hotuba yake ya kuvunja bunge aliyoitoa huko Dodoma tarehe 20 Julai 2010, chini ya kipengele cha “Michezo, Burudani na Utamaduni” Rais alinukuliwa akisema, pamoja na mambo mengine kwamba: “... Hivi sasa tumelipia mtaalamu mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam asaidie kutengeneza njia bora ya kusambaza kazi za wasanii wa muziki na filamu ili wapate malipo halali kwa jasho lao. Mafanikio ya zoezi hili yatatufundisha namna ya kuwasaidia wasanii wa fani nyingine pia ...”

Hivyo basi, ninashauri kwamba tumuandikie barua Mheshimiwa Rais ya kumshukuru kwa juhudi zake na serikali anayoiongoza kuhusu kutengeneza njia bora ya kusambaza kazi za wasanii wa muziki na filamu ili wapate malipo halali kwa jasho lao, lakini pia kumuomba, kama alivyosimamia suala la mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake wa awamu ya kwanza, basi aongoze na asimamie kidedea suala la kupambana na wizi wa kazi za sanaa. Naomba mnipe mawazo/maoni yenu kuhusu pendekezo hilo.

Naomba kuwasilisha.

Wenu,

Said A. Ibrahim
Katibu - TAIPA

No comments: