Dec 12, 2012

Kurasmisha sekta ya filamu/muziki sawa lakini kwa hili la stempu tunakurupuka


Afisa Utafiti Mwandamizi wa TRA, Ephraim Mdee, akielezea
kuhusu stempu maalum zitakazoanza kutumia mwakani

BADO naikumbuka hotuba ya Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, aliyoitoa katika kikao cha bunge la bajeti kwa mwaka 2012/13, pale aliposema: “Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-
“Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wasanii kudurufiwa kazi zao za sanaa na kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya. Ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato itaanza kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu kwa nia ya kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo vya kudurufu kazi za sanaa hali ambayo inadumaza ukuaji wa sanaa na vipaji hapa nchini.
“Aidha, Mamlaka ya Mapato itaweka stampu kwenye bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi na kuwawezesha wasanii kupata kipato stahili kutokana na kazi zao. Vilevile hatua hii itaiingizia serikali mapato. Kwa kuwa yanahitajika maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa hatua hii utaanza rasmi tarehe 1 Januari, 2013…”

Kauli hii ilinifanya kuona kuwa angalau sasa serikali imeanza kuonesha kuutambua mchango wa sekta ya burudani (filamu na miziki) hapa nchini. Ikumbukwe kwa miaka mingi sasa, wasanii na watengenezaji wa sinema miongoni mwa wadau wengine wa sekta ya burudani wamekuwa wakitoa sinema ili kujipatia riziki kutokana na kazi yao bila mafanikio.

Mwanzoni niliamini kabisa kuwa kauli ya waziri iliashiria kuwa Serikali imekusudia kusaidia sekta ya burudani ikue na kuleta tija kwa nchi yetu, na nilidhani imechelewa kutolewa lakini baada ya kufuatilia kwa makini zoezi zima la matayarisho kuelekea kwenye uwekaji stampu maalum kwenye kazi za sanaa litakaloanza Januari Mosi, 2013, nimekuwa na wasiwasi kama kweli serikali kupitia taasisi zake wanaifahamu nguvu ya soko la filamu na muziki.

Nilihudhuria semina moja iliyofanyika siku za karibuni katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Peacock, ambapo mwakilishi wa TRA alikuwepo na kuelezea jinsi ambavyo mamlaka hiyo ilivyojiandaa kushughulikia suala la stempu maalum katika kuhakikisha wasanii wanafaidi jasho lao.

Taarifa za mamlaka zimetawanywa wiki hii kwenye vyombo vya habari kupitia kwa Afisa Utafiti Mwandamizi wa TRA, Ephraim Mdee, kuwa mamlaka itaanza kuzishughulikia kazi ambazo hazina stempu maalum kuanzia Januari Mosi mwakani, na kwamba uzalishwaji, usambazwaji, uingizwaji kutoka nje, uuzaji, utumiaji au ununuaji wa bidhaa za tasnia za filamu na muziki nchini kama vile CD, DVD au kanda zisizo na stempu maalum za kodi litakuwa ni kosa la jinai na hivyo wahusika watachukuliwa hatua kali! Eti lengo likiwa kukomesha wizi kupitia udurufishaji wa nakala bandia na hii itasaidia kuinua pato la nchi na kuwanufaisha wasanii kutokana na jasho lao!

Hivi, ni nani aliyewaambia kuwa piracy (uharamia) ndiyo tatizo pekee lililopo katika soko la filamu na muziki nchini? Hivi stempu hizi katika mazingira ya soko la sasa zitasaidia nini kutibu matatizo kwa maendeleo ya sekta ya burudani? Hivi TRA wanajua kuwa sekta ya filamu imefukarishwa kwa makusudi na watu wachache kwa maslahi binafsi, tena hata baadhi ya viongozi wa serikali na taasisi zake wakiwemo?

Je, wanaelewa kuwa utengenezaji wa filamu kwa soko la Tanzania unatafsiriwa kuwa sawa na biashara ya barafu inayoweza kumyeyukia aliyenayo mikononi wakati wowote? Hali hii huwafanya watengeneza filamu wa Kitanzania wajikute wakiingia mikataba haraka ya kupata pesa japo kiduchu kabla barafu haijawayeyukia na kugeuka maji? Wakati mwingine bila hata kurudisha gharama walizoingia!

Sijaelewa kama TRA wana lengo la kuisaidia sekta ya filamu na muziki na wakati huohuo kuongeza pato la nchi au lengo lao ni kujipatia pato litakalowafanya wafikie lengo walilowekewa na rais na mwisho wa siku wasifie kuvukaa lengo! Maana nawaona wanawekeza nguvu kubwa kuhakikisha stempu zinatengenezwa na kuanza kutumika badala ya kuwekeza nguvu kubwa katika kutoa elimu kwa wasanii na wanunuzi wa kazi za sanaa.

Niliongea na wasanii kadhaa, tena kati yao wakiwa ni wasomi walioonesha kufurahishwa sana na mpango huu wa TRA wa kuweka stempu, wakielekeza matumaini yao kwa TRA kuwa itafanya kazi ya kulinda haki za wasanii, wakisahau kuwa TRA kazi yake ni kukusanya kodi tu. Sasa kama elimu haijatolewa tutakuja kuingia kwenye mgogoro mkubwa sana kwa wasanii kudhani kuwa kazi zao zinalindwa na TRA.

Tusidanganyane, hakuna mnunuzi wa kazi za sanaa Tanzania anayenunua kwa kutazama stempu. Kwanza kazi hizi zinanunuliwa na watu wa tabaka la chini, na wala si wale wa tabaka la kati na la juu ambao wala hawana habari nazo. Hivyo elimu ni muhimu sana kutolewa kwa wanunuzi katika kuzitambua hizi stempu maalum, na kujua umuhimu wa kununua kazi halisi.

Ki ukweli, Mpango huu wa TRA umebeba maswali mengi kuliko majibu. Hivi wanadhani stampu za TRA pekee zinatosha kuleta ufanisi katika soko la filamu bila hata kuijua nguvu ya soko? Mbali na stampu hizi je, kuna mikakati gani katika kudhibiti kazi zisizo na mhuri? Je, mlaji atatofautisha vipi mhuri halali na batili? Hivi hawadhani kuwa ili zoezi hili lifanikiwe inahitajika elimu kwa walaji?

Ni mechanisim gani itakayotumika kuweza kutekeleza hilo na je, msanii atahakikisha wapi kipato chake? Kwenye stampu au wapi? Nasema hivi kwa kuwa hata kazi feki nayo inaweza kuwekewa stampu na atakayenufaika ni msambazaji na TRA wala si msanii!

Hapa TRA wanataka kuvuna pasipo kupanda kwa kutotaka kuwekeza kwanza, sijui ni kwanini wanakimbilia kutaka kukusanya wakati hawajaweka miundombinu mizuri ya soko la kazi za sanaa. Unatozaje kodi kwa soko la ovyo lisilo na uhakika ambalo hujaliweka na wala huijui nguvu yake? Nina uhakika kwa kile ninachokisema na ninachokiona hapa ni sawa na kutaka kumkamua ng’ombe maziwa pasipo kumlisha. Matokeo yake ng’ombe atakufa na hata hayo maziwa kidogo hayataonekana.

Mfumo wa biashara ya filamu nchini umekaa kienyeji sana. Sijui Mamlaka ina mpango gani katika kuandaa miundombinu ya soko la filamu/muziki ili wasanii na watengeneza filamu pia wafaidi jasho la kazi zao tofauti na ilivyo sasa? Hivi wakisharasimisha sekta hii, serikali itawekeza au ndiyo itaingia kwenye mpango ninaousema wa kuvuna pasipo kupanda? Sidhani kama itakuwa busara kwa serikali (kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania) kukusanya mapato wakati haijengi miundombinu ya soko, haijengi shule zitakazowasaidia wadau wa filamu kujiendeleza, na wala haisaidii katika kutafuta soko!

Hapa hata wakikusanya kiasi gani, bado haitawasaidia wasanii kama elimu kwa wasanii na wadau wengine haitatolewa. Hivi wamewahi kujiuliza; kuna vyuo vingapi vinavyofundisha filamu nchini? Hawadhani kuwa sheria hii waliyopitisha itaishia kumbana msambazaji/muuzaji kuhakikisha analipa kodi lakini haitamsaidia mtayarishaji/msanii ambaye ataendelea kunyonywa kama kawaida?

Ukiiangalia kijuujuu utadhani ni jambo zuri, lakini ukweli serikali kupitia TRA inatengeneza bomu kwa tasnia ya burudani, bomu ambalo limeleta mgogoro mkubwa katika nchi ya Ghana sababu ya msingi ikiwa ni ndogo tu, kazi ya Mamlaka ya Mapato si kulinda haki za wasanii bali ni kukusanya kodi. Kazi ya kulinda haki hizi iboreshwe katika vyombo vya wasanii husika ili TRA iweze kupata takwimu sahihi za kukusanya kodi.

Mi nadhani ili kuleta ufanisi katika sekta hii walipaswa kwanza kuandaa takwimu za kina kuhusu soko la filamu/muziki na kuzitazama fursa zilizopo kabla ya kuamua chochote. Walipaswa pia kushirikiana na taasisi zingine za serikali kuandaa sera nzuri ya filamu itakayosimamia mambo haya kwa kivtendo. Kwa kufanya haya, pia walipaswa kushirikiana na wadau na jopo la wataalam watakaoangalia kanuni zilizopo kwa lengo la kuoanisha na kuhuisha kiini cha sera mpya ya filamu. Sera ya filamu ndiyo hati pekee yenye kueleza kwa ufasaha uwezekano mbalimbali katika kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa filamu.

Sera hii inapaswa iende mbali zaidi ikizingatia mchakato wa utoaji wa filamu na uanzishwaji wa haki za usambazaji wa miliki. Katika mchakato huu, wasambazaji wanapaswa kuwasilisha ripoti ya kila wiki ya kisheria katika shughuli zao za usambazaji ambayo inaweza kutumiwa katika kutathmini utendaji wa kifedha wa filamu. Lakini pia wawekewe mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao.

Nitashangaa kama TRA watakana kuwa hata hizo DVD zinazoitwa za wizi huwa hazilipiwi kodi TRA. Zinalipiwa kwa kisingizio cha wao hawajui kipi halali na kipi si halali, kwa msingi huu TRA wamekuwa wanakusanya kodi ya kazi za wizi za wasanii siku zote. Wanatuhakikishiaje kuwa mchezo huu hautakuwepo tena?

Kurasimisha sekta ya filamu/muziki ni sawa, lakini tujipe muda kwanza kwenye hili suala la stempu na kuelekeze nguvu kwenye kutoa elimu kwanza na kuandaa sera nzuri ya filamu, vinginevyo tujiandae kuizika rasmi tasnia ya filamu/muziki.

Alamsiki…

No comments: