Jan 1, 2010

Nawatakia wote Heri ya Mwaka Mpya, 2010Naitwa Bishop John Hiluka (nilizaliwa siku ya Alhamisi, Machi 26, 1970, siku tatu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, saa kumi na moja alfajiri), ni Mtanzania Muongozaji wa Filamu, Mwandishi wa Miswada ya Filamu (Scriptwriter), Mchoraji wa picha za hadithi (Comic Artist), Tabibu (Medical Personnel), Mtaalam wa sauti (Sound Expert) na Mtafiti ambaye nina uzoefu mkubwa katika ubunifu na uandishi kwa ajili ya sinema na uongozaji wa sinema. Nimeshiriki kama Mshauri, Muongozaji, Mwandishi wa Miswada ya Filamu, Meneja Uzalishaji, Mbunifu, Mtaalamu wa sauti nk katika miradi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 10.

Bishop J. Hiluka

Maisha ya awali

Nlizaliwa katika Hospitali ya Wamisheni ya Ndala iliyopo katika Wilaya ya Nzega, Tabora, kutoka kwenye familia ya baba Mngoni na mama Mnyamwezi. Mama yangu, Catherine Kimwaga (alizaliwa 15 Februari 1945 na kufariki ghafla tarehe 20 Desemba 2004 akiwa safarini akitokea Dar es Salaam kuelekea Tabora) alikuwa mfanyakazi wa Hospitali wilayani Nzega. Baba yangu Mzee Alex M. Hiluka, pia alikuwa tabibu kabla hajajikita kusomea masuala ya.lishe na kuwa Afisa Mtaalam wa Lishe na Mkuu wa Idara ya Lishe, Makao Makuu katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, jijini Dar es Salaam.