Nov 11, 2013

KWA KUANDAA MAFUNZO: Wasanii mkoani Iringa wanapaswa kuigwa


Mmoja wa wasanii mjini Iringa akikabidhiwa cheti cha kuhitimu mafunzo na Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba

ILIONEKANA kama masikhara, wengi waliwabeza, hata rafiki zao waliona kuwa walichokuwa wakikifanya ulikuwa ni upuuzi mtupu. Hatimaye siku zikaanza kujongea taratibu, mara wiki, mbili, hadi ukatimia mwezi tangu waanze kuchukua mafunzo yaliyobeba dhana nzima ya kujitambua, kujifunza misingi ya uigizaji, uandishi, uongozaji na utayarishaji wa filamu.

Mafunzo haya ya mwezi mmoja yaliandaliwa na Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Tanganyika Center for Development and Advocacy (TCDA) ya mjini Iringa na kufadhiliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Fredrick Mwakalebela. Taasisi hii ni matokeo ya vijana wawili waliomaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani tofauti na kukumbana na changamoto za ajira baada ya kurudi mtaani. Moja ya malengo ya Taasisi hii ni kuwaelimisha vijana umuhimu wa kujiajiri kwa kutumia fursa zilizopo.