UONGOZAJI wa filamu ni
zaidi ya kujua “standby... action... cut!” Uongozaji wa filamu ni tatizo kubwa mno
kwenye tasnia ya filamu nchini, ni tatizo kwa kuwa waongozaji wetu wa filamu hudhani
kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua “standby... action... cut!” na
kusahau kuwa muongozaji wa filamu anapaswa kuwa mbunifu na kiungo muhimu kati
yake na timu ya uzalishaji.
Muongozaji wa filamu anawajibika
kuutafsiri muongozo wa filamu ulioandikwa kwenye karatasi na kuuhamishia katika
picha halisi na sauti kwenye skrini – na anapaswa kuiona taswira halisi na
kutafsiri mtindo na muundo wa filamu hiyo, na hivyo kufanya kazi zote mbili
kama kiongozi wa timu na msimulizi kwa kutoa picha halisi. Pia anapaswa
kuangalia mtu anayefaa kuigiza, ndiyo maana mojawapo ya majukumu ya muongozaji
ni pamoja na kufanya usaili (casting).